WINGU zito limetanda kuhusu afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison
Mwakyembe baada ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda,
kusema kuwa ripoti ya ugonjwa wa Mwakyembe, anayo mwenyewe na kwamba
wizara haina ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, Robert
Manumba, kwa waandishi wa habari.
Lakini wakati Dk Mponda akitoa
kauli hiyo, baadhi ya watu wa kada tofauti wakiwamo viongozi wa dini na
wasomi, wamekosoa ripoti hiyo ya polisi.
Mmoja wa watu hao,
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod
Slaa alisema,"hata mimi simwamini Manumba."
Malumbano hayo
yanakuja wakati Dk Mwakyembe ambaye ni pia ni Mbunge wa Kyela,
akitarajiwa nchini jana kwenda India kwa matibabu katika Hospitali ya
Apollo.
Mahojiano na Waziri Mponda
Gazeti: Salaam
Mheshimiwa waziri. Nimekupigia kutaka ufafanuzi kuhusu ripoti
iliyotolewa na DCI Manumba kuhusu ugonjwa wa Dk Mwakyembe. Ninyi wizara
mnaitambuaje?
Waziri: Kiutaratibu ripoti ya daktari ni ya
mgonjwa. Sisi hatujaandika ripoti, muulizeni DCI Manumba awape ufafanuzi
kama kuna kitu mnataka kuuliza zaidi kwa alichokizungumza na ninyi
waandishi.
Gazeti: DCI Manumba alitoa taarifa kwa waandishi
lakini aki-refer (rejea) ripoti kutoka wizarani (afya), baada ya
kuwasiliana nanyi, kwa nini wewe usiizungumzie?
Waziri: Narudia tena, muulizeni yeye DCI au Dk Mwakyembe mwenyewe, wao wanaweza kuwapa ufafanuzi.
Gazeti:
Tayari Dk Mwakyembe mwenyewe amekwishatoa tamko kwamba ripoti
iliyosomwa na polisi, haina uhusiano na ripoti aliyokuwa nayo yeye
kuhusu uchunguzi wa maradhi yake. Je, ripoti hii ya polisi ambayo
wamedai wameipata kwenu (wizara) mmeitoa wapi?
Waziri: Ni hivi,
baada ya daktari kumchunguza mgonjwa, hutoa ripoti na kumpa mgonjwa. Kwa
hiyo, ripoti ya Hospitali ya Apollo anayo Dk Mwakyembe mwenyewe. Tena
yeye kaeleza vizuri kabisa kwamba hata uchunguzi bado unaendelea. sasa
hapo mnataka niseme nini tena?
Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk
Mwakyembe mwenyewe na tayari amesema ripoti ya polisi waliyosema
imetoka kwenu siyo sahihi, je wizara iliwahi kupata ripoti ya Hospitali
ya Apollo.
Waziri: Sisi tulichokifanya ni kumpa rufaa Dk
Mwakyembe kwenda India. Ripoti hadi sasa anayo mwenyewe ingawa huwa
tunapata taarifa baada ya yeye mgonjwa kuzileta kwetu. Hizo ndizo kanuni
za taaluma ya udaktari, kwa hiyo ripoti anayo mwenyewe.
Gazeti: Sasa kama ripoti anayo Dk Mwakyembe mwenyewe, hii iliyosomwa na DCI imetoka wapi?
Waziri:
Kumbuka DCI ana njia zake nyingi za kupata taarifa. Kwa hiyo ndiyo
maana nasisitiza, muulizeni mwenyewe awape ufafanuzi kwa aliyozungumza
na waandishi. Sisi wizara mnatuonea tu.
Gazeti: Lakini, hata kama
ugonjwa ni siri, huoni mheshimiwa waziri kwamba kuna haja ya kuondoa
utata kuhusu suala hili ikizingatiwa kuwa Dk Mwakyembe ni kiongozi
anayegusa hisia za watu tofauti?
Waziri: Wanaoweza kuzungumzia
maradhi yake, ni familia yake au yeye mwenyewe kwani ndiye mwenye
ripoti. Mtafuteni au iulizeni familia yake iwapatie majibu. Lakini
wizara haiwezi kufanya hivyo. Narudia tena, kuhusu hilo la DCI muulizeni
mwenyewe awape ufafanuzi, mimi sijaona ripoti ya DCI aliyozungumza na
waandishi wa habari.
Alichosema DCI
Akizungumza na
waandishi mwishoni wa wiki iliyopita, Manumba alisema, “ukweli kuhusu
kauli hiyo inayodai kuwekewa sumu, tumeupata baada ya kuwasiliana na
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambayo nayo imewasiliana na hospitali
aliyokuwa amelazwa Dk Mwakyembe nchini India. Taarifa zinaonyesha kuwa
hakuna sumu."
Jana, alipoelezwa kwamba Dk Mwakyembe ameikana ripoti yao, Manumba alisema "sasa suala hilo litashughukiliwa kisheria."
Alisisitiza
kuwa suala hilo litashughulikiwa kwa kufuata misingi ya kisheria na
kwamba, Jeshi la Polisi haliko tayari kuendeleza malumbano kupitia
vyombo vya habari.
"Hatua zaidi zinachukuliwa dhidi ya jambo
hilo, kwa sasa litashughukiliwa kwa kufuata misingi ya kisheria kama
nilivyokwishaeleza awali,"alisema Manumba.
Kauli ya Dk Mwakyembe
Juzi,
akitoa tamko baada ya kukerwa na kauli ya Jeshi la Polisi alisema
mbunge huyo alisema ‘napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake
waliisoma taarifa halisi ya matibabu yangu au walisoma taarifa
“nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”!
"Nasema
hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa waandishi wa habari,
hakifanani kabisa na picha iliyoko kwenye taarifa halisi ya Hospitali ya
Apollo inayotamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea
hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua,
kukidhibiti au kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na
mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”,
“hakulishwa sumu”
Dk Mwakyembe pia alitoa sababu kuu tatu za kupinga ripoti o ya DCI akisema:
"Kwanza,
kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu
kiini chake, unaoendelea katika Hospitali ya Apollo, nchini India,
ambako bado sijahitimisha matibabu yangu, pili kwa ufinyu wa uelewa
unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa
“sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru,
inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu.
Alisema sababu ya tatu ni
kitendo cha Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban
mwaka mzima sasa, halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au
kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Dk Slaa
Akizungumzia
sakata hilo, Dk Slaa alisema hana imani na ripoti ya uchunguzi
iliyofanywa na Jeshi la Polisi na kutolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai, kuhusu hali ya Mwakyembe.
"Mimi siwezi
kuzungumzia ugonjwa wa mtu, lakini niseme tu kwa kifupi kuwa ripoti ya
DCI Manumba siwezi kuiamini. Sina imani na Manumba kwa sababu mimi
mwenyewe imenitokea,"alirusha kombora kwa Manumba.
"Niliwekewa
vipaza sauti kwenye kitanda changu mjini Dodoma, taarifa za tukio hilo
zilifika kwake lakini hadi leo hajatoa majibu yoyote ya uchunguzi wake,"
alisisitiza.
"Nani asiyemfahamu Manumba ndiye alishuhudia watu
50 wakipoteza maisha kwa kufukiwa mgodini na kesi ikaenda mahakamani,
ikafutwa, Kwa nini Serikali yetu inamweka mtu wa aina hiyo kwenye nafasi
kubwa kama hiyo," alihoji Dk Slaa.
Alisema hata katika tukio la kuwekewa vinasa sauti kwenye kitanda huko Dodoma, hakuwahi kuitwa na kuhojiwa.
Askofu Ruwa'ich
Akizungumzia
mvutano huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Yuda Thadeus
Ruwa'ichi, alisema kinachoendelea kati ya jeshi na Dk Mwakyembe, ni
ishara ya kutosha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji.
"Malumbano
hayo yanaonyesha kuwa taifa liko kwenye ubabaishaji na hiki siyo kitu
kizuri. Ushauri wangu turudi na kuwa wakweli, tufanye kazi kwa
uadilifu,"alisema askofu Ruwa'ichi.
Rais huyo wa TEC, pia
aliwataka waandishi wa habari kufanya uchunguzi wao na kutoa taarifa za
kubaini ukweli kuhusu jambo hilo, ili kuondoa utata uliopo.
Jukwaa la katiba
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba alielezea kushangazwa kwake juu ya
nguvu aliyopata Manumba ya kupishana na mawaziri.
Alisema
kinachotakiwa ni jopo la madaktari bingwa wa nchini, kuunda tume ili
kuja na jibu litakalowawezesha wananchi waache kuihofia Serikali.
"Mabishano
baina ya viongozi wa Kikwete (Rais), yanaonyesha dhahiri kwamba
Serikali ina ulegevu, unaotokana na kiongozi wake mkuu kukaa kimya,"
alisema.
Kibamba alisema wakati umefika kwa Rais wa nchi kujitokeza
hadharani na kuwawajibisha mawaziri, kama anaamini kuwa yanayoongelewa
ni ya uwongo.
“Kilichoelezwa na Manumba hakiingii akilini kwa
mwananchi wa kawaida, hii nchi sasa ni ya kisanii maana umegeuka mchezo
wa Bongo land wa kuongea bila kuthitibishwa na madaktari
bingwa,”alisema.
“Afya za mawaziri si suala la siri hasa
ikizingatiwa kuwa wanatumia fedha za Watanzania katika kutibiwa . Kama
kiongozi anataka kuweka siri aondoke kwenye uongozi atumie fedha zake,”
alisisitiza.
“Siamini kama DCI Manumba ni daktari , kinachotakiwa
ni kuundwa jopo la madaktari bingwa na Rais kuwaeleza Watanzania
kinachowasibu viongozi wake,” aliongeza.
Alisema Watanzania wanaamini kuwa Dk Mwakyembe alilishwa sumu na kwamba ni vema Serikali ikaondoa mkanganyiko huo.
Akizumngumzia
sakata hilo kwa njia ya simu, Mbunge wa Nyamagana, jijini Mwanza,
Hezekiah Wenje alisema ni dhahiri kwamba kuna kitu ambacho Jeshi la
Polisi linakificha.
“Hali halisi inaonyesha wazi kuwa kuna
ukweli mwingi unaofichwa na Jeshi la Polisi na ndiyo maana kunakuwa na
upotoshaji wa wazi,” alisema Wenje.
Mbunge huyo alisema kuna haja sasa ripoti ya madaktari kuwekwa wazi ili watu wajue.
Kwa
upande wake, wakili wa kujitegemea mkoani Mwanza, Stephen Magoiga
alisema Jeshi la Polisi, linaonyesha wazi kwamba lina matatizo makubwa
ya kiutendaji linapotaka mlalamikaji kuwasilisha ushahidi.
Akikumbushia
Dk Mwakyembe kudaiwa ushahidi alipopeleka malalamiko yake juu ya maisha
yake kuwa hatarini, Magoiga alisema ushahidi ni suala la kitaalamu
ambalo si mtu yoyote anaweza kukusanya.
“Jeshi la Polisi ndilo
lenye utaalamu wa kukusanya ushahidi na wanalipwa kwa kazi hiyo, sasa
wanapodai mlalamikaji alete ushahidi na baadaye kupingana na madai yake,
ni dhahiri kwamba jeshi hilo linasema uwongo,” alisema Magoiga.
Alisema
polisi wanapaswa kufanya kazi kisayansi kwa kuzingatia kwamba tuhuma za
Dk Mwakyembe kulishwa sumu zimetolewa mara ya kwanza na mtu mzima
mwenye hadhi yake katika jamii ya Kitanzania.
Alisema ni jambo la
kushangaza kuona polisi wakioonyesha dharau za waziwazi kwa tuhuma
zilizotolewa na mtu kama Waziri Samwel Sitta.
“Kama kauli ya Sitta inaweza kutendewa hivi na polisi je, ya mtu wa kawaida itakuwaje," aliohoji wakili huyo.
Ijumaa
iliyopita Manumba alitoa tamko kuhusu kauli zilizowahi kutolewa na
Sitta akiziita kuwa ni za uwongo na kuwataka watu wazipuuze.
Pia alitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Waziri huyo wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Gaudence Mpangala, alisema
mabishano yanayoendelea ndani ya Serikali, yanaonyesha kuwa kuna kitu
kinachofichwa.
Profesa Mpangala alihoji kuhusu mahali ambako kumpa nguvu Manumba kuongelea afya ya Dk Mwakyembe.
Alisema
kitendo hicho kinapingana na msimamo wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda
ambaye aliwahi kukaririwa akisema Dk Mwakyembe ndiye anayepaswa kueleza
hadharani maradhi yanayomsumbua.
Alisema Jeshi la Polisi limedharau kauli ya Pinda na kwamba hiyo inaonyesha kuwa Serikali, imekosa msemaji wa mwisho.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es salaam
Shehe
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Musa Salim, alisema hatua ya
viongozi kupishana inaonyesha kuwa hawafanyi kazi kwa umoja.
“Kilichoongelewa
na Jeshi la Polisi ni sahihi kwa sababu limepewa jukumu la kuchunguza
na kama kuna viongozi hao wanapinga majibu hayo, nadhani wanapaswa kuja
na jibu,” alisema.
“Mimi sijui chochote lakini kama unachoeleza
ni hivyo, maoni yangu ni kwamna tunatakiwa kuheshimu uchunguzi wa polisi
ambao wamepewa dhamana ya kuchunguza,” alisema Sheikh Salim.
Historia ya ugonjwawa Mwakyembe
Dk
Mwakymbe alianza kuumwa Oktoba 9 mwaka jana na baadaye kupelekwa India
ambako alilazwa katika Hospitali ya Apollo kwa matatibu.
Alirejea nchini Desemba 11 mwaka jana, baada ya kulazwa hospitalini kwa takribani miezi miwili.
Msemaji
wa familia ya Dk Mwekyembe ambaye ni Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa
alisema mara baada ya mbunge huyo wa Kyela kuwasili nchini kuwa, afya
yake ni nzuri na ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitalini.
Kauli za Waziri Sitta
Mara
kadhaa Waziri Sitta amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari
akisisitiza kuwa ugonjwa wa Dk Mwakyembe, umetokana na kulishwa sumu.
Akiwa
kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa kiongozi,
iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Jijini Dar es Salaam
Januari 28 mwaka huu, Sitta alisema “ Dk Mwakyembe kapewa sumu, kama
vyombo vya uchunguzi vinasema siyo, basi watueleze ukweli, tena haraka.”
“Ni
vipi uone binadamu ambaye ukimshika katika ngozi unga unamwagika chini,
mhudumu anakuja kuufagia, lakini baada ya saa moja unarudia tena, kitu
hicho si cha kawaida,” alisisitiza Sitta.
Sitta alisema wamejaribu wameshindwa kwa kuwa Dk Mwakyembe analindwa kwa jina la Yesu ambalo ni kubwa kuliko yote.
Waziri Nahodha
Hata
hivyo, akijibu moja ya kauli hizo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi
Vuai Nohodha alimtaka Waziri Sitta awasilishe ushahidi wake ili ufanyiwe
kazi badala ya kuzungumza nje ya vyombo vya sheria.
Lakini, Sitta alisema hatapeleka ushahidi kuhusu madai kwamba Dk Mwakyembe alilishwa sumu kwa kuwa polisi tayari wana ushahidi.
Alilaumu kuwa hata yeye aliwahi kupeleka tuhuma za kutaka kuawa lakini alipuuzwa.
Alisema inachotakiwa kufanywa na polisi ni uchunguzi kuhusu madai ya Dk Mwakyembe kulishwa sumu.
“Waziri
Nahodha anataka ushahidi gani ikiwa taarifa za madaktari zinazomhusu Dk
Mwakyembe kuhusu sumu aliyopewa zilishapelekwa polisi, anataka mimi
nitoe ushahidi gani,” alisema Waziri Sitta.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, February 19, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment