Sunday, May 20, 2012

Rage ataja kilichomliza kwa Patrick Mafisango

Best Blogger Tips
MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, ameanika kilichomliza wakati wa kusoma risala kwenye zoezi la kuaga mwili wa kiungo wa timu hiyo, Patrick Mafisango kwenye viwanja vya TCC, Chang’ombe juzi, jijini Dar es Salaam aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi.

Baada ya kufika katikati, Rage alijikuta akilemewa na simanzi hadi kuangua kilio, hivyo risala hiyo kusomwa na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu,’ hali ambayo ilizidi kuongeza huzuni kwa wengi.

Rage alisema jana kwa njia ya simu kuwa, alishindwa kuendelea na risala baada ya kuvuta hisia ya mengi mazuri, kubwa zaidi la utayari wake wa kuchezea Simba hata bure.

Alisema, Mafisango aliyekuwa akichezea Simba kwa mkopo akitokea Azam, baada ya timu kurejea kutoka Sudan, alimfuata na kumweleza kuwa, kama watamtema, yu tayari kuchezea timu hiyo bila kulipwa.

Rage alisema hayo baada ya kuona mkataba wake wa kuichezea Simba unakaribia mwisho, hivyo akaamua kueleza ya moyoni mwake kwa kusema, alikuwa tayari kubaki akicheza hata bure, ni timu aliyokuwa ameipenda.

“Ukweli ni kwamba, kilichoniliza hasa ni pale nilipokumbuka kauli yake ya mwisho ya kuniambia maadamu mkataba wake umeisha, ni bora aendelee kuichezea Simba hata bure kutokana na mapenzi yake kwa Simba,” alisema Rage na kuongeza: “Ni vigumu kumsahau mchezaji wa aina hii.

Rage, Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salam (DRFA) na Shirikisho la Soka Tanzania -TFF (wakati huo FAT), alisema kingine kilichomfanya apate uchungu zaidi, ni ushujaa wa Mafisango kukiri kosa.

Alisema, wakati Simba ikiwa kambini kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya ES Setif ya Algeria katika raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, Mafisango alisimamishwa kwa utovu wa nidhamu.

Rage alisema nyota huyo alifanya kitu cha kishujaa ambacho hajapata kukiona, baada ya kwenda kambini Bamba Beach na kuwaomba msamaha wachezaji wanzake na benchi la ufundi chini ya Milovan Cirkovic.

Alisema, baada ya kufanya hivyo, Mafisango alifunga safari hadi nyumbani kwake (Rage), na kumwomba msamaha kwa kosa ambalo alilokuwa ametenda, kitu ambacho si cha kawaida kwa wachezaji walio wengi.

“Ni wachache wenye ujasiri wa kiwango chake, lakini Mafisango alifanya hivyo kiasi cha kunishangaza hata mimi, kuniafuata hadi nyumbani! “Sikusita kumsamehe, ingawa ilikuwa imesalia siku moja kabla ya kwenda Algeria,” alisema.

Alisema, kwa vile hakuwemo kwenye hesabu ya kwenda Algeria, alilazimika kufanya kazi ya ziada kupata tiketi na suti ya ziada, kabla ya kumpigia simu usiku kumjulisha alikuwa miongoni mwa wanaokwenda Algeria, hivyo kuwa ‘surprise’ kwa nyota huyo.

“Tiketi na suti kwa wachezaji zilikuwa tayari, kitendo cha Mafisango kuomba msamaha, nikampigia simu Meneja wa Egypt Air (Shirika la Ndege la Misri), kumwomba anitafutie tiketi moja, pia nikamnunulia suti kama wenzake, kisha nikampigia simu na kumpa taarifa ya ghafla,” alisema.

Aidha, Rage alisema kuelekea mechi ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga, Mafisango alimwendea na kumweleza kuwa angemfurahisha kwa kucheza vizuri katika mechi hiyo, ikiwezekana kufunga mabao hadi wamtambue yeye ni nani.

“Kabla ya mechi ya Yanga, alinifuata na kunieza: “Mwenyekiti lazima nikupe raha baada ya mechi kwa kuwashindilia Yanga mabao mpaka wakome; wanitambue mimi ni Mafisango,” alisema Rage akimnukuu nyota huyo anayezikwa leo kwao DR Congo.

Rage alisema, alipotafakari utayari wa Mafisango kucheza Simba bure, kitendo cha kuomba radhi kwa staili ya kipekee na umati uliokuwa unazidi kufurika kuaga mwili wake, akajikuta ameshindwa kuendelea kusoma risala.

Alipoulizwa ni vipi ameshindwa kuondoka na mwili kama kiongozi mkuu wa klabu, Rage alisema alitamani iwe hivyo, lakini naye jana jioni alitarajiwa kuondoka kwenda Marekani kwenye msiba wa shangazi yake.
“Nilitamani sana kwenda, lakini leo jioni (jana), natarajia kwenda Marekani kwenye msiba wa shangazi yangu, ila nitawakilishwa na wengine. Mungu amlaze mahali pema peponi amen,” alisema Rage.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits