Monday, May 28, 2012

Nchimbi aonya vurugu Zanzibar

Best Blogger Tips
 WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kumkamata mtu yeyote atakayechochea fujo na vurugu visiwani hapa bila kujali wadhifa wake.

Akizungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo wanajumuia za maimamu (Jumaza) pamoja na mwakilishi wa mabalozi katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani Kilimani, katika mkutano uliohudhuriwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Saidi Mwema, Nchimbi alisema Watanzania wanahitaji amani ambayo inatakiwa kulindwa na kila Mtanzania.

Nchimbi ambaye alidai kuridhishwa na kurejea kwa utulivu katika viunga vya mji huu, alisema serikali haiwezi kamwe kunyamaza na kuwaachia watu wachache wakivuruga amani na kuhatarisha usalama wa wengi.

Bila kutafuna maneno, waziri huyo alikiri kutofurahishwa kwake na mwenendo mzima wa kikundi cha Uamsho kinachotuhumiwa kushiriki vurugu kubwa zilizozuka kwa siku mbili zilizopita.

Alisema jumuia hiyo, ambayo kwa karibu mwaka mzima imekuwa ikiitwa na kuonywa na polisi dhidi ya matamshi mbalimbali yaliyolenga kuwagawa Watanzania, lakini mara tu inapotoka katika meza ya mazungumzo hurejea tena kuhubiri yaleyale, jambo alilosema sio la kiungwana.

“Hata katika mikutano na maandamano ya juzi walikuwa na haki ya kufanya maandamano, na walitakiwa kuomba kibali na kupatiwa ulinzi, jambo ambalo hawakulifanya,” alisema.

Aliwaomba viongozi wa serikali kushirikiana na kuona wananchi wanarudi katika hali yao ya zamani na kusisitiza jeshi kutosita kuchukua hatua kwa yeyote atakayevunja sheria.

Naye sheikh kutoka msikiti wa Amir Tajo, Omar Mohamed Ali, alimtaka waziri huyo kuangalia kanda za jumuia za Uamsho na kuona kama kuna uvunjifu wa amani, na kudai kuwa juzi walifanya matembezi ya hiyari bila kudhuru mtu, ambapo polisi walikuwa na habari ya matembezi hayo na badala yake, walimchukua sheikh wao kwa njia ya kumteka nyara hali iliyozua hisia tofauti kwa wananchi.

Katika hatua nyingine watu 30 wakiwemo viongozi watatu wa jumuiya ya Uamsho akiwemo Mussa Juma Issa wamepandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Mwanakwerekwe wakikabiliwa na tuhuma ya kukusanyika na kuandamana bila kibali na kufanya fujo.

Viongozi na watu hao hata hivyo, wameachiwa kwa dhamana ambapo upelekezi wa kesi hiyo bado unaendelea.

Vurugu kubwa zilizuka juzi mjini hapa ambapo, kundi la watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Uamsho walifanya ghasia kubwa ikiwemo kuchoma magari, kushambulia nyumba ambapo kanisa moja la T.A.G Kariakoo lilichomwa moto na kuharibiwa vibaya ikiwa ni pamoja na magari ya watu.
Aidha katika vurugu hizo inadaiwa kwamba watu wasiofahamika walianza kusaka nyumba wanazoishi watu kutoka Tanzania Bara wakitishia kuwaua.

Marekani yahuzunika
Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, ameeleza kusikitishwa kwake na vurugu zilizozuka mjini hapa na amewataka viongozi wa makundi yote kuhakikisha kuwa wanasimamia amani na utulivu kwa nguvu zote.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, balozi huyo alisema vurugu hizo zimetia doa amani, umoja na mshikamano ambao umekuwepo tangu uchaguzi mkuu uliyopita, na kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa.

Amesema ni vema kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kulinda amani kwa kuwa ghasia hizo zitaleta athari kwa uchumi wa nchi na kuwaogopesha watalii na wawekezaji wa kigeni kuingia nchini.

Uamsho yakana kuchoma kanisa
Katika hatua nyingine, Taasisi za Kiislamu na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI), imepinga kuhusika kuhamasisha kufanya machafuko yaliyotokea mji wa Zanzibar usiku wa Mei 26 na kusababisha kuchomwa moto kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) la Kariakoo ikiwa ni pamoja na kuharibu magari, miundo mbinu na mali nyingine.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari imesema, “Kama alivyosema Mtume (S.A.W) katika Hijatul Wadaa, kwamba ni haramu kumwaga damu zenu, kuharibiana mali zenu, kuvunjiana heshima zenu ila kwa haki ya Uislamu (maana yake pale mtu anapofanya kosa na likathibitika atahukumiwa kwa hukumu ya Kiislamu). Vile vile Uislamu unaheshimu nyumba za ibada (makanisa, mahekalu na sehemu nyingine za ibada) zisivunjwe wala zisiharibiwe.”

Jumuia hiyo ilitoa wito kwa Waislamu na Wazanzibar wote kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi na kutoharibu mali za serikali, mali za wananchi, taasisi za dini zenye imani tofauti, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Taarifa hiyo ilibainisha kwamba matukio hayo wanayachukulia kama njama za makusudi za wale wasioipendelea amani ya nchi hii, pamoja na kutaka kuipaka matope jumuiya na kutaka kuzuia lengo la Wazanzibari kudai nchi yao.

“Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya dola wafanye kazi zao kama wanavyotakiwa kwa mujibu wa muongozo wa haki za binadamu kwa polisi na vikosi vingine kwani wana jukumu la kutunza amani na utulivu na jukumu la kutoingilia haki za watu,” ilisema taarifa hiyo.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits