Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais
wa Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF- kuomboleza kifo cha msanii maarufu
nchini Steven Charles Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo, Jumamosi,
Aprili 7, 2012.
Katika salamu hizo, Rais
Kikwete amemwomba kiongozi huyo wa TAFF kufikisha salamu za rambirambi za dhati
ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba na kwa wasaani wote nchini ambao
wamepotelewa na mdau na mwenzi wao.
Rais
Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye
amemwelezea kuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye katika uhai wa
maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia kwa kiwango kikubwa
maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa hiyo kuitangaza Tanzania
kimataifa.
Amesema
Rais: ”Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven
Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa
namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa
ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya
filamu nchini hautasahaulika.”
Ameongeza
Rais Kikwete: “Ndugu Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi
yetu ya Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo
mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi yetu.”
“Nakutumia
wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote
wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa.
Aidha, naomba unifikishie
salamu za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao
katika msiba huu mkubwa. Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki
kigumu cha msiba,” amesema
Rais Kikwete na kuongeza:
“Namwomba
Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa
sababu yote mapenzi yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote
nchini kuwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya
Marehemu Steven Charles Kanumba. Amen.”
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
07 Aprili, 2012
No comments:
Post a Comment