TAARIFA za kuvuja kwa nyatraka za siri kutoka ofisi ya Kiongozi wa
Kanisa Katoliki duniani zimeibua taswira mpya, wataalamu wakieleza kuwa
zinaambatana na mchakato wa kuanza kumuandaa kiongozi mpya wa Kanisa
hilo, atakayechukua nafasi ya kiongozi wa sasa, Papa Benedict XVI.
Kwa
mujibu wa wataalamu wa masuala ya kanisa hilo mjini Vatican, wameeleza
kuwa hilo ni jaribio la kwanza la kumwondoa madarakani Papa Benedict
XVI.
Nyaraka hizo za siri ambazo zimepewa jina la "Vatileaks"
zimesababisha kashfa mpya katika kanisa hilo, zikifichua mpango wa
kumwondoa madarakani, Tarcisio Bertone, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Vatican ambaye anaonekana kuwa na sauti na madaraka makubwa, kiasi cha
kwenda kinyume na maadili ya kanisa hilo.
Huku Vatican ikiendelea
kusafisha waovu na wanaovujisha nyaraka hizo kutoka dawati binafsi la
Papa Benedict XVI, uvumi umezagaa kwamba mzozo huo unazidi kutanuka na
kwa sasa ni vigumu kuuzima.
Kanisa Katoliki limekuwa na rekodi
mbaya ya kuzima kashfa ambazo zimewahi kulikumba kama vile za
utakatishaji fedha, udhalilishaji watoto na kashfa ya sasa inaweza
kuanzisha mchakato wa kusaka Papa mpya.
"Kundi la makadinali
kadhaa katika Vatican limeanza kwa siri mchakato wa kumwondoa Waziri wa
Mambo ya Nje, kufikiria pia mchakato wa kusaka mrithi wa Papa
(conclave) wakiangalia ni nani anafaa miongoni mwao," limeeleza gazeti
La Repubblica la Italia.
"Nyaraka hizo zilizovujishwa
zinamhusisha Kardinali Bertone kwa njia moja au nyingine," anaeleza
Marco Politi, mtaalam wa masuala ya Vatican wakati akizungumza na
Shirika la Habari la AFP.
"Huu ni mpango wa kumwondoa na kuweka waziri mwingine," ameongeza mtaalam huyo.
Bertone,
ambaye ni mshirika na rafiki wa karibu wa Papa Benedict XVI, amezusha
mijadala mkali hasa kuhusu uendeshaji wa benki ya Vatican, jambo ambalo
limetia doa uongozi wa kanisa hilo.
Nyaraka hizo zimefichua siri
nyingi za Vatican, zikiwamo za matatizo ya ulipaji kodi, udhalilishaji
wa kijinsia wa watoto na majadiliano na makundi ya waasi wenye msimamo
mkali ndani ya kanisa hilo.
Ingawa nyaraka hizo hazitoi habari za
kushtua wala kushangaza, zimefungua ‘dirisha la sumu’ ambayo imekuwa
ikisambaa miongoni mwa watendaji wa Vatican.
Taarifa hizo ambazo
zilivuja Januari mwaka huu zinaonyesha kuwapo kwa mzozo mkubwa baina ya
Bertone na Askofu Mkuu Carlo Maria Vigano, ambaye amekuwa akijaribu
kusafisha hesabu za Vatican, kiasi cha kuondolewa ikidaiwa kwamba ni
kutokana na kupambana na maovu.
Askofu Vigano alimwandikia barua
Papa Benedict na kuomba asiadhibiwe kwa kuondoa waovu na wale
waliohusika na matumizi mabaya ya fedha za Vatican ambazo zimesababisha
benki inayomilikiwa na kanisa hilo kupoteza mamilioni ya euro kwa
kuingia mikataba mibaya, lakini hakufanikiwa.
Watu walio karibu
na Vatican wanamtuhumu Papa Benedict XVI kwa kutokuwa thabiti na kukosa
nguvu za kupingana na uamuzi wa Bertone.
"Risasi hizi zinamlenga
Bertone. Zinalenga kumwangusha na kumzamisha, kwa lengo la kutaka
ajiuzulu," alieleza mtaalam wa theolojia wa Italia, Vito Mancuso
akizungumza na wanahabari wiki jana.
Kardinali huyo mwenye umri
wa miaka 78, pia anatuhumiwa kwa kulazimisha benki ya Vatican kumtimua
kazi mkuu wake, Ettore Gotti Tedeschi, ambaye ni mtaalam wa masuala ya
fedha kwa kushindwa kufuata maagizo.
Gotti Tedeschi alikabidhiwa
jukumu la kusafisha Vatican na kuirejesha katika nchi zenye vitabu safi
vya hesabu, lakini alishindwa baada ya Bertone kusisitiza kwamba benki
hiyo inao uhuru wa kujiendesha, bila kuingiliwa.
"Bertone ana
madaraka makubwa. Tunatakiwa kuondoa uoza ndani ya kanisa," alieleza
mmoja wa maofisa wa Vatican akizungumza na gazeti la La Repubblica.
"Wale wanaovuisha siri, wanafanya hivyo kwa maagizo ya papa," kilieleza
chanzo hicho.
Mzozo huo uliingia sura mpya baada ya Vatican
kutishia kumshitaki mwandishi wa habari Gianluigi Nuzzi kwa kitabu
chake kipya "His Holiness", ambacho kimeandikwa kwa kutumia nyaraka hizo
zilizovujishwa.
Kama njia ya kuzuia kuvuja zaidi kwa nyaraka
hizo, Msaidizi wa Papa Benedict, Paolo Gabriele amekamatwa kwa tuhuma za
kuvujisha nyaraka hizo na amekuwa akihojiwa na watu wengine walioko
karibu na Papa.
Uvumi umezagaa kuhusu watu 20 ambao wamekuwa
wakivujisha siri hizo kwa vyombo vya habari, huku wawili kati yao ambao
wamezungumza kwa masharti ya kutotajwa wakieleza kwamba Vatican
imechafuka haiwezi kujisafisha.
"Kitu dhahiri ni kwamba Tarcisio
Bertone hawezi kujiondoa katika kashafa hii kwa sasa," alieleza mtaalamu
wa masuala ya Vatican, Sandro Magister.
"Hawezi kupona, kuna kila dalili kwamba papa atachukua uamuzi wa kumwondoa na kumweka mwingine katika muda mfupi ujao."
Kulingana
na mtaalam mwingine, Bruno Bartoloni, siri hizo za "Vatileaks" ni
kashfa ambayo inakamilisha miongo ya utawala mbovu na rushwa unaoitesa
Vatican.
Chanzo: Mwananchi
Tuesday, May 29, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment