WACHUMI kutoka China na Vietnam wamesema umasikini unaoikabili Tanzania
unatokana pamoja na mambo mengine, viongozi kuwa na maneno mengi kuliko
vitendo.Walisema hayo jana mbele ya Rais Jakaya Kikwete na kukosoa
mchakato wa ubinafsishaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu ambao
umebinafsisha na kuua viwanda vingi vya msingi.
Wakichangia mada
katika mkutano wa 17 wa mwaka wa Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini
Tanzania (Repoa), wachumi hao waliokuwa wamealikwa kueleza uzoefu wao
katika masuala ya kuondoa umasikini, walisema Tanzania haikuwa nchi ya
kutegemea misaada kutoka kwa wahisani, bali ilipashwa kujitegemea.
Akitoa
uzoefu wake, Profesa Do DucDinh wa Taasisi ya Kimataifa ya Uchumi ya
Vietnam alisema inasikitisha kuona Tanzania ina kila rasilimali lakini
ni masikini wa kutupwa.
“Nchi imebinafsisha viwanda bila ya
umakini na matokeo yake viwanda vingi vimekufa. Kwetu suala la
ubinafsishaji tulikuwa makini na Serikali inamiliki viwanda vingi
ambavyo vinatoa ajira,” alisema Profesa DucDinh na kuongeza:
“Vietnam
hatulimi korosho lakini tuna viwanda vingi vya kubangua korosho,
tunategemea malighafi kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.”
Profesa
DocDinh aliishangaa Tanzania ambayo inalima korosho lakini
ikabinafsisha viwanda vya kubangua zao hilo ambavyo vingi vimekufa.
“Utabinafsisha
vipi viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo ambacho
kinategemewa na zaidi ya asilimia 80 ya wananchi?” alihoji.
Alisema
kama Tanzania ina nia ya dhati ya kupunguza umasikini wa wananchi wake,
inatakiwa kujipanga na kusaidia kuikuza sekta ya kilimo.
“Sekta
ya kilimo iboreshwe kwa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kujenga
miundombinu na wakulima kutumia mbegu bora na mbolea,” alisema.
Kwa
upande wake, Profesa Li Xiaoyung wa Kituo cha Kimataifa cha Kuondoa
Umasikini cha Beijing alisema maisha magumu yanayolalamikiwa na wananchi
yanatokana na mfumuko wa bei hasa vyakula… “Ugali ni chakula kikuu
lakini bei ya unga ni kubwa ambayo wengine wanashindwa kumudu,
unategemea nini?”
“Nilipokuja mwaka jana nilikuta kilo moja ya
mchele inauzwa kwa Sh1,200 lakini nimeshangaa sasa inauzwa kwa Sh2,500!
Huu ni mfumko wa ajabu.”
Alisema mfumko huo kwenye bidhaa za
chakula ndio unaowasababishia wananchi umasikini kwa sababu ni bidhaa
wanazozihitaji katika matumizi ya kila siku.
Mchina huyo alisema
sekta za mawasiliano na madini ambazo zinakua kwa kasi haziwezi
kuwaondolea umasikini Watanzania kama kilimo hakitapewa kipaumbele.
JK anena
Awali,
akifungua mkutano huo wa siku mbili, Rais Kikwete alisema Serikali
itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya kilimo ili
kuwanufaisha wananchi na wawekezaji akisema kinachotakiwa ni wananchi
kubadili mtizamo wa kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa ajili ya kupora
mali za wananchi.
“Tukiendelea kudhani kwamba wawekezaji wapo kwa
ajili ya kupora mali wakakasirika na kuondoka zao, tutaendelea kuwa
masikini,” alisema.
Rais Kikwete alisema Serikali iliamua kuacha
kufanya biashara na kuiachia sekta binafsi na yenyewe kubaki na kazi ya
kujenga na kuboresha huduma za jamii.
“Serikali ilikuwa inauza
viberiti na nyama tukabinafsisha viwanda na sasa tumebaki kuandaa
mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa
Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema mkutano huo utawasaidia watafiti wa
masuala ya uchumi kubadilishana mawazo kwa lengo la kufanikisha ajenda
muhimu ya kuondoa umasikini nchini.
Chanzo: Mwananchi
Thursday, March 29, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment