RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa jana alijikuta katika
wakati mgumu baada ya kubanwa na wasomi waliokosoa hadharani sera zake
za ubinafsishaji kwa maelezo kwamba hazijaonesha mafanikio, badala yake
zimechangia kudorora kwa uchumi wa nchi.
Sakata la Mkapa na wasomi
hao lilibuka jana katika Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere
lililofanyika kwenye ukumbi wa Nkrumah katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na kuibua msisimko wa aina yake kwa watu waliohudhuria.
Katika
mjadala huo uliochukua takribani saa mbili, washiriki hao wengi wao
wakiwa wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), walihoji
sababu za Rais huyo mstaafu kupigia debe sera zake za uwekezaji kwamba
zingekuwa suluhisho lakini hadi sasa hali ya uchumi wan chi imezidi
kudorora.
Hata hivyo, Mkapa alipinga vikali hoja za wasomi hao
na kuwahoji akitaka wamtajie, tangu mwaka 2005 alipoondoka madarakani,
ni viwanda vingapi vipya vimejengwa?
'Mnanilaumu kwa sera ya
ubinafsishaji lakini niambieni viwanda vingapi vipya vimejengwa tangu
mwaka 2005?" Alihoji Mkapa ambaye aliongoza Tanzania kuanzia mwaka 1995
hadi 2005.
Mkapa alitetea sera za ubinafsishaji na kueleza kwamba
kimsingi hazikushindwa lakini zimeonekana kuwa na kasoro kwenye
utekelezaji wake kutokana na matatizo ya uongozi na kwamba aliamua
kubinafsisha baadhi ya vitega uchumi kwani vilifilisika.
“Ili
uendesha kiwanda unahitaji mitaji, uongozi bora na soko pamoja na ujuzi,
sisi tulibinafisha baada ya kukosa mitaji na uwezo wa kuviendesha,
tulishindwa kuviendesha, tulikuwa na viwanda vitano vya nguo… vyote
vilikwenda hovyo hovyo,”alisema Mkapa.
Aliilaumu mamlaka
iliyohusika na uwekezaji wakati wa utawala wake, kwa kile alichodai,
kushindwa kuueleza umma ukweli uliosababisha Serikali yake kuchukua
uamuzi wa kubinafisha mashirika na viwanda mbalimbali.
“Tulibinafsisha
mashirika na viwanda 330, kati yake 180 walikabidhiwa Watanzania na 23
wageni, vilivyobaki vilimilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni,
kwanini watu hawahoji sababu za hata wenyeji kushindwa kuviendeleza?
Twende tufanye utafiti tupate sababu za kushindwa,”alisizitiza Mkapa.
Aliongeza
kuwa mbali ya kuwapo matatizo katika sekta ya uchumi wa nchi, baadhi
ya viwanda vilivyobinafisishwa vinafanya vizuri huku akitolea mfano kile
cha Sukari cha Kilombero mkoani Morogoro.
Mkapa alitoa wito kwa
watanzania kujituma kwa bidii kutafuata maendelea badala ya kuendelea
kujadili masuala yasiyo na tija kwa maendeleo ya taifa.
Akizungumza
kwenye mjadala huo, Profesa Issa Shivji, alisema ubinafsishaji
uliofanywa nchini uliuza njia kuu za uchumi zikiwemo benki na Shirika la
Bima na kuifanya Serikali kushindwa kusimamia na kulinda uchumi wa
nchi.
Shivji alitofautiana na mtazamo wa Mkapa aliyedai kuwa
ubinafishaji ulifanywa kwenye viwanda vilivyoshindwa kujiendesha kwa
kukosa mitaji akisema:
“Viwanda tulivyobinafisha ni vile
vilivyokuwa vinatoa faida, tatizo tulilofanya tulibinafisha njia kuu
zote za uchumi hali iliyosababisha Serikali kushindwa kusimamia uchumi
wa nchi.”
Msomi huyo alibainisha kuwa hata nchi zilizoendelea,
ikiwamo China, ziko kwenye ubinafishaji lakini zinatenga maeneo ya
kubinafisha.
Kwa upande wake Dk Ng'wanza Kamata ambaye ndiye
aliyechokoza mada katika mdahalo huo, alihoji kama Afrika inaweza
kutimiza ndoto ya kuwa kitovu cha uchumi duniani kwa kutumia sera na
mfumo uliopo ambao unatoka mataifa ya Ulaya.
“Katika hotuba yako
uliyoitoa Afrika ya Kusini umesema Afrika inaweza kuwa kitovu cha uchumi
wa dunia kutokana na wingi wa raslimali zilipo, je ni kweli tunaweza
kufika huko kwa kutumia mifumo na sera zilizopo? Alihoji Dk Kamata na
kuongeza:
“Wazungu wanajua kuwa Afrika ina utajiri wa rasilimali tangu mkutano wa Berlin”.
Dk
Kamata alisema mfumo wa utandawazi unaonekana kama umejileta wenyewe
ambao ndani yake watu wa Ulaya wanatafuta mahali pa kupeleka mitaji yao
ili waweze kupata faida.
“Zipo kampuni 600 zinazoshika uchumi wa
dunia, lengo lao siyo kusadia wananchi katika nchi husika bali
kutengeneza faida kwa maslahi yao,”alisema.
Kuhusu udhaifu wa
Serikali wadau hao walisema mikakati mingi ya maendeleo inashindwa
kutekelezeka kutokana na tatizo la viongozi kutowashirikisha wananchi
katika kuandaa miradi ya maendeleo.
“Kama viongozi serikalini
wangewashirikisha wananchi katika kujadili miradi ya maendeleo mikakati
mingi ingefanikiwa,”alisema Maselina Charles kutoka Morogoro.
Historia ya ubinafsishaji
Ubinafsishaji
wa Mashirika ya umma hapa nchini ulianza tangu mwaka 1993 na ulikuwa
unaratibiwa na Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC)
iliyopewa mamlaka ya kusimamia
na kuongoza shughuli zote za ubinafsishaji.
Hata
hivyo shughuli za tume hiyo zilisitishwa Desemba 2007 baada ya
kukamilisha ubinafsishaji wa mashirika mengi ambayo yalikuwa
yametengwa.
Mashirika ya Umma 34 ambayo yalikuwa kwenye hatua za
ubinafsishwaji yalihamishiwa katika Shirika Hodhi la Mali za Makampuni
yaliyobinafsishwa kutoka PSRC kuanzia kuanzia Januari 2008.
Januari 2008 Shirika Hodhi la Mali za
Makampuni Yaliyobinafsishwa lilipewa majukumu ya kuendesha shughuli za kampuni zilizokuwa kwenye makakati wa kubinafsishwa.
Matatizo kwenye Ubinafsishaji
Kwa
mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(SAG)mashirika yaliyotengwa kawa ajili ya kubinafsishwa, yalikuwa
yamezuiwa kupanuka zaidi kwa sababu hayawezi kuandaa na kutekeleza
mipango mikakati au kuwekeza.
Pia wafanyakazi wa mashirika hayo
wanakuwa hawana morali wa kufanya kazi au kutimiza wajibu wao kwa sababu
ya kutokujua hatima ya ajira yao na ya mwajiri wao.
Uchakavu wa
mali na raslimali za mashirika yaliyotengwa unakuwa ni wa kiasi cha juu
kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya ukarabati au urudishwaji wa mali
zilizoharibika unakuwa mgumu.
Chanzo: Mwananchi
Saturday, April 14, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment