BAADA ya wabunge kuwasulubu mawaziri wakiwatuhumu baadhi yao kuhusika na
ubadhirifu wa fedha za Serikali, lakini kutokuwa na mamlaka ya
kuwafukuza katika nyadhifa zao, wametangaza azma ya kumng’oa Waizri Mkuu
Mizengo Pinda.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), alitoa hoja hiyo jana usiku
wakati akihitimisha hoja ya taarifa ya Kamati yake aliyoiwasilisha
bungeni juzi.
Zitto alisema bunge halina mamlaka na mawaziri hao isipokuwa wana
mamlaka na Waziri Mkuu ambaye kuanzia kesho, watakaa mlango wa Bunge kwa
ajili ya kukusanya saini hizo.
"Mawaziri kwa njia moja au nyingine wamekuwa wagumu sana kuwajibika wanampa
kazi rais kuwafukuza. Sisi hatuwezi kuwafukuza, tuna mamlaka na mtu mmoja, Waziri
Mkuu wa Jamhuri; bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa mawaziri waliotajwa hawatatoka.
Na wasipotoka madudu haya yatarudia," alisema. "Mbunge yeyote anayekereka...kuanzia
kesho tunakusanya saini ili Jumatatu tutoe hoja ya kutokuwa na imani
na Waziri Mkuu," alisema na kuwataka mawaziri waliotajwa kujipima.
Hata hivyo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema suala la kumwajibisha Waziri
Mkuu ni lazima lifuate Kanuni za Bunge.
Kuhusu hoja nyingine, Zitto alikubaliana na mapendekezo ya wabunge kuboresha pendekezo
namba saba kwamba Bunge liunde kamati teule kuchunguza mazingira ya ukodishaji wa ndege ya ATCL.
Wajumbe watatu wameteuliwa ambao ni Ester Bulaya, Mustafa Mangungu,
Kibona Aidha, kuhusu CHC wamekubaliana kuwa taarifa ya CAG ifanyiwe kazi
na kamati.
Zitto pia aliwashauri mawaziri wasiingilie mashirika ya umma. Kuhusu
Bodi ya Pamba na majibu aliyoyatoa Waziri Maghembe kwamba anasubiriwa
Rais ateue Mwenyekiti, Zitto aliwaonya mawaziri kumsingizia Rais kwa
baadhi ya maamuzi yaliyo ndani ya uwezo wao kwa
kuwa wanao uwezo wa kuvunja bodi.
“Tabia ya kumsingizia Rais ikome…” alisema. Alisema tatizo lililopo ni ukosefu wa uwajibikaji
ambalo alisema linapaswa liwekwe katika Katiba mpya. Alisema bila
kuhakikisha serikali inawajibika katika hayo, mwaka kesho watarudia.
Awali, juzi na jana, Bunge lilitawaliwa na mjadala mzito wakati wa
kujadili taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za Usimamizi wa Fedha za
Umma ambazo ziliwasilisha taarifa zake juzi.
Hizo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Mashirika ya Umma (POAC) na Serikali za Mitaa (LAAC).
Wabunge bila kujali itikadi za vyama vyao, walidai wapo baadhi ya mawaziri ambao
‘wanaitafuna’ nchi wakiwatuhumu kwa kuhusika katika ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alikwenda mbali zaidi
akisema ana ushahidi unaoonesha kuwa wengi wa viongozi hao wa wizara
‘wanaitafuna’ nchi.
Tuhuma hizo, zilisababisha Mnadhimu Mkuu wa Shughuli za Serikali
Bungeni, William Lukuvi kusimama na kutaka ushahidi huo na orodha ya
majina ya mawaziri husika viwasilishwe kwa Spika.
Hata hivyo, baadhi ya mawaziri jana walijibu hoja mbalimbali
zilizoibuliwa katika taarifa hizo pamoja na michango ya wabunge pamoja
na Ofisi ya Waziri Mkuu kuagiza kuanzia sasa kwamba Serikali nayo
itakuwa inatoa taarifa za utekelezaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika alisema wakurugenzi 35 na wakuu wa
idara mbalimbali 197 wamechukuliwa hatua kutokana na kuhusika na
ubadhirifu wa fedha za umma.
Alisema kati ya hao, wapo waliofikishwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine kufikishwa mahakamani.
Mkuchika aliyekuwa na orodha ya watumishi hao ambayo hata hivyo hakuisoma bungeni
kutokana na muda, aliwaambia wabunge siyo kwamba Serikali haichukui hatua.
Hata hivyo, alisema Baraza la Madiwani linalohusisha pia wabunge,
ndilo ndiyo serikali ya wilaya ambalo linapaswa liwe mlinzi namba moja
wa mali ya umma.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Hawa Ghasia alisema Takukuru imepelekewa majina ya watu walio nje ya
utumishi wa umma walioshiriki katika malipo hewa.
Aidha, walio katika utumishi wa umma, wametakiwa warejeshe fedha.
Zaidi ya Sh milioni 800 zimesharejeshwa na ziko katika akaunti ya Benki Kuu (BoT) kwa
mishahara iliyochukuliwa kama hewa.
Pia wafanyakazi waliostaafu waliendelea kupewa mshahara, walikatwa kwenye pensheni yao.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) akizungumza kwa niaba ya
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema Serikali ilikuwa ikitekeleza maagizo ya CAG, lakini tatizo
lilikuwa ni kwamba hapakuwa na utaratibu wa kutoa taarifa.
“Kuanzia sasa Waziri Mkuu amesema kwamba kwa taarifa ya Serikali za
Mitaa kwa kuwa inatolewa Machi, watazirudisha taarifa na kuielekeza
mikoa kati ya Mei na Julai halmashauri zijibu zote na hatua ziwe
zimechukuliwa. Taarifa zote za CAG zijadiliwa na vikao vya RCC.
Zitarudishwa kwenye halmashauri kama hazikujibiwa vizuri,” alisema
Lukuvi. Kwa mujibu wa Lukuvi, pamoja na utekelezaji uliokuwa ukifanyika
bila kuwa na taarifa kwa umma, safari hii lazima kitabu kichapishwe na
wabunge wapate, wajue fedha za wananchi zinatumikaje.
Aidha, Waziri Mkuu ameagiza mashirika yote yaliyotajwa kwenye
taarifa za kamati, yahakikishe kwamba ifikapo Septemba mwaka huu ziwe
zimejibiwa kwa uhakika ili pia
zichapishwe kwenye kitabu na kiwasilishwe kwa wabunge.
“Mwakani tutakuwa na mapinduzi juu ya taarifa za serikali,” alisema Lukuvi.
Awali, Filikunjombe alisema anayo orodha ya mawaziri wabadhirifu
baada ya kuomba Mwongozo wa Naibu Spika, juu ya mchango wa Waziri wa
Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami aliyefafanua juu ya sakata la
Shirika la ViwangoTanzania (TBS) kwa kusisitiza kuwa Wizara yake
haimkingii kifua Mkurugenzi, Charles Ekelege, kama wanavyosema wabunge.
“Waziri anapolidanganya Bunge, achukuliwe hatua gani? Waziri Chami
anasema alitekeleza maelekezo yote ya PAC, kwamba uchunguzi unapofanyika
Mkurugenzi wa TBS akae pembeni.
Uchunguzi umefanyika Mkurugenzi akiwa kazini…tuna ushahidi wa
kutosha, kwamba wanaoongoza ‘kutafuna’ nchi hii ni mawaziri wenyewe na
nitataja mmoja mmoja kwa majina na ushahidi tunao,” alisema
Filikunjombe.
Waziri Lukuvi alisimama na kusema: “Ningeelewa kama angejenga hoja
kuona kama Waziri Chami alidanganya…kuhitimisha kwamba mawaziri wote ni
wezi, athibitishe.
Naomba akukabidhi (Naibu Spika) wizi uliofanywa wa kila waziri aliye katika Bunge.”
Hata hivyo, Filikunjombe alisimama tena na kusema ni mawaziri wengi na akasisitiza kutoa
ushahidi.
Dk. Chami katika kuchangia mjadala, alisema ikibainika kuwapo mtu,
ndugu au rafiki mwenye kampuni hewa au maslahi binafsi katika ukaguzi wa
magari nje ya nchi, ataweka uwaziri wake rehani kwa kujiuzulu.
“Haina maana, nitaamua kumfukuza kazi mteule wa Rais bila kufuata
utaratibu? Nimekosea wapi? Kwamba mimi namlinda Mkurugenzi?” Alihoji na
kusisitiza kwamba hakuna mtu atakayelindwa au kukingiwa kifua
asichunguzwe.
Mbunge wa Singida Magharibi, Tundu Lissu (Chadema), aliwataka wabunge kuanzisha mjadala wa kutokuwa na imani na Serikali.
Alisema kila mwaka taarifa ya CAG imekuwa ikionesha wizi mkubwa
uliofanyika, lakini hakuna waziri anayewajibika kwa wizi unaofanyika
katika wizara.
“Hatujawahi kuona mtendaji akichukuliwa hatua. Hatujaona Waziri
akiwajibika kwa sababu ya wizi katika wizara yake au sababu ya
kuhusishwa na uvundo wa wizi wa fedha za umma,” alisema Lisu na kuongeza
kuwa wapo wanaotaka ubunge ili wawe mawaziri kwa lengo la kupora.
Hata hivyo, Lisu alisema hoja yake ya kutaka mjadala wa kutokuwa na
imani ya Serikali na Waziri Mkuu, si kwamba ana hila na Mizengo Pinda,
isipokuwa ni kwa sababu ya mfumo wa utawala uliopo.
“Tuna uwezo kusema Waziri Mkuu wajibika kwa madudu ya Serikali yako,” alisisitiza.
Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed aliwataka wabunge watumie
mamlaka waliyopewa na Katiba, kuhakikisha wanawajibisha wasiotaka
kuwajibika.
Alisema Katiba inawapa mamlaka ya kutumia asilimia 30 kuishauri Serikali na iliyobaki ni kuidhibiti.
“Asilimia 70 tumeshafanya muda mrefu, sasa tutumie kudhibiti madhambi yasiyopatiwa ufumbuzi,” alisema.
Akizungumzia taarifa ya CAG iliyoonesha kuwapo mishahara hewa
iliyolipwa katika baadhi ya vyuo vikuu, Mbunge wa Viti Maalumu,
Christowaja Mtinda (Chadema) aliitaka Serikali itoe maelezo ni nani
anapokea fedha hizo.
Mtinda ambaye alipinga makatibu wakuu kupewa nyumba Dodoma na
kuzitumia kipindi cha mikutano ya Bunge pekee, alisema katika kupitia
taarifa za mwaka za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) alikuta jina
lake kwenye orodha ya watumishi wa chuo hicho, licha ya kwamba hajawahi
kufanya kazi katika taasisi hiyo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Aina Mohamed Mwidau (CUF), aliendelea kuhoji
mkataba wa ukodishaji ndege kwa kuhoji Menejimenti ya Kampuni ya Ndege
Tanzania (ATCL) iliyokuwapo ilipata wapi kiburi cha kuchukua uamuzi huo
wakati timu ya wataalamu ilisema si busara kufanya hivyo.
Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM) alitaka halmashauri
zinazotuhumiwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wakurugenzi na watendaji
wasimamishwe mara moja.
Hata hivyo, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele (CCM) licha ya
kueleza kusikitishwa na ripoti za CAG kutofanyiwa kazi, alisema wapo
mawaziri na wakurugenzi wanaofanya kazi nzuri isipokuwa wanaangushwa na
Wizara ya Fedha kwa kuwapa fedha kidogo tofauti na bajeti.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, akichangia mjadala alitangaza ‘vita’
kwenye halmashauri na kusema itakapoanza, Serikali haitataka suluhu.
“Tuachieni, msitushike mkono. Tutaandaa vita katika jambo hili ili kutatua tatizo la msingi,”
alisema na kusisitiza kwamba wataingia pia kwenye halmashauri zenye
hati safi kuangalia thamani ya fedha na kwamba kwa wenye hati chafu,
Katibu Mkuu ameshaagizwa wakurugenzi watendaji wawajibishwe.
Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Ame Silima akichangia mjadala,
alisema imeundwa timu kwenda halmashauri zote kufuatilia mishahara hewa.
Alikiri kuwepo tatizo hilo na watendaji wanaojihusisha huku akisema baada ya taarifa, hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
Chanzo: HabariLeo