Thursday, March 29, 2012

Wachumi waipiga kombora Serikali mbele ya Kikwete

Best Blogger Tips
WACHUMI kutoka China na Vietnam wamesema umasikini unaoikabili Tanzania unatokana pamoja na mambo mengine, viongozi kuwa na maneno mengi kuliko vitendo.Walisema hayo jana mbele ya Rais Jakaya Kikwete na kukosoa mchakato wa ubinafsishaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ambao umebinafsisha na kuua viwanda vingi vya msingi.

Wakichangia mada katika mkutano wa 17 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini Tanzania (Repoa), wachumi hao waliokuwa wamealikwa kueleza uzoefu wao katika masuala ya kuondoa umasikini, walisema Tanzania haikuwa nchi ya kutegemea misaada kutoka kwa wahisani, bali ilipashwa kujitegemea.

Akitoa uzoefu wake, Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya Vietnam alisema inasikitisha kuona Tanzania ina kila rasilimali lakini ni masikini wa kutupwa.

“Nchi imebinafsisha viwanda bila ya umakini na matokeo yake viwanda vingi vimekufa. Kwetu suala la ubinafsishaji tulikuwa makini na Serikali inamiliki viwanda vingi ambavyo vinatoa ajira,” alisema Profesa DucDinh na kuongeza:

“Vietnam hatulimi korosho lakini tuna viwanda vingi vya kubangua korosho, tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.”

Profesa DocDinh aliishangaa Tanzania ambayo inalima korosho lakini ikabinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo ambavyo vingi vimekufa.

“Utabinafsisha vipi viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo ambacho kinategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi?” alihoji.

Alisema kama Tanzania ina nia ya dhati ya kupunguza umasikini wa wananchi wake, inatakiwa kujipanga na kusaidia kuikuza sekta ya kilimo.

“Sekta ya kilimo iboreshwe kwa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kujenga miundombinu na wakulima kutumia mbegu bora na mbolea,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Li Xiaoyung wa Kituo cha Kimataifa cha Kuondoa Umasikini cha Beijing alisema maisha magumu yanayolalamikiwa na wananchi yanatokana na mfumuko wa bei hasa vyakula… “Ugali ni chakula kikuu lakini bei ya unga ni kubwa ambayo wengine wanashindwa kumudu, unategemea nini?”

“Nilipokuja mwaka jana nilikuta kilo moja ya mchele inauzwa kwa Sh1,200 lakini nimeshangaa sasa inauzwa kwa Sh2,500! Huu ni mfumko wa ajabu.”

Alisema mfumko huo kwenye bidhaa za chakula ndio unaowasababishia wananchi umasikini kwa sababu ni bidhaa wanazozihitaji katika matumizi ya kila siku.

Mchina huyo alisema sekta za mawasiliano na madini ambazo zinakua kwa kasi haziwezi kuwaondolea umasikini Watanzania kama kilimo hakitapewa kipaumbele.

JK anena
Awali, akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais Kikwete alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili kuwanufaisha wananchi na wawekezaji akisema kinachotakiwa ni wananchi kubadili mtizamo wa kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa ajili ya kupora mali za wananchi.

“Tukiendelea kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa ajili ya kupora mali wakakasirika na kuondoka zao, tutaendelea kuwa masikini,” alisema.

Rais Kikwete alisema Serikali iliamua kuacha kufanya biashara na kuiachia sekta binafsi na yenyewe kubaki na kazi ya kujenga na kuboresha huduma za jamii.

“Serikali ilikuwa inauza viberiti na nyama tukabinafsisha viwanda na sasa tumebaki kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema mkutano huo utawasaidia watafiti wa masuala ya uchumi kubadilishana mawazo kwa lengo la kufanikisha ajenda muhimu ya kuondoa umasikini nchini.
Chanzo: Mwananchi

Sunday, March 25, 2012

Abdoulaye Wade akubali ameshindwa

Best Blogger Tips
Macky Sall kiongozi mpya wa Senega
Shirika la habari la serikali nchini Senegal limetangaza kuwa rais Abdoulaye Wade amekubali kushindwa na mpinzani wake Macky Sall katika dura ya pili ya uchaguzi wa Urais.

Bwana Wade alimpigia simu mpizani wake Macky Sall, na kumuambia kuwa amekubali kushindwa.
Na maelfu ya wafuasi wa Macky Sall wamejitokeza katika barabara za mji wa Dakar wakisherehekea ushindi wa kiongozi wao.

Miongoni mwa waliokuwa wakisherehekea ni Bi Seynabou Seck " Nimefurahi sana , Macky bado ni kijana na tena ni mtu mpole sana na ana heshima! Kwa hakika anastahili ushindi huu . Kila mtu alikuwa akimuombea ashinde”.

Mshindi huyo wa duru hiyo ya pili ya uchaguzi wa urais ameutaja ushindi wake kama muamko mpya kwa raia wa Senegal.

Macky Sall alikuwa akizungumza mara tu baada ya mpinzani wake Abdoulaye Wade mwenye umri wa 85 kukubali kuwa ameshindwa katika duru hiyo ya pili.

Wade alikuwa anataka kuchaguliwa tena kama raia wa Senegal kwa muhula mwengine wa tatu baada ya kubadilisha katiba ya nchi hiyo.

Mabadiliko hayo yalizua machafuko na vurugu kubwa nchini Senegal.

Machafuko hayo halishtua ulimwengu kwani tofauti na jirani zake Senegali imekuwa tulivu na hajawahi kuwa na mapinduzi ya kijeshi kama jirani zake.

Lakini upinzani ulipinga hatua ya kiongozi wao mkongwe na kwenda mahakamani. Hata hivyo mahakama iliidhinisha hatua ya Wade ya kubadili katiba ili aweze kusimama tena kama rais.

Na baada ya dura ya kwanza kukosa kuwa na mshindi wa moja kwa moja kwani hakuna aliyepata zaidi ya asilimia 50, ikiwa ni lazima kuwe na duru ya pili ambapo viongozi wote wa upinzani walimuunga mkoni Macky Sall.

Na sasa Macky Sall ambaye zamani alikuwa Waziri mkuu katika serikali ya Abdoulaye wade ameibuka mshindi.
Chanzo: BBC

Friday, March 23, 2012

Wabonga wakitoa Accapella

Best Blogger Tips

Thursday, March 22, 2012

Tido Mhando bosi mpya Mwananchi

Best Blogger Tips
BODI ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), imemteua mwandishi wa habari mkongwe barani Afrika, Dunstan Tido Mhando, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni hiyo.Tido alianza kazi rasmi jana, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya kumkaribisha, iliyofanyika katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Tabata Relini jijini Dar es Salaam.

Tido anachukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Sam Shollei ambaye mkataba wake wa kazi ulimalizika mwishoni mwa mwaka jana. Shollei kwa sasa ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Nation Media Group (NMG)

Kabla ya kujiunga na MCL, Tido alishafanya kazi ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 30.
Amewahi kufanyakazi katika iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kisha kwenda nje ya nchi na kufanikiwa kupata heshima ya kuwa Mwafrika wa kwanza,  kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza  (BBC). Akiwa BBC, Tido aliingia katika historia ya habari kwa kuwa mwandishi wa habari ambaye amefanya mahojiano ya ana kwa ana marais wengi wa Afrika.

Mbali na BBC, Tido amewahi pia kufanya kazi katika mashirika mengine ya habari ya nje ambayo ni pamoja na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na Redio Deutche Welle (DW) ya Ujerumani.

Akizungumza ofisini kwake Tabata Relini jana, Tido alisema: "Ninafurahi kujiunga na kampuni ya Mwananchi na nitatumia uzoefu wangu kuiinua kampuni kwa kuongeza kiwango cha weledi wa habari."

Kuhusu historia yake, Tido alisema alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka 1969 Redio Tanzania, akiwa mtangazaji, akabobea hasa katika michezo, hasa mpira wa miguu.

"Niliwahi kutangaza mpira katika nchi nyingi ikiwamo Uganda katika Kombe la Chalenji mwaka 1973, mashindano ya Nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 1974 na nilikuwa nasafiri na Taifa Stars katika nchi kadhaa ikiwamo Nigeria, Sudan, Kenya na Malawi," alisema Tido.

Wakati akiripoti kwenye Michezo ya Madola huko Christchurch, New Zealand mwaka 1974, Tido alikuwa shuhuda wakati mwanariadha wa Tanzania, Filbert Bayi alipovunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 alipomsambaratisha bingwa wa dunia wa wakati huo. "Mwaka 1976 nilichaguliwa kwenda kutangaza mashindano ya Olimpiki nchini Canada, ingawa Tanzania ilijitoa na mwaka 1978 nilienda kutangaza mashindano ya nchi za Jumuiya za Madola huko Edmonton, Canada, kabla sijaenda nchini Kenya mwaka 1979 kutangaza mechi za Kombe la Chalenji na Taifa Stars."

Katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1978 nchini Canada, Tido alitangaza moja kwa moja wakati Mtanzania Gidamis Shahanga alipotwaa medali ya dhahabu kwenye marathon na Bayi alipata medali ya fedha kwenye mbio za mita 1500.Tido alisema baada ya mashindano hayo, alichukuliwa na kampuni ya High Fidelity Production Ltd ya nchini Kenya akiwa mtengenezaji wa vipindi na baadaye kuanza kufanya kazi ya uandishi wa habari kwa kujitegemea akiyawakilisha mashirika ya BBC, VoA na Dutch Welle.

"Nilikaa Kenya kwa miaka kumi kuanzia 1980 hadi 1990, wakati huo nikiwa mwakilishi wa mashirika hayo katika nchi zote za Afrika Mashiriki na Kati. Moja ya habari maarufu nilizowahi kutangza nikiwa Kenya, ni ile ya kuibua taarifa ya kifo cha kutatanisha cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Dr Robert Ouko kunako mwaka 1990," alisema Tido.

Tido alisema mwaka 1990 hadi 2007, alijiunga na BBC na anajivunia kuwa Mwafrika wa kwanza kuliongoza shirika hilo katika Idhaa ya Kiswahili na kufanikiwa kuongeza idadi ya wasikilizaji kutoka milioni saba hadi milioni 21 kwa juma."Ilipofika mwaka 2007, Rais Jakaya Kikwete alinifuata London, Uingereza, na akanitaka nirudi nchini kuliongoza Shirika la Habari la Taifa  (TBC)," alisema, na kuongeza:

"Ninafurahi kuja Mwananchi, kampuni kubwa ya habari nchini na nitatumia uzoefu wangu kutoa mchango wangu katika kukuza demokrasia ya kweli nchini kwa faida ya Watanzania na taifa kwa ujumla."

Akizungumzia ujio wa Tido, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Theophil Makunga, alisema kampuni ya Mwananchi ina kila sababu ya kufurahia kumpata mkurugenzi huyo mpya kwani atasaidia kuharakisha mafanikio ya kampuni.

"Tumepata mtu makini na mwenye msimamo katika taaluma ya habari na tunaamini atatusaidia sana. Hakika tumempata mtu sahihi kwa wakati sahihi," alisema Makunga.
Chanzo: Mwananchi

Wednesday, March 21, 2012

Muamba alifariki kwa dakika 78

Best Blogger Tips
Fabrice Muamba ''alifariki'' kwa dakika 78 baada ya kuzirai uwanjani, amebainisha daktari wa klabu yake ya Bolton Wanderers' Jonathan Tobin.

Madaktari wanasema kua bado ni mapema kutabiri kama atarejea uwanjani kucheza soka.

Lakini Dr Tobin amesema ameshangazwa na jinsi mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alivyoweza kuponyoka hadi wakati huu.

Katika mahojiano yenye makiwa, Dr.Tobin amesema hatukua na hakika, fikra zetu ziliwaza mengine kabisa hatukutazamia kufikia hali hii ya afuweni kiasi hiki. Ni ajabu.

Muamba alizirai kutokana na kukwama kwa mishipa ya moyo wakati wa mchuano wa Kombe la FA kwenye uwanja wa White Hart Lane jumamosi iliyopita.

Dr Tobin ameiambia BBC Michezo kua muuguzi wa klabu ya Bolton Andy Mitchell alikua wa kwanza kutambua kua mchezaji huyo amezirai.

Nilimsikia akipiga kelele, ''Nendeni uwanjani,nenda uwanjani'' Hapo ikawa wazi kua kuna hatari pale uwanjani.

Alisema kua Muamba alipewa vifaa viwili vya kumsaidia kuikunjua mishipa ya moyo mara ya kwanza uwanjani mara ya pili wakati akipitishwa uwanjani na mara nyingine 13 kwenye gari la wagonjwa kuelekea hospitali lakini ajabu ni kwamba hakuna hata moja lililofanikiwa.

Moyo wa Muamba ulipoteza mapigo na kwa mda wa dakika 78 hakupumuwa.

Saa mbili baada ya leo kurejesha fahamu, nilimsogelea na kumuuliza jina lake, akajibu,Fabrice Muamba. Nikasema nasikia wewe ni mchezaji mzuri wa mpira' akasema'Najitahidi' Nilijihisi chozi likinitoka.''

Mtaalamu ameongezea kusema kua: "singependa kuahidi muujiza kwa wakati huu lakini kwa hali ilivyo maisha yake hayamo hatarini tena.

Bado ni mapema mno kusema kwa uhakika kama atarudi kucheza mpira au la.

Dr Sam Mohiddin, mshauri wa masauala ya magonjwa ya Moyo anayemuangalia Muamba kwa sasa, alisema kua Fabrice amezidi kuonyesha dalili nzuri za kupona.

Matokeo yake yamekua ya ajabu kutokana na utunzaji usio wa kawaida. Hali ya afya yake imetushangaza sana.

"Jambo la muhimu ni jinsi alivyotunzwa mara tu alipoanguka na kuzirai uwanjani, huduma ya haraka na hasa majaribio ya kuamsha moyo wake uwanjani White Hart Lane na wakati wa kusafirishwa kuelekea hospitali.
Kwa sasa kurejelea maisha yake ya kawaida ni jambo lenye uwezekano mkubwa.
Chanzo: BBC

Muamba azungumza na Coyle kwa ufupi

Best Blogger Tips
Meneja wa Bolton Owen Coyle amesema alizungumza "kwa ufupi" na Fabrice Muamba kwa mara ya kwanza tangu kiungo huyo alipopoteza fahamu kutokana na matatizo ya moyo.

Mchezaji huyo amelazwa katika hospitali ya London Chest baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati Bolton walipokuwa wakicheza dhidi ya Tottenham katika robo fainali ya kuwania Kombe la FA siku ya Jumamosi.

"Bado ana safari ndefu kupona kabisa lakini kusema ukweli maendeleo yake yanatia moyo," alisema Coyle.
"Kwa hali tuliyokuwa nayo siku ya Jumamosi usiku, kwa hapa tulipofikia kamwe sikutarajia hali ya kutia moyo kama hii."

Muamba alipata usingizi "mzuri" usiku wa Jumatatu katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum, taarifa ya pamoja ya klabu ya Bolton na hospitali ilieleza siku ya Jumanne.

Waganga wamesema wanaendelea kumuangalia kwa karibu kujua maendeleo yake.

Siku ya Jumatatu ilielezwa bado alikuwa akiumwa sana lakini kwa sasa hali hiyo imetengemaa baada ya mchezaji huyo wa zamani wa kikosi cha vijana cha England chini ya umri wa miaka 21 kuanza "kupumua bila ya msaada wa mashine".
Source: BBC

Monday, March 19, 2012

Dk Mwakyembe aweka hadharani ugonjwa wake

Best Blogger Tips
 BAADA ya utata wa muda mrefu wa ama Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe amelishwa sumu au la, jana Mbunge huyo wa Kyela, aliweka hadharani ugonjwa wake akisema unafahamika kitaalamu kwa jina la Popular Scleroderma huku akisisitiza: “Sasa nimepona kabisa.”

Dk Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo mwaka jana yalizidi kumtikisa na Oktoba 9, Serikali iliamua kumpeleka Hospitali ya Appolo, India kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe akiwa amevalia kofia ya pama alisema: “Si kwamba sijambo, bali nimepona kabisa baada ya kugundulika na maradhi hayo na kutibiwa.”

“Nimerudi juzi kutoka India na daktari wangu ameniambia nimepona, nilikuwa nasumbuliwa na maradhi ya ‘Popular Scleroderma’ iliyosababisha ‘skin disorder’ (ngozi kutokuwa katika hali ya kawaida), lakini kwa nguvu za Mungu nimepona, namshukuru Mungu.”

Kuhusu sumu
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za kulishwa sumu, Dk Mwakyembe alikataa kuzungumzia hilo akisema anasubiri uchunguzi ulioagizwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.

Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema angependa kuona uchunguzi huo unakamilika haraka na ripoti yake inatangazwa kwa umma.

Alisema yuko tayari na anasubiri tume hiyo ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri Nahodha imhoji ili atoa kile kilichomo katika ripoti ya daktari wake.

Dk Mwakyembe alisema anachoshukuru hadi sasa ni kwamba afya yake imeimarika kutokana na shinikizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza Serikali kumpa kipaumbele wakati wote akiwa nchini na India hatua ambayo imemwezesha kufika hapo alipo.

Kutokana na hali hiyo, Dk Mwakyembe aliwataka wananchi wote wakiwemo wa jimboni kwake Kyela kuondoa wasiwasi akisema sasa yupo imara kwa ajili ya ujenzi wa majukumu ya taifa.

“Ninaomba wapiga kura wangu wa Kyela waache jazba, wawe na subira juu ya matatizo yangu. Wiki ijayo nitakwenda kuzungumza nao ili niweze kuwaeleza matatizo yaliyokuwa yananisumbua, lakini sasa hivi niko fit,” alisema.

Mtaalamu auzungumzia
Mtaalamu wa afya ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ugonjwa huo wa ‘Popular Scleroderma’ unasababishwa na chembechembe hai nyeupe kushambulia kitu kigeni kilichoingia kwenye mwili na kusababisha magonjwa ya ngozi.

Alisema chembechembe hizo zinaweza kusababisha ngozi ya mwili kuharibika... “Ni magonjwa yanayosababishwa na chembechembe hai nyeupe kujikataa zenyewe na kusababisha ugonjwa wa ngozi na mifupa.”
Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe kuhusu ugonjwa wake imefungua ukurasa mpya hasa baada ya baadhi ya wanasiasa kuamini kuwa hakuwa na tatizo jingine bali, amelishwa sumu. Tayari Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba ambaye alitoa ripoti akisema Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu kama inavyodaiwa, amefanyia uchunguzi madai hayo na kukabidhi jalada lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP ili afungue kesi.

Kauli ya Sitta

Mmoja wa wanasiasa waliodai kuwa Dk Mwakyembe amelishwa sumu, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alipoulizwa jana juu ya kauli hiyo mpya ya Dk Mwakyembe alisema hana cha kuzungumza.

Januari 28, mwaka huu akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe, Dar es Salaam Sitta alisema Dk Mwakyembe amelishwa sumu.

Akizungumza kwa utaratibu, Sitta alisema hana mengi ya kuzungumza kuhusu ugonjwa unaomsumbua Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa isubiriwe ripoti kutoka India ambako alikuwa akitibiwa.

“Dk Mwakyembe si anatibiwa India?,” alihoji na kuendelea, “Nadhani umeshapata jibu, tusubiri… acha huko India waendelee na uchunguzi wao, siwezi kusema lolote zaidi ya hilo nililokuambia.”

Dk Mwakyembe alianza kuugua Oktoba 9, mwaka jana na alitibiwa Apollo hadi aliporejea Desemba 11, mwaka jana. Alirejea tena India kuendelea na matibabu hadi Ijumaa iliyopita aliporudi na kusema kuwa amepona.

Matatizo yake ya kiafya yamesababisha mvutano baina ya viongozi wa Serikali. Wakati Manumba akisema ripoti kutoka Wizara ya Afya ilionyesha hakupewa sumu, waziri mwenye dhamana na afya Dk Haji Mponda alimkana.

Pia Waziri Nahodha ambaye ana dhamana na jeshi hilo la polisi, alikana ripoti hiyo ya DCI Manumba na kutaka aulizwe mwenyewe alikoitoa huku akisema uchunguzi alioagiza bado unaendelea.

Ugonjwa wa Scleroderma

Kwa mujibu wa mtandao wa Johns Hopkins wa www.hopkinsscleroderma.org, Scleroderma ni ugonjwa unaohusisha mfumo wa kinga ambao wakati mwingine dalili zake zinaweza kuwa mtu kuwa na baridi yabisi na sugu. Ni ugonjwa unaoathiri mwili, hasa muunganiko wa tishu na kuufanya kuwa mgumu.

Mfumo wa Kinga
Scleroderma iko katika kundi la ugonjwa wa mfumo wa kinga. Hii ina maana kwamba mfumo wa kinga wa mtu hufanya kazi kwa kujitegemea. Hulinda mwili dhidi ya maadui mbalimbali kama virusi na maambukizi.

Kuwa na ugonjwa huo wa mfumo wa kinga maana yake ni tishu au kinga kuvamiwa na wageni, ama virusi au maambukizi mengine na hivyo kusababisha matatizo.Mtu anapokuwa na scleroderma, seli huathirika kwa sababu katika hali ya kawaida seli haipaswi kuwa na kitu kingine cha ziada katika mfumo wake wa utendaji kazi na kama ikitokea hivyo, mtu huyo hujikuta katika matatizo yanayosababisha mfumo wa mwili wake kutokuwa kama ulivyo kawaida.
Unawezaje kuupata?
Watu wachache hupata ugonjwa huu na hakuna anayejua unatokana na nini. Scleroderma ni ugonjwa nadra. Chini ya watu 500,000 Marekani wanasumbuliwa nao na hakuna anayejua kwa uhakika chanzo chake.
Baadhi ya wataalamu wanabainisha kuwa watu kati ya saba wenye kusumbuliwa na ugonjwa huo ni wanawake. Wenye kusumbuliwa zaidi na ugonjwa huo ni wale wenye umri wa kati ya miaka 35 na 50. Hata hivyo, watoto wadogo na watu wazima zaidi wanaweza kuupata.
Baadhi ya familia zimekuwa zikiathirika zaidi na ugonjwa huu kuliko zingine. Ingawa scleroderma hauonekani kuathiri kifamilia, lakini mara nyingi hutokea katika familia ambayo imewahi kuwa na mtu mwenye magonjwa yanayokaribiana nao kama vile tezi au mengine yanayofahamika kitaalamu kama arthritis rheumatoid au lupus ambayo msingi wake ni kuathirika kwa mfumo wa kinga.

Dalili za awali
Kwa baadhi ya watu kuna dalili mbili za kwanza:
• Vidole kuwa vya baridi na wakati mwingine kubadilika rangi au mtu kuonekana mwenye msongo wa mawazo.
• Vidole na mikono kuwa migumu na kutoa magamba au unga
Mabadiliko ya rangi ya kidole husababishwa na kupungua kwa uwezo wa mishipa ya damu kupitisha damu ipasavyo. Hii hutokea kwa sababu ya madhara yaliyotokea dhidi ya mishipa ya damu iliyoharibiwa kutokana na ugonjwa huo.
Hali ya ubaridi na mabadiliko ya rangi huitwa raynaud’s (hutamkwa ray-knowds). Watu wengi wenye hali hii wanaweza kudumu nayo bila kuwa na ugonjwa wa scleroderma.

Athari tofauti
Athari ya scleroderma inatofautiana sana kati ya watu. Wengi huanza kuona dalili za vidole kubana na hata kuvimba. Kisha kwa baadhi ya watu huchukua miezi sita wakati wengine hata zaidi ya mwaka ugonjwa kujitokeza rasmi.
Chanzo: Mwananchi

Saturday, March 10, 2012

Madaktari warudi kazini Tanzania

Best Blogger Tips
Chama cha Madaktari nchini Tanzania kimetangaza kuwa wanachama wake wanarudi makazini, baada ya kikao cha jana, ambapo viongozi wa madaktari waliokuwa wamegoma walikutana na Rais Jakaya Kikwete ikulu, mjini Dar-es-laam.

Madaktari hao wanasema Rais ameonyesha nia ya dhati katika kutatua mgomo huo pamoja na madai yao mengine , lakini hawana imani na maafisa wakuu katika wizara ya afya nchini humo.

Dr Ulimboka Steven ni Mwenyekiti wa kamati ya Jumuia ya madaktari hao waliokuwa wakigoma na alitoa sababu za kumaliza mgomo:

"Baada ya kujadili kwa kina mapendekezo ya mheshimiwa rais kuhusiana na njia za kutatua mgogoro huu, madaktari kwa umoja wao wametoa heshima kubwa kwa mheshimiwa rais, na kwamba kuanzia muda huu baada ya kikao, wanarejea kazini.

Lakini kitu kikubwa tunapenda tukiweke wazi ni kuwa waziri wa afya na naibu wake bado ni tatizo kwa madktari.

Hatuna imani nao na hatuko tayari kufanya nao kazi.

Na madaktari wamemvua waziri uanachama wa chama cha madaktari wa Tanzania na siyo mwenzetu tena.
Chanzo: BBC

Friday, March 9, 2012

Mahakama Kuu yasitisha mgomo wa madaktari

Best Blogger Tips
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi imewaagiza madaktari walioitisha mgomo nchi nzima, kuusitisha mara moja.

Mbali na kusitisha mgomo huo, madaktari hao wameagizwa kutumia vyombo vya habari ilivyotumia kutangaza mgomo huo, kuutangazia umma kwamba mgomo huo haupo tena na kwamba wanarejea kazini.

Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya madaktari hao kuanza rasmi mgomo wao wakishinikiza kujiuzulu kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, kama moja ya sharti la kuendelea na mazungumzo na Serikali juu ya
madai yao mbalimbali ya maslahi.

Uamuzi wa Mahakama hiyo ulitolewa jana usiku na Jaji Regina Rweyemamu baada ya kusikiliza maombi ya Serikali yaliyowasilishwa mahakamani hapo Jumatano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, kupinga mgomo huo uliotangazwa juzi na madaktari hao, kinyume cha utaratibu.

Katika maombi yaliyowasilishwa mahakamani juzi chini ya hati ya dharura, Jaji Werema, alidai kuwa mgomo huo ni hatari kwa maisha ya watu na unafanyika wakati majadiliano yameanza kati ya madaktari na Serikali na huku kukiwa na kesi Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambayo haijamalizika.

Pia alidai kuwa mgomo ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu kwani madaktari hao wana kiapo cha taaluma yao, ambacho kinaeleza kuwa wao ni sehemu ya taaluma ambazo haziruhusiwi kugoma.

Awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alifungua kesi katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi, Jumanne iliyopita, lakini licha ya kupelekewa hati ya kuitwa katka shauri hilo, madaktari hao hawakutokea na zaidi ya hapo wakatangaza mgomo.

Kutokana na hilo, Serikali ililazimizika kwenda Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi chini ya hati ya dharura juzi kuiomba izuie mgomo huo.

Mbali na kugoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alidai madaktari hao walikuwa na njia za kufanya kabla ya kugoma ikiwemo, kwenda Tume ya Usuluhishi na Uamuzi au kwenda katika Kamati inayoshughulika Huduma Maalumu.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Chama cha Madaktari (MAT) na Jumuiya ya Madaktari ambayo
Serikali inadai kuwa ni batili kwa kuwa haijasajiliwa.

Katika kesi hiyo, Serikali iliwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Edson Mweyunge na walalamikiwa, MAT walihudhuria katika shauri hilo.

Mwishoni mwa wiki, madaktari walitangaza kuanza mgomo juzi baada ya Serikali kukataa matakwa yao ya kujiuzulu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya.

Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete leo anatarajia kuzungumza na Taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alisema jana kwenye maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani kimkoa kuwa Rais Kikwete atazungumza na Watanzania wote kupitia wazee hao na kuwataka wafungulie vyombo vya habari kumsikiliza.

“Naomba nitoe tangazo muhimu sana, wanawake wote na Watanzania wote kwa ujumla kesho
(leo) mfungue televisheni na redio zote, mumsikilize Rais Jakaya Kikwete atazungumza na Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam, tafadhali mfanye hivyo,” alitangaza Sadiki aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya wanawake iliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi
Mmoja, Dar es Salaam.

Sadiki alitoa tangazo hilo kwa msisitizo mara baada ya kuhutubia hadhara hiyo ambayo pamoja na mambo mengine, yeye (RC) alizungumzia suala la mgomo wa madaktari na kuhamasisha wanawake kushiriki katika maoni ya Katiba mpya pindi mchakato utakapoanza.

RC Sadiki alisema Rais Kikwete atazungumza na wazee hao asubuhi, lakini hakueleza atakutana nao wapi wala maudhui ya kukutana nao, ingawa imekuwa ni kawaida ya kiongozi huyo wa nchi kukutana na wazee wa mikoa mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam na Dodoma na kupitia kwao, huzungumzia masuala ya kitaifa.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu alipoulizwa kuhusu Rais kukutana na wazee hao wa Dar es Salaam, alisema kama Mkuu wa mkoa ametangaza hivyo, basi anukuliwe alivyosema.

Kwa sasa, suala la mgomo wa madaktari ulioanza jana nchini kote ndilo linalogonga vichwa kwa sasa na limetokea licha ya rai ya Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwasihi madaktari hao kutogoma kwa sababu matatizo yao yanashughuliwa.

Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (TUGHE), vimewanasihi madaktari wanaogoma na kuwataka wazingatie kiapo chao cha kuhudumia jamii na kurejea kazini.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila, alisema jana kwamba pamoja na madaktati hao kuwa na hoja ya msingi kuhusu madai yao, jambo la msingi zaidi wangeweka maslahi ya Watanzania mbele.

“Tayari Serikali imeonesha dalili ya kuzungumza nao, kuhusu madai waliyoyawasilisha, wangetumia fursa hiyo na kurejea kazini, kwa kuwa wao bado wanabaki kuwa watu muhimu na kugoma kwao kunaweza kuleta maafa makubwa katika jamii,” alisema.

Aliwataka kuangalia kiapo chao, lakini pia kujifunza kuwa na subira wakati masuala yao yakishughulikiwa, kwani hata dini imeweka wazi kuwa mtu anapokuwa na subira hupata mafanikio na thawabu kubwa.

Katibu Mkuu wa Tughe, Ali Kiwenge, alisema mgogoro wa madaktari kwa sasa unaumiza zaidi
wananchi hasa kisaikolojia.

“Kwa sasa mtu hata ukipigiwa simu tu ukaambiwa mtoto, baba au mama anaumwa, unaanza kuwaza utafanyaje, kwa mgogoro huu nchi iko kwenye wasiwasi mkubwa bila sababu za msingi,” alisema.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus
Mgaya, alipotakiwa kutoa maoni na ushauri wake, alisema atazungumza na vyombo vya
habari leo kuhusu mgomo huo.

Kwa upande wa hali katika hospitali nchini, Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI) jana ilisitisha huduma za wagonjwa wa nje kutokana na kupungukiwa madaktari.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema katika taasisi hiyo wameathirika sana na mgomo kwani wamebaki madaktari 10 ambao ni wakuu wa vitengo na Idara kati ya madaktari 72 waliopo.

Katika hospitali nyingine za Dar es Salaam, wagonjwa walirudishwa nyumbani na kutakiwa kurudi hospitalini baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa huduma zimerejea.

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wagonjwa walikutwa wamekaa nje kwenye viti vyao
huku ndugu wakitafuta jinsi ya kuwahamishia katika hospitali zingine za binafsi.

Aidha, RC Sadiki aliwaondoa hofu madaktari wanaoendelea kutoa huduma katika hospitali za
mkoa huo, licha ya kushinikizwa wagome, na kusema Serikali itawapa ulinzi, kwa kuwa wamekuwa wakipokea vitisho.

Aliwaomba waendelee kuokoa maisha ya Watanzania wenzao, kulingana na kiapo walichokula
kwa kuwa tayari Serikali imekubali kushughulikia madai yao hivyo kugoma si ufumbuzi.

Mikoani katika hospitali za Bugando Mwana, KCMC Moshi, Dodoma na Morogoro kulikuwa na
mgomo baridi.
Chanzo: HabariLeo

Wednesday, March 7, 2012

Back in the days!

Best Blogger Tips


Madaktari wampinga Pinda, waanza mgomo

Best Blogger Tips
UPATIKANAJI wa huduma za afya nchini uliendelea jana isipokuwa katika Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza na Amana Ilala, Dar es Salaam huku Muhimbili huduma zikitolewa kwa kusuasua.Jana, ilikuwa siku ambayo madaktari hao walitangaza kuanza mgomo nchi nzima wakishinikiza madai yao ya kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya wajiuzulu au wawajibishwe licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwasihi wabadili msimamo huo kwa maslahi ya wananchi.

Hata hivyo, akizungumzia na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari uliofanyika Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi alisema wamekubaliana kurejea kwenye mgomo kuanzia jana mchana hadi hapo dai lao la msingi la kuwajibika au kuwajibishwa kwa mawaziri hao litakapotekelezwa.

“Madaktari wanasikitika kutoa taarifa kuwa sasa wanarejea kwenye  mgomo na utakuwa kwa nchi nzima hadi dai lao litakapotekelezwa. Wanawaomba wananchi kuelewa kuwa lengo lao ni kutaka kuboresha huduma za afya nchini. Uzorotaji wa huduma za afya nyote mnaufahamu, hata wakilazimishwa hakuna kitakachoendelea tunaomba nia ya madai yetu yasipotoshwe.”
Alisema hayo akipinga kauli ya Waziri Mkuu, Pinda aliyoitoa juzi kwamba madai hayo ya kutaka Dk Mponda na Dk Nkya wang’olewe ni mpya na kusema imewafanya pia watilie shaka utekelezwaji wa madai mengine.

“Madaktari wamesikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Pinda kuwa dai la madaktari kutaka Waziri, Dk Mponda na Naibu wake, Dk Nkya ni jipya. Hii si kweli dai hilo lipo kwenye madai yote ya madaktari na yeye alilipata katika nyaraka zake zote alizokabidhiwa. Hata kauli yake aliyoitoa Februari 9, mwaka huu inaonyesha anatambua dai hilo na kuonyesha nia ya kulitatua.”
Alisema kinachofanyika sasa ni kushinikiza kutekelezwa kwa dai la kwanza kati ya matatu waliyokubaliana na wawakilishi kutoka serikalini ambalo ni hilo la kuwajibika au kuwajibishwa kwa viongozi hao.

Serikali imejiandaa
Akizungumzia mgomo huo jana, Pinda aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam kwamba Serikali imejipanga kukabiliana nao.Alisema juzi alipozungumza na waandishi ofisini kwake, tayari Serikali ilikuwa na mipango yake na ilichokuwa ikisubiri ni kuona matokeo ya mgomo huo kuanzia jana.

“Serikali imejipanga kukabiliana na mgomo huo. Pale jana (juzi) nilipozungumza na waandishi ofisini kwangu sikutaka kueleza mipango yote na kila kitu, lakini tulikuwa tunawasubiri tu wagome,” alisema Pinda.

Hata hivyo, alisema ni matumaini yake kwamba bado milango ya mazungumzo iko wazi na jambo hilo linaweza kupatiwa suluhu bila mgomo na kuwataka madaktari waendelee na kazi.

Alisisitiza kwamba ni makosa kitaaluma kwa daktari kugoma na kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia: “Ningewashauri madaktari waendelee na kazi.”      

Dar es Salaam

Jana katika Hospitali ya Amana kulizuka vurugu baada ya wagonjwa na jamaa zao kuvamia mlango wa mapokezi huku wakitishia kuvunja vioo vya majengo ya hospitali hiyo baada ya kuelezwa kuwa hapakuwa na huduma.

Hali ilionekana kuwa mbaya hadi wanamgambo wa Manispaa ya Ilala walipofika. Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya wahudumu wanaopokea wagonjwa na kuwaandikisha kabla ya kuonana na madaktari kuwaeleza wagonjwa kuwa huduma zimesitishwa.

Kauli hiyo iliwafanya baadhi ya wagonjwa wa nje kuondoka hospitalini hapo na baadhi yao wakiendelea kubishana na wahudumu hao, jambo ambalo lilileta tafrani.
“Sisi tuna makosa gani kwa nini tuambiwe huduma zimesitishwa. Sisi tunaonewa tumetangaziwa tangu jana (juzi) kwamba kuna mgomo lakini wanaoumia ni sisi,” alisema Justine Mushi.
Alipoulizwa kuhusu mgomo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa Amana, Dk Christopher Mnzava alikanusha akidai huduma zinaendelea kama kawaida lakini alielezwa kwamba wahudumu wa mapokezi wamesema kwamba zimesitishwa.

Alifika mapokezi na kuonana na wagonjwa ambao walimweleza walivyoambiwa kuhusu kusitishwa kwa huduma na kutakiwa waondoke lakini Dk Mnzava alisema hizo ni kauli zilizotolewa baada ya kutokea vurugu na si kutokana na mgomo wa madaktari.

Katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili, (Moi) utoaji wa huduma ulikuwa wa kusuasua na baadhi ya madaktari walisema walikuwa katika maandalizi ya kuanza mgomo.

Bugando

Madaktari waliopo katika mafunzo ya vitendo Bugando jana walitangaza kuanza mgomo kuungana na wenzao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha kujadili mgomo huo, mmoja wa madaktari ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini alisema wameamua kurejea katika mgomo wao mpaka hapo madai yao yatakapotekelezwa na Serikali.

Jana hospitalini hapo kulikuwa na tangazo lililokuwa likieleza kuanza kwa mgomo huo ambalo hata hivyo, uongozi wa Bugando umesema ni la kihuni na haulitambui.

Ofisa Tawala wa hospitali hiyo, Joachim Wangabo alisema  mgomo huo ni batili na kwamba watafuatilia kila hatua kujua ni nani wameingia katika mgomo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.

“Naomba niseme Bugando hakuna mgomo, haya matangazo yanabandikwa tu na wahuni, ofisi yangu inafuatilia kujua waliogoma. Wakibainika tutawachukulia hatua,” alisema.

Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Omary Salehe alisema waliogoma ni wanafunzi 65 walioko katika mafunzo ya vitendo na kwamba licha ya mgomo wao, huduma zinaendelea kutolewa na madaktari bingwa licha kuwepo na hatihati ya kuzidiwa kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa.

Hali ya upatikanaji wa huduma hospitalini hapo jana ilikuwa imezorota kwa kiasi kikubwa na katika baadhi ya maeneo hapakuwa na huduma kabisa.

Mmoja wa wagonjwa, James Paul alisema alikuwa amepangiwa kufanyiwa upasuaji leo, hivyo alitakiwa afike jana kwa ajili ya kulazwa lakini aliambiwa aondoke na arejee baada ya wiki tatu.
Chanzo: Mwananchi

Tuesday, March 6, 2012

Mgomo

Best Blogger Tips

Sunday, March 4, 2012

CCM, Chadema sasa vita rasmi

Best Blogger Tips
VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.CCM ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na  Chadema itawatumia viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.

Wakati huohuo, Kamati Kuu (CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho, wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama chochote.

Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya siasa ambavyo hakuvitaja.

Alisema mara nyingi mipasuko ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au ukwasi wa mtu.

“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.

Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888 zilizopigwa kwenye kura za maoni.

“Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema.

Katika kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa  aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata kura chini ya 20.

Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.

Nasari ashukuru

Akitoa shukrani mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, Nasari aliwaomba wafuasi, wapenzi na wanachama wote wa Chadema kushikamana na kuwa tayari kwa mapambano ya haki, kuhakikisha wanaibuka na ushindi mnono kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

"Wao (CCM), najua watatumia dola na fedha, lakini sisi tusihofu kwani tuna Mungu anayetupigania kwa sababu mapambano yetu ni kudai haki dhidi ya uovu.
Kwa pamoja tukishirikiana kuondoa hofu kwani tutashinda," alisema Nasari.

CCM

Kwa upande CCM Kamati Kuu (CC) ya chama hicho jana ilimteua Mwenyekiti mstaafu ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya Tatu , Mkapa, kuongoza kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa chama hicho, Siyoi Sumari katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana, kilipitisha jina la Siyoi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na baba yake, Jeremia Sumari aliyefariki usiku wa Januari 18 mwaka huu.
Nape alieleza kwamba, kamati hiyo pia imemteua Katibu wa Idara ya Uchumi na Fedha ya chama hicho, Mwingilu Nchemba kuratibu kampeni hizo.
Katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga ambao CCM ilishinda, Mkapa ndiye aliyefungua kampeni hizo huku, Nchemba akiratibu kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Akizungumzia tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikiripotiwa katika mchakato wa uteuzi, aliitaka Takukuru kuhakikisha wanakamata mtandao mzima uliohusika na utoaji rushwa.

Kauli ya Siyoi

Sumari, aliambia Mwananchi Jumapili kuwa kwamba pamoja na kufurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake kupeperusha bendera ya CCM wilayani Arumeru Mashariki, chama hicho kinapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kuhakikisha kinatetea jimbo hilo.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba changamoto zote alizozipitia katika mchakato wa uteuzi , zikiwemo tuhuma mbalimbali za rushwa ni misukosuko ya kisiasa ambayo haiwezi kuepukwa zaidi ya kukabiliana nayo.

“Nashukuru chama kwa kupitisha jina langu, lakini changaomoto zote nilizokuwa nikipitia naamini ni misukosuko tu ya kisiasa, lakini tusahau yaliyopita sasa tusonge mbele kunyakua ushindi,” alisema Sumari

UVCCM

Katika hatua nyingine Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM ) wilayani Arumeru, imefurahishwa na uamuzi uliofanywa na CC ya  CCM kumpitisha Siyoi kupeperusha bendera ya chama hicho na kueleza kwamba kilio cha wanachama wa CCM wilayani humo, sasa kimesikilizwa.

Hata hivyo, wakati jumuiya hiyo ikiupokea ushindi huo kwa furaha, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) imeendelea na kamata kamata yake ambapo safari hii ilimshikilia na kumhoji kwa muda Katibu Hamasa wa umoja huo wilayani Arumeru Mashariki, John Nyiti kisha kumwachia huru.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Esther Maleko alisema mbali na kilio cha wakazi wa jimbo hilo kusikika juu ya mgombea wao, umoja wao umejipanga kikamilifu kuingia ulingoni kuhakikisha ushindi unapatikana.

Hekaheka za uchaguzi wa jimbo hilo wakati zikiendelea baadhi ya makada wa CCM na UVCCM wilayani humo wameendelea kukumbwa na misukosuko baada ya viongozi wake akiwemo Nyiti kushikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa wilayani humo.

Nyiti alipoulizwa juu ya taarifa hizo kwa njia ya simu alikiri kukamatwa na maofisa wa Taasisi hiyo.

Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto alipoulizwa na gazeti hili juu ya taarifa hizo hakuweza kukiri wala kukataa juu ya kuhojiwa kwa kada huyo na kudai kwamba wanaohojiwa na Taasisi hiyo wako wengi na wengine wanahojiwa kama mashahidi, hivyo alidai si vyema kuwataja majina kwa kuwa bado wanakamilisha uchunguzi wao.

Hali ilivyo ndani ya vyama

Makundi ya vigogo wa CCCM ambao wanajipanga kugombea Urais mwaka 2015, yametajwa kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho katika uteuzi wa mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki.

Mpasuko wa makundi hayo, inaelezwa unaweza kuchangia chama hicho kupoteza jimbo hilo.

Sumari amekuwa akiungwa mkono  na kundi la Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa huku wagombea wengine, walikuwa wakiungwa mkono na kundi la na vigogo wa chama hicho wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji dhidi ya ufisadi.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili jana katika mahojiano maalumu baadhi ya viongozi wa CCM na makada wa Chama hicho, wameeleza mpasuko huo ni mkubwa tofauti na wengi wanavyofikiri.

Asantaeli Erio alifafanua kuwa, kwa sasa baada ya  Sumari kupitishwa, kundi la vigogo wa CCM na Serikali huenda wakasusa kumpigia kampeni hasa kutokana na kubainika wazi kutomuunga mkono na siri za hoja zao kuvuja.

 Wafuasi wa Sarakikya
Kundi la wafuasi wa aliyekuwa mgombea wa ubunge wa CCM, William Sarakikya na Elishilia Kaaya jana, walieleza kutokubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu kupitisha jina la Sumari kuwania jimbo hilo.

Mmoja wa wafuasi hao, Emanuel Kanangira alisema wanapinga uteuzi wa Sumari na leo wanatarajia kurejesha kadi za CCM.
Chanzo: Mwananchi

Thursday, March 1, 2012

Kambi ya Lowassa yaumiza vigogo CCM

Best Blogger Tips
 KWA mara ya pili, wana CCM Jimbo la Arumeru Mashariki wamedhihirisha kuwa chaguo lao ni Siyoi Sumari baada ya kumchagua kwa kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, William Sarakikya aliyepata kura 361 katika uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.Matokeo hayo ni kama ushindi kwa mojawapo ya kambi ndani ya CCM inayohusishwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa dhidi ya wanachama waliopo katika makundi mengine, ambayo yalikuwa yakipinga kwa nguvu zote kupitishwa kwa jina la Siyoi.

Vyombo mbalimbali vya habari kwa wiki nzima sasa, vimekuwa vikiripoti kuhusu mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala kutokana kuwa na misimamo inayokinza kuhusu nani atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo mdogo.

Siyoi alianza kuzua mtafaruku ndani ya CCM pale suala la uraia wake lilipozua utata ndani ya kikao cha Sekretarieti ya chama hicho, hivyo kusababisha kutolewa kwa mapendekezo kwamba aenguliwe katika kinyang’anyiro hicho.

Kundi linalomtetea limekuwa likilalamikia kile linachodai kwamba ni kuwapo kwa njama za kumtosa mshindi huyo kwa sababu kadhaa za kimakundi.

Hata hivyo, Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana chini ya Mwenyekiti, Rais Jakaya Kikwete kiliamuru kurudiwa kwa uchaguzi baina ya Siyoi na Sarakikya, kwa maelezo kwamba katika wagombea wote sita hakuna aliyekuwa amepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.

Habari zaidi zilidai kuwa, hata baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo, mmoja wa vigogo wa CCM alituma mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu kwenda kumshawishi Siyoi ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho, jitihada ambazo hazikufanikiwa kwani alikataa.

Matokeo ya kura
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa Saa 11:30 jioni na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, Sumari aliibuka na ushindi huo wa silimia 67.8 kati ya kura halali 1,122 zilizopigwa, dhidi ya asilimia 32.2 za mpinzani wake anayedaiwa kupigiwa chapuo na viongozi wa chama na Serikali kuanzia ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi taifa.

Jumla ya kura 1,124 zilipigwa ambapo mbili ziliharibika na kura halali kubakia 1,122.

Akitangaza matokeo hayo, Msekwa alilazimika kuanza kwa kumtangaza mshindi hali iliyofanya ukumbi kukosa usikivu kwa wapenzi, mashabiki na wafuasi wa Siyoi kuanza kushangilia.

Msekwa alisema ameridhishwa na upigaji kura na matokeo hayo yameonyesha imani kubwa waliyonayo wana Arumeru kwa mgombea huyo.

Baadhi ya wana CCM walidai kuwa kauli tata za Msekwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), John Chiligati  katika ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa Wilaya ya Arumeru jana zilimponza, Sarakikya baada ya wajumbe kuamua kupiga kura za hasira wakipinga kile walichodai kushinikizwa kumchagua mtu aliyeelezwa anatakiwa na mfumo (system), wa Serikali na uongozi wa chama.

Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliohudhuriwa na idadi kubwa ya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), maofisa usalama wa taifa na askari kanzu kutoka Jeshi la Polisi, Msekwa na Chiligati waliwataka wajumbe kutumia vyema kura yao kumchagua mtu atakayemudu na kuhimili vishindo vya upinzani kutoka vyama vingine vitakavyosimamisha wagombea.

“Ndugu wajumbe napenda kuwakumbusha jambo moja muhimu kabla ya kupiga kura, leo hatuchagui mbunge, mnachofanya ni kupiga kura za maoni. Mgombea atateuliwa na kikao cha Kamati Kuu Machi 3, mwaka huu,” alisema Chiligati.

Wakati Chiligati akisititiza hoja hiyo, Msekwa alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maneno aliyokuwa akiyasema Naibu Katibu Mkuu huyo huku baadhi ya wajumbe wakiguna.

Msekwa aliyetumia muda mwingi kuzungumzia historia yake ya uongozi ndani ya chama kuanzia TANU hadi CCM aliwataka wajumbe kutoangalia uswahiba wala ushawishi wa aina yoyote katika maamuzi yao bali wahakikishe wanayemchagua anastahili kupeperusha bendera ya chama hicho tawala na kukiletea ushindi.

Katika uchaguzi wa awali wa kura za maoni uliofanyika Februari 20, mwaka huu, Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari aliyefariki hivi karibuni aliongoza kwa kupata kura 361 akifuatiwa na Sarakikya alijinyakulia kura 259.

Wagombea wengine na kura walizopata katika uchaguzi wa awali kwenye mabano ni pamoja na Elirehema Kaaya (205), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Elishilia Kaaya (176), Antony Msami (22) na Elishiankira Urio aliyeambulia kura 11.

Msami tayari amehamia Chadema alikochukua fomu kuomba uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama hicho na kuambulia kura 8 katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya chama hicho zilizopigwa juzi eneo la Maji ya Chai wilayani Arumeru.

Kamatakamata ya Takukuru

Katika hatua nyingine, kitendo cha kuwakamata baadhi ya viongozi na makada wa chama hicho juzi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa lengo la kumsaidia mmoja wa wagombea jana kilibadilisha upepo miongoni mwa wapiga kura ambao wengi walidai kitendo hicho kililenga kumnufaisha mmoja wa wagombea na hivyo kuazimia kuonyesha hasira yao kwenye sanduku la kura.

Miongoni mwa viongozi na makada wa CCM aliyekamatwa kwa kudaiwa kujihusisha isivyo halali katika kampeni za Siyoi ni pamoja na Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kwa jina la ‘Askofu’ aliyesema baada ya kutiwa mbaroni kwa maagizo ya watu aliowaita wakubwa, alihojiwa kwanini anamfanyia kampeni mgombea huyo na aliyemtuma kufanya hivyo.

Ingawa kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa Kasomambuto alikataa kuwataja viongozi wengine walioshikiliwa juzi kwa mahojiano, waandishi wetu waliofika ofisi za taasisi hiyo walimshuhudia mmoja wa waliogombea katika awamu ya kwanza ya kura za maoni pamoja katibu wa UVCCM katika moja za Wilaya za Mkoa wa Arusha wakihojiwa na maafisa wa idara hiyo ya dola.

Katika orodha hiyo pia walikuwapo madiwani wawili wa Kata za Arumeru na jana eneo lote la mkutano ulijaa maafisa wa Takukuru, na askari kanzu waliokuwa wakiranda kila kona na kujisogeza kwenye kila kundi la watu zaidi ya wawili walioonekana kuzungumza kwa lengo la kunasa mazungumzo yao.

Maofisa wa Takukuru jana waliendela na kamatakamata hadi muda mfupi kabla ya matokeo ambapo mmoja wa kada maarufu wa vijana wa CCM wilayani Arumeru, Ally Majeshi alitiwa mbaroni kwa mahojiano baada ya kudaiwa kutajwa na baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa juzi.

Shamrashamra
Baada ya matokeo, Siyoi alitoka ukumbini akiwa amebebwa juu juu na wafuasi wake kwa umbali wa zaidi ya kilomita mbili huku watu wanaoaminika kuwa wafuasi wa Sarakikya wakiwa wamebaki eneo la ukumbi wa mkutano katika makundi wakijadiliana.

Akizungumzia matokeo hayo, Sarakikya alikubali kushindwa na kumpongeza mgombea mwenzake akimtakia kila la kheri katika uchaguzi ujao wakati mshindi akiwashukuru wajumbe kwa imani waliyoonyesha kwake akiwataka kuanza kampeni za kutafuta ushindi wa CCM.
Chanzo: Mwananchi

Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits