RAIS Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa jana alipanda kizimbani
kumtetea Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa
Mahalu katika kesi ya uhujumu uchumi yanayomkabili, huku akimmwagia sifa
kemkem za utumishi mwema.
Profesa Mahalu na mwenzake, Grace
Martin aliyekuwa Ofisa Utawala wa Ubalozi huo, wanakabiliwa na kesi hiyo
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuisababishia
Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60, kupitia mchakato wa ununuzi wa
jengo la Ubalozi wa Tanzania Italia.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais Mstaafu kupanda kizimbani kwa sababu yoyote ile.
Mkapa
ambaye wakati wa ununuzi wa jengo hilo alikuwa Rais, aliieleza Mahakama
kuwa anatambua mchakato wa ununuzi huo na kwa kuwa yeye ndiye aliyetoa
idhini ya ununuzi, mchakato wote ulikwenda vizuri.
Mkapa na
msafara wake ulioongozwa na maofisa wa itifaki aliwasili mahakamani hapo
saa 3:45 asubuhi. Akiwa amevalia suti ya rangi ya kijivu alielekea
ndani ya Mahakama hiyo akiwa amezungukwa na wapambe wake akitabasamu
baada ya kuwaona wanahabari.
Aliingia katika chumba maalumu cha mapumziko hadi saa 5:32 asubuhi muda ambao aliitwa kizimbani kutoa ushahidi wake.
Kabla
hajaanza kutoa ushahidi, alikula kiapo maalumu cha kutoa ushahidi wa
ukweli na baadaye kuendelea hadi saa 7:31 mchana alipomaliza na
kuondoka.
Mkapa alianza kutoa ushahidi katika kesi hiyo
inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ilvin Mugeta, akiongozwa na
mmoja wa mawakili wa Profesa Mahalu, Alex Mgongolwa kwa kueleza historia
ya utumishi wake katika nafasi za kidiplomasia.
Mkapa alijibu
maswali kwa kujiamini na kwa umakini mkubwa huku mara kadhaa akiwavunja
mbavu wasikilizaji kwa jinsi alivyokuwa akiwajibu mawakili wa Serikali
wakati mwingine mwenyewe alishindwa kujizuia kucheka.
Akielezea
mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo. Mkapa alidai kuwa Serikali yake
ilifahamu ununuzi wake na taratibu za malipo baada ya kufahamishwa na
Profesa Mahalu na kwamba lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
“Nilitambua
muuzaji alipaswa alipwe malipo kwa kutumia akaunti mbili tofauti na
Serikali ilitoa baraka. Mimi nilitaarifiwa na sikuzuia,” alidai Mkapa.
Kuhusu
kuwepo kwa mikataba miwili katika ununuzi wa jengo hilo Mkapa alijibu:
“Ninachoweza kukumbuka kwa hakika mimi ni kwamba niliambiwa kuwa kuna
malipo katika akaunti mbili ‘separate’ (tofauti).
Alieleza
kushangazwa na taarifa kwamba aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Martin
Lumbanga katika ushahidi wake alidai kuwa alikuwa hajui mchakato wa
ununuzi wa jengo hilo.
Wakili Mgongolwa: Shahidi, alikuja hapa
Shahidi wa kwanza wa mashtaka (PW1), Martin Lumbanga akasema kuwa hakuwa
na taarifa za idhini ya Serikali katika ununuzi wa jengo hilo. Je, wewe
unasemaje?
Mkapa: Ninashangaa ni kwa nini alisema hivyo.
Mgongolwa: Lakini wewe ukiwa Rais ulijua na ukabariki, inawezekana yeye asingeweza kujua?
Mkapa: Ndiyo.
Mkapa
alidai kuwa katika mchakato wa ununuzi wa jengo hilo, mbali na Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia kwa Balozi Mahalu,
wizara nyingine ambazo zilihusika ni Ujenzi na Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi akidai kuwa zote zilituma wataalamu wake kufanya
tathmini ya jengo hilo kabla ya ununuzi.
Akielezea maelezo
yaliyoko katika kielelezo cha 6 cha ushahidi wa upande wa utetezi
ambacho ni taarifa ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa bungeni wakati huo Jakaya Kikwete (sasa Rais) juu ya mchakato
wa ununuzi wa jengo hilo Mkapa alisisitiza:
“Maneno hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi kuwa ndiyo yaliyotokea.”
Taarifa
hiyo pamoja na mambo mengine, inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa
jumla ya Sh.2.9 bilioni na kwamba hati za umiliki wake
zilishawasilishwa wizarani na kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
Mkapa alieleza kuwa hajawahi kupata
malalamiko yoyote kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa sheria katika
mchakato wa ununuzi wa jengo hilo na wala kwa mmiliki wa jengo hilo
kudai kuwa alilipwa pungufu ya kiasi walichokubaliana.
Wakili
Mgongolwa: Kikatiba Rais hukabidhiwa ripoti ya CAG. Je, una taarifa
yoyote ya CAG kuhusu malalamiko juu ya ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Sikuwahi kupata malalamiko hayo.
Wakili: Nini ufahamu wako kama Rais Mstaafu juu ya utumishi wa mshtakiwa ambaye ulimteua kuwa Balozi Italia?
Mkapa: Ninamfahamu kama ni msomi mzuri, mwadilifu na mfanyakazi mwaminifu na kiongozi wa haki.
Akizungumzia
mawasiliano yake na Profesa Mahalu wakati akiwa Balozi, Mkapa alidai
kuwa walikuwa wakiwasiliana ama kwa maandishi au kwa mdomo na kwamba
hiyo ilitegemea usiri wa jambo husika, lakini akasisitiza kuwa wakati wa
mchakato wa ununuzi wa jengo hilo waliwasiliana.
Baada ya kumaliza
kutoa ushahidi wake, Mkapa aliulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa
Serikali, Vicent Haule na Ponsiano Lukosi kuhusu ununuzi wa jengo hilo,
sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:
Wakili Haule:
Mheshimiwa katika Hansard (kielelezo namba 6 cha upande wa utetezi)
uliyosoma imeandikwa jumla ya pesa zilizopelekwa kununua jengo hilo ni
kiasi gani?
Mkapa: Sh.2.9bilioni.
Haule: Na zilizoandikwa kwenye hii risiti ambazo ulisema ulikuwa unazifahamu ni kiasi gani?
Mkapa:
Nilichosema ni Euro 3milioni, mimi sijui exchange rate (gharama za
ubadilishaji wa fedha) wakati huo ilikuwa ni kiasi gani hiyo si kazi
yangu.
Haule: Nani aliagiza upelelezi wa ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa: Mimi Sijui.
Haule: Uchunguzi wa malipo hayo ulifanyika lini ukiwa bado madarakani au baada ya kutoka madarakani?
Mkapa: Mimi sijui, nilikuja kusikia tu kuwa Balozi wako anashtakiwa.
Haule: Ulijua lini kuwa Balozi wako uliyekuwa umemteua wewe anashtakiwa?
Mkapa: Siku alipofikishwa mahakamani ndipo nilipoambiwa na kesho yake kweli nikamuona kwenye magazeti.
Haule: Ulisema ulipotaarifiwa kuhusu ununuzi huo ulibariki na hukuzuia, kwani ulipaswa kuzuia?
Mkapa:
Ningeweza kuzuia na kuamuru hizo pesa zipelekwe kwingine kwa kuwa
wakati huo tulikuwa na crisis (tatizo) ya fedha, lakini kwa kuwa niliona
umuhimu wa ununuzi wa jengo hilo nikaagiza linunuliwe.
Haule: Umuhimu upi wa kulipa kupitia akaunti mbili?
Mkapa: Kupata Chancellery (ofisi ya ubalozi)
Haule:
Baada ya kutoa maagizo hayo (kwa Profesa Mahalu) ni nani mwingine
wizarani (Mambo ya Nje) uliyemwarifu kuhusu malipo hayo kwa akaunti
mbili?
Mkapa: Kwani hiyo inahusiana na nini? Maagizo yangu mimi
nilishatoa kwa balozi jengo linunuliwe, kama Rais nilikuwa ninaagiza tu.
Haule:
Mheshimiwa, nakuuliza tena na nisingependa nawe uniulize swali. Ni
kweli au si kweli kwamba hakuna mtu mwingine wizarani ambaye ulimpa
taarifa hizo?
Mkapa: Sikumbuki mimi.
Lukosi: Mheshimiwa, Lumbanga akiwa Katibu Kiongozi ulikuwa ukimwamini?
Mkapa: Ndiyo.
Lukosi: Ni kwa kiasi gani ulimshirikisha katika ununuzi wa jengo hilo?
Mkapa:
Specifically katika hilo sikumbuki lakini ki-principle nilishatoa
maagizo kuwa kupata chancellery nunueni na yeye alikuwa akijua.
Tulifanya hivyo India, Marekani na Uingereza.
Lukosi: Sasa Lumbanga alisema hajui ununuzi wa hili. Je, wewe unaona ni kitu cha kawaida?
Mkapa:
Ndiyo maana nimesema nashangaa, maana haingewezekana kwamba mimi
nika-communicate (nikafanya mawasiliano) na wizara moja tu na Lumbanga
asijue.
Lukosi: Ulipata kujua au kuuliza ni kwa nini muuzaji alitaka alipwe kupitia akaunti mbili tofauti?
Mkapa: Sikuuliza, mimi nilichokuwa nataka ni Chancellery.
Lukosi:
Unakumbuka kuna jengo jingine la ubalozi ambalo muuzaji alitaka alipwe
kwa utaratibu huu wa kupitia akaunti mbili tofauti?
Mkapa: Siwezi
kusema, nakumbuka lakini siwezi kusema kwa sababu mambo mengine
ukiyasema, yanaweza kuharibu uhusiano na nchi husika.
Hakimu Mugeta: Kwa hiyo hayo mazingira huwa yapo?
Mkapa: Ndiyo.
Lukosi: Unawakumbuka watu wengine uliowahi kuwateua ambao wako mahakamani na yuko mwingine alishakuja kukuomba umtetee?
Mkapa: Ni lazima nilijibu hili? Alihoji Mkapa huku akicheka na kuwafanya wasikilizaji nao wacheke.
Lukosi: Kwa hiyo hii ni kesi ya kwanza kwako kuombwa kuja kutoa ushahidi?
Mkapa: Ndiyo.
Wakili:
Nikiwaambia lengo la mwenye jengo kutaka mchakato wa uuzwaji kuwepo na
mikataba miwili lilikuwa ni kukwepa kodi kwa Serikali yake utasemaje?
Mkapa:
Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na
nimepata nyumba, nasema Al Hamdulillah, alisema Mkapa huku akicheka tena
na kuwafanya wasikilizaji nao wavunjike mbavu.
Lukosi: Nikikwambia
kuwa hizo pesa kulipwa kwa instalment (awamu), Profesa Mahalu alikuwa
anataka azitumie kwa maslahi yake utasemaje?
Mkapa: Mimi nitashangaa sana, hasa nitakushangaa wewe, maana Profesa mimi namuamini. Alisema Mkapa na kuwachekesha wasikilizaji.
Mahojiano
kati ya Mkapa na Wakili wa Profesa Mahalu, Mabere Marando katika
kusawazisha maswali aliyoulizwa na mawakili wa Serikali yalikuwa kama
ifuatavyo:
Wakili Marando: Shahidi, Umewahi kupata malalamiko yoyote
kutoka wizarani kuwa kuliwapo makosa katika ununuzi wa jengo la Ubalozi
Italia?
Mkapa: Sijawahi.
Wakili: Ama kutoka kwa Katibu Mkuu
Kiongozi, Martin Lumbanga au Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje au wa
Wizara ya Fedha au Hazna kwamba Balozi alifanya kosa kwenda kufanya
malipo katika akaunti mbili za muuzaji?
Mkapa: Yeyote kati ya hao hakuna.
Marando:
Mpaka unaalikwa kwenda kuzindua jengo hilo uliwahi kupata ushauri
kutoka Ofisi ya DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma) au kwa AG
(Mwanasheria Mkuu wa Serikali) kwamba usiende katika uzinduzi wa jengo
hilo kwa kuwa kuna uchafu?
Mkapa: Sikuwahi kushauriwa.
Awali,
Profesa Mahalu akijibu maswali ya Wakili Mgongolwa, alisema kuwa
Februari 19, 2006 alipigiwa simu na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya
Nje na kumwarifu kuwa kesho yake anatakiwa afike Dar es Salaam kwa
ajili ya mashauriano.
Alidai kuwa alimwambia kuwa kesho yake
isingewezekana kwa sababu ilibidi ajiandae, ndipo akaambiwa kuwa
Februari 21, awe amefika.
Alidai kuwa majira ya alasiri kama saa
10:30 ya Februari 21 alikuwa ameshafika ofisini kwa Kaimu Katibu Mkuu,
Balozi Patrick Mombo ambaye alimpa barua ya utenguzi wa uteuzi wake kama
Balozi nchini Italia iliyokuwa imeandikwa siku hiyohiyo ya Februari 21,
2006.
Profesa Mahalu alisema kuwa alishangaa maana hakuwahi kuwa
na jambo la kusababisha uteuzi wake kutenguliwa na kwamba alipomuuliza
Mombo alimjibu tu kuwa ni agizo ya Rais.
“Kabla ya kutenguliwa kwa uteuzi huo sikuwahi kuwa na tuhuma yoyote juu ya jambo lolote,” alisisitiza Profesa Mahalu.
Katika
kiapo chake alichokiwasilisha mahakamani mwaka jana Mkapa alisema: “Kwa
kipindi chote ambacho nimefanya kazi na Balozi Mahalu katika nafasi
mbalimbali za utumishi wa Serikali ameonyesha tabia thabiti na za dhati,
uaminifu, utiifu, uchapakazi na ubora.”
Alisema kuwa sifa hizo
zilimfanya atunukiwe na Rais wa Italia, Tuzo ya Heshima ya Juu wakati wa
kuadhimisha siku ya taifa hilo, muda mrefu baada ya kuwa ameondoka
nchini humo.
Mahalu na mwenzake wanadaiwa kula njama na kutenda
makosa hayo katika tarehe tofauti na katika maeneo tofauti huko Italia,
likiwamo la kumpotosha mwajiri wao katika hati ya matumizi.
Wanadaiwa
kuwa Septemba 23, 2002 jijini Rome, wakiwa waajiriwa wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walisaini vocha yenye namba
D2/9/23/9/02 ikionyesha kuwa bei ya ununuzi wa jengo la ubalozi ni Euro
3,098,741.58, maelezo ambayo yalikuwa ni ya uongo na yenye nia ya
kumdanganya mwajiri wao.
Chanzo: Mwananchi
Monday, May 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment