MSANII wa filamu, Elizabeth Michael Kimemeta maarufu kama Lulu, jana
alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku akibubujikwa
machozi kiasi cha kumfanya Hakimu Ritha Tarimo ambembeleze ili
kumnyamazisha.
Lulu anashtakiwa mahakamani hapo kwa kutuhuma za kumuua
msanii mwenzake, Steven Kanumba na alifikishwa jana kwa mara ya pili
akiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza na Polisi.
Lulu
alifikishwa mahakamani hapo saa 3:06 asubuhi akiwa katika basi dogo la
Magereza pamoja na mahabusu wengine wanawake ambalo lilikuwa
likisindikizwa na magari mengine mawili na alikuwa chini ya ulinzi wa
askari sita wa kike wa Magereza na askari mmoja wa kike wa Polisi
wakishirikiana na askari wa kiume wa Magereza zaidi ya sita.
Mara
baada kuingia katika chumba cha Mahakama, Lulu ambaye alikuwa amevalia
dira jekundu alianza kulia kwa uchungu hali ambayo ilimlazimu Hakimu
Tarimo pamoja na baadhi ya askari kumnyamazisha.
Kutokana na kujaa
kwa watu mahakamani hapo, askari wa Kikosi Maalumu cha Magereza
walilazimika kuufunga mlango wa Mahakama hiyo ili kesi hiyo isikilizwe.
Baada
ya kesi hiyo kutajwa, Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda
aliiomba Mahakama iamuru watu wote watoke nje kwa sababu walikuwa
wamefunga njia ili mtuhumiwa huyo aweze kupitishwa.
Hakimu Tarimo
alikubaliana na ombi hilo na kuwaamuru askari kusafisha njia ili waweze
kumpitisha msanii huyo kwa kile alichosema kuwa Lulu bado ni mtuhumiwa
na anaweza kuumizwa.
“Askari safisheni njia ili mtuhumiwa aweze kupita kwa sababu yeye bado ni mtuhumiwa anaweza kuumizwa,"alisema Hakimu Tarimo.
Baada
ya kutolewa kwa amri hiyo, askari walitimiza wajibu wao na muda mfupi
njia ilipatikana na msanii huyo kutolewa mahakamani hapo.
Jopo la mawakili
Katika
kesi hiyo, Lulu anatetewa na jopo hilo la mawakili akiwemo Kamishna wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Joaquine De- Melo,
Kenedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Massawe.
De- Melo
pia aliwahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) na mshindi
wa Tuzo ya Mwanamke Jasiri Tanzania ya Martin Luther King.
Fungamtama
ambaye ndiye kiongozi wa jopo la mawakili hao wanaomtetea Lulu,
anakumbukwa kwa kuitetea kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Dowans,
katika kesi dhidi ya Tanesco, ambayo alishinda na shirika hilo kuamriwa
kuilipa kampuni hiyo zaidi ya Sh94 bilioni kwa kuvunja mkataba.
Kibatala
ambaye pia anamtetea kada wa Chadema, Fred Mpendazoe katika kesi ya
uchaguzi Jimbo la Segerea, pia ni Makamu wa Rais wa TLS, wakati Massawe
anatoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Mawakili hao
walijitokeza jana mbele ya Hakimu Tarimo tayari kumtetea Lulu na baada
ya mawakili hao kujitambulisha, Wakili Kaganda alisema upelelezi wa kesi
bado haujakamilika na kuiomba Mahakama iipangie tarehe nyingine.
Hakimu Tarimo aliiahirisha kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka huu itakapofikishwa mbele ya Mahakama hiyo kwa ajili ya kutajwa.
Kwa
mara ya kwanza Lulu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, mwaka huu
mbele ya Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando akikabiliwa na la shtaka hilo
la mauaji.
Wakili Kaganda alimsomea hati ya mashtaka alidai
kuwa Aprili 7, mwaka huu katika maeneo ya Sinza Vatican, Wilaya ya
Kinondoni, mtuhumiwa alimuua Kanumba. Kanumba alifariki dunia siku hiyo
saa 9:00 usiku kwa kile kilichodaiwa kuwa ni baada ya ugomvi baina yake
na Lulu.
Chanzo: Mwananchi
Monday, April 23, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment