Mazishi ya aliyekuwa msanii maarufu wa filamu nchini
Tanzania Steven Kanumba yamefanyika katika makaburi ya Kinondoni mjini
Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Tanzania Dr Ghalib Bilal aliwaongoza maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaokadiriwa kufikia elfu arobaini, kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa msanii huyo kabla ya mwili wake kwenda kuzikwa.
Shughuli hiyo ya mazishi ilisitishwa kwa muda baada ya umati huo wa watu kusongamana na kukosekana udhibiti na utaratibu wa kuuga mwili huo.
Msanii Kanumba alijipatia umaarufu mkubwa ndani na nje ya Tanzania kutokana na fani ya uigizaji wa filamu za Kiswahili maarufu kama Bongo Movies.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali Waziri wa Habari,utamaduni,vijana na Michezo Dr Emmanuel John Nchimbi amesema, ‘Tanzania imempoteza kijana shupavu aliyetumia vema kipaji chake kujitafutia maendeleo na pia kuitangaza nchi yake.’
Kanumba alikuwa mbunifu katika Fani ya Filamu. Juhudi zake zilimefikisha hadi Afrika Magharibi ambako aliweza kuwashirikisha wasanii kadhaa maarufu kutoka Nigeria katika Filamu zake.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi nchini Tanzania, linaendelea kumshikilia binti mmoja ambaye jeshi hilo limemweleza kuwa alikuwa na Uhusiano wa Kimapenzi na Marehemu Steven Kanumba, kwa maelezo kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu muda mfupi kabla ya kifo chake.
Aidha uchunguzi wa Daktari katika mwili wa marehemu bado unasubiriwa ili kujua chanzo cha kifo cha msanii huyo. Polisi inasema uamuzi wa kumfungulia mashtaka Binti huyo utafuta baada ya taarifa za daktari.
Kifo cha Msanii huyo Steven Kanumba kimegusa hisia za wengi nchini Tanzania kiasi cha kuufanya msiba wake kuwa na sura ya Kitaifa ambako hii leo barabara kadhaa jijini Dar es Salaam zilifungwa kwa muda ili kupisha msafara wa mwili wa marehemu wakati ukielekea kwenye viwanja vya Leader Club Kinondoni.
Mamia ya wananchi kutoka pande mbali za jiji la Dar es Salaam walilazimika kutembea umbali mrefu kwa miguu kwenda kutoa heshma zao za mwisho kwa msanii huyo aliyejizolea sifa nyingi katika sanaa hiyo na wengi kuipenda na kuiheshimu kazi yake.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment