MAWAKILI wa Serikali katika kesi ya mauaji inayomkabili mwigizaji wa
filamu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, wamepinga maombi ya mawakili wa
mshitakiwa huyo kutaka umri wake uchunguzwe.
Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana mahakamani hapo mbele ya
Jaji Fauz Twaib, lakini kabla ya kusikilizwa, mawakili wa Serikali
walidai kuwa na pingamizi la kusikilizwa maombi hayo.
Awali kabla ya pingamizi hilo, mawakili wanaomtetea Lulu waliiomba
Mahakama Kuu ichunguze umri wa msanii huyo au kuiamuru Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu ifanye hivyo.
Lakini Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro aliiomba Mahakama hiyo
isisikilize maombi ya Lulu kwa madai kwamba yaliwasilishwa mahakamani
hapo kimakosa, huku pia sheria iliyotumika ina kasoro.
Sheria iliyotumiwa na mawakili wa utetezi ni Sheria ya Mtoto ya
mwaka 2009, kifungu cha 113 inayoruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa
umri wa mshitakiwa.
Kimaro alidai kuwa maombi hayo yalikwishatolewa katika Mahakama ya
Kisutu na ‘kugonga mwamba’ na kuongeza kuwa mawakili wa utetezi
walitakiwa kuukatia rufaa uamuzi huo au kuomba mapitio yake, lakini si
kuwasilisha maombi mapya.
Vile vile Kimaro aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali,
Elizabeth Kaganda, alidai kuwa maombi ya pili kwa Mahakama hiyo ya
kusitisha kesi ya Kisutu ni batili.
Alidai ubatili huo ni kwa sababu kesi ya Lulu Kisutu haisikilizwi,
iko katika hatua ya uchunguzi na sheria inataka kesi kusimama ikiwa
katika hatua ya kusikilizwa.
Hata hivyo mawakili wa Lulu, Peter Kibatala, Fulgence Masawe na
Kennedy Fungamtama na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo aliyetambulishwa kama mtazamaji,
walipinga.
Mawakili hao walidai kuwa waliwasilisha maombi yao mahakamani hapo
kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliotamka kama kuna maombi
yoyote yawasilishwe katika Mahakama hiyo.
Walidai kuwa Mahakama ya Kisutu ina uwezo wa kutoa uamuzi wa maombi
yao kwa mujibu wa sheria na hakuna walipokosea na kuiomba Mahakama
ipuuze maombi ya mawakili wa Serikali.
Baada ya kusikiliza maombi hayo, Jaji Twaib alisema ni vema apate
muda wa kutoa uamuzi kwa sababu ana safari na kupanga kutoa uamuzi huo
Juni 16.
Lulu jana alionekana mchangamfu akiashiria kuanza kuzoea maisha hayo
tofauti na siku za awali, alipokuwa mnyonge mahakamani na wakati
mwingine akilia.
Lulu anadaiwa kufanya mauaji ya msanii mwenzake Steven Kanumba.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na itatajwa tena Juni 4 mwaka huu.
Chanzo: HabariLeo
Monday, May 28, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment