Wakati mshambuliaji wa Ivory Coast Didier Drogba
akiwa uwanjani, mama yake anawapikia chakula mashabiki wa nchi yake
katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Mama huyo anapika kuku na samaki na wali, ndizi na vyakula vingine kwa ajili ya mashabiki, wakati mwanaye akila chakula cha hoteli aliyofikia pamoja na wachezaji wenzake.
Mama yake Drogba pia alipika chakula kwa ajili ya mashabki wakati wa Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.
Drogba ni mmoja wa watu maarufu sana nchini Ivory Coast, na mwaka jana alijumuishwa katika Tume ya Ukweli na Maridhiano iliyoundwa ili kupunguza mvutano uliotokana na utata wa matokeo ya uchaguzi na miaka mingi ya mgawanyiko.
Kundi la mashabiki wapatao 60 limesafiri kwenda Equatorial Guinea, ambapo Ivory Coast inacheza mechi zake za awali, na kila siku mashabiki hao wanapata chakula chao cha asili kilichopikwa na mama wa mshambuliaji wao mashuhuri.
"Kila mtu anafanya anachopenda kukifanya," Amesema mama yake Drogba, huku akiwa amevalia nguo za rangi ya chungwa ambayo huvaliwa na Ivory Coast.
"Hii sio kwa sababu ya mwanangu, ni kwa sababu ya kuunga mkono taifa langu."
Mama yake Drogba aliiambia AP kuwa alitazama mechi za ufunguzi kupitia televisheni huku akiwa anakata nyanya na vitunguu na kupika kuku.
Amesema ana imani ya kutazama mechi ya nusu fainali kwenye uwanja wa Bata - iwapo Drogba na timu yake watafuzu.
Amesema anaheshimu sheria, na hiyo ina maana kuwa mwanaye hawezi kula chakula chake wakati huu - anatakiwa kula chakula cha hotelini tu kwa mujibu wa utararibu.
Mama yake Drogba ameiambia AP kuwa ana uhakika atamuona mwanaye akilibeba Kombe la Mataifa ya Afrika.
Chanzo: BBC
No comments:
Post a Comment