Lula wa Ndali Mwananzela
Msiba wa Msanii maarufu zaidi wa filamu Tanzania Stephen Kanumba
umekuja na kutuachia mshtuko kupita kiasi. Kutokea kwake katikati ya
Ijumaa Kuu na Pasaka kwa kweli umefanya sikuu ya Pasaka (yenye
kuadhimisha ufufuko) kuwa na maana ya pekee kwa baadhi yetu. Sisi
wengine tayari tulikuwa tunaomboleza kuondokewa kwa aliyekuwa Inspekta
Generali wa Polisi Mzee Harun G. Mahundi hatukutarajia mioyo yetu
kuchomwa na msiba mwingine ndani ya muda huo. Lakini Mungu ni Mungu
kwani nina uhakika wapo watu wengine wengi tu ambao walikuwa kwenye
misiba mingine wakati huo huo na msiba wa Kanumba ukaja kama kidonda
kingine.
Kilichoshtua wengi zaidi na hasa tuliopata habari mapema zaidi ni
nini kilitokea. Taarifa za mwanzo kama ilivyotarajiwa zilikuwa na utata
sana maana wengine walianza kusema ilikuwa ni ajali ya gari huko
Mbagala wakati wengine wakitaja vyanzo mbalimbali. Lakini baada ya muda
taarifa zikawa wazi zaidi kwamba kifo cha Kanumba kimesababishwa kwa
namna moja au nyingine katika mazingira ya ugomvi wa kwenye nyumba
(domestic conflict) ambao matokeo yake ni mmoja kufariki. Na
kilichokuwa wazi mapema hiyo ni kuwa msanii mwingine maarufu Elizabeth
Michael a.k.a Lulu alikuwa anahusika.
Mara moja hata hivyo baadhi ya watu walianza kueneza habari kuwa
“Lulu kamuua Kanumba” na wengine kwenda mbali na kumuita “muuaji”.
Niliwasoma wengine wakielezea kifo cha Kanumba kama “mauaji” bila ya
shaka wengine wakishindwa kujua kuwa baadhi ya lugha wanayotumia ina
maana ya kisheria zaidi. Kwamba Kanumba ametutoka hilo halina ubishi
lakini ni mazingira gani yalisababisha hilo hilo ni suala la kitaalamu
na la kisheria. Hapa ndio hoja ya Lulu kutendewa haki inapokuja kwa
sababu tusipoangalia kutokana na maumivu tuliyonayo ya kupotelewa na
mtu tuliyempenda mno basi tunapoteza macho yetu ya haki na tunajenda
macho ya kisasi ambayo hayataki kuutafuta wala kuujali ukweli.
Niwashirikishe maneno yenye hisia hizo yaliyoandikwa na mmoja wa
wanaForum wa JamiiForums.com akijaribu kuturudisha kwenye fikra za
kujali haki bila kumuangalia nani atanufaika na haki hiyo. Yaani,
badala ya kuangalia ni “Lulu” anahusika basi tumweke huyo “Lulu” kama
ni mdogo wetu, binti yetu, rafiki yetu n.k na amefanya kitu ambacho pia
kimemsababishia mauti ndugu, rafiki au jamaa yetu mwingine; je
tungependa atendewe vipi? Ni wazi wengi tungependa atendewe haki;
asionewe, asidhulumiwe au kupendelewa. Yaani, isije kuwa watu ambao
walikuwa na chuki na Lulu kabla ya tukio hili ndio wanakuwa wa kwanza
kupiga debe la “muuaji muuaji” kumbe wanathibitisha tu midomoni mwao
kile wanachokiamini moyoni kutokana na chuki.
Mwanachama huyo aitwaye WomanofSubstance aliandika hivi katika mtandao huo na nimebandika hapa ili kutupa fikra na sisi wengine:
Naanza na kutoa Pole kwa watanzania wote, hasa ndugu jamaa na
marafiki wa karibu wa Kanumba The Great (R.I.P) kabla sijatoa mchango
wangu kuhusu hili jambo zito na nyeti ambalo limetawala maongezi katika
kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka. Mengi yamesemwa na pia kuna mengi
pia hayajasemwa, moja wapo likiwa "ujinai" wa Lulu katika kifo cha
Kanumba.
Katika mukatadha wa sheria, tunaona kwamba Tanzania ni moja ya nchi
zenye kuuweka uwajibikaji kijinai kuwa chini ya UMRI wa miaka 18 kwa
kuweka miaka 10 kama umri ambapo mtu anaweza kushtakiwa kwa kosa la
jinai. (Linganisha na Kenya miaka 8, Zimbabwe -7,Zambia 8,Africa Kusini
10) n.k. Ina maana kwamba mtu (mtoto) aliye chini ya umri huu hawezi
kushtakiwa labda ithibitishwe kuwa alikua anajua kabisa anachokifanya.
Lulu hafit kwenye kundi hili hata kama ana umri wa miaka 17 kama
ambavyo Mh Halima Mdee ame tweet leo baada ya kumtembelea LuLU
Oysterbay Polisi.
Tukiacha sheria na matakwa yake, kwa kuzingatia yale yanayosemwa
kuhusu mkasa huu wa kifo cha Kanumba (R.I.P), inatupasa tuone kuwa kila
hadithi ina pande mbili. Hadithi ya Kanumba ambaye kwa sasa hayupo
kuelezea, na hadithi ya Lulu aliye mahabusu. Inasikitisha sana kwamba
kifo kimetokea katika mazingira ya kutatanisha. Kifo hiki kimesikitisha
watu wengi na kufanya udadisi wa kutaka kujua ukweli ulio objective
iwe vigumu. Watu wamebakia kushusha lawama ZOTE kwa Lulu tu bila kutaka
kujua haswa ilitokea nini hadi kifo hicho kikatokea.
Endelea kusoma habari hii..............
Sunday, April 15, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment