BAADA ya utata wa muda mrefu wa ama Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk
Harrison Mwakyembe amelishwa sumu au la, jana Mbunge huyo wa Kyela,
aliweka hadharani ugonjwa wake akisema unafahamika kitaalamu kwa jina la
Popular Scleroderma huku akisisitiza: “Sasa nimepona kabisa.”
Dk
Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya ngozi ambayo mwaka jana
yalizidi kumtikisa na Oktoba 9, Serikali iliamua kumpeleka Hospitali ya
Appolo, India kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Dk Mwakyembe
akiwa amevalia kofia ya pama alisema: “Si kwamba sijambo, bali nimepona
kabisa baada ya kugundulika na maradhi hayo na kutibiwa.”
“Nimerudi
juzi kutoka India na daktari wangu ameniambia nimepona, nilikuwa
nasumbuliwa na maradhi ya ‘Popular Scleroderma’ iliyosababisha ‘skin
disorder’ (ngozi kutokuwa katika hali ya kawaida), lakini kwa nguvu za
Mungu nimepona, namshukuru Mungu.”
Kuhusu sumu
Alipoulizwa
kuhusu tuhuma za kulishwa sumu, Dk Mwakyembe alikataa kuzungumzia hilo
akisema anasubiri uchunguzi ulioagizwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Shamsi Vuai Nahodha.
Hata hivyo, Dk Mwakyembe alisema angependa kuona uchunguzi huo unakamilika haraka na ripoti yake inatangazwa kwa umma.
Alisema
yuko tayari na anasubiri tume hiyo ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri
Nahodha imhoji ili atoa kile kilichomo katika ripoti ya daktari wake.
Dk
Mwakyembe alisema anachoshukuru hadi sasa ni kwamba afya yake
imeimarika kutokana na shinikizo la Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza
Serikali kumpa kipaumbele wakati wote akiwa nchini na India hatua ambayo
imemwezesha kufika hapo alipo.
Kutokana na hali hiyo, Dk
Mwakyembe aliwataka wananchi wote wakiwemo wa jimboni kwake Kyela
kuondoa wasiwasi akisema sasa yupo imara kwa ajili ya ujenzi wa majukumu
ya taifa.
“Ninaomba wapiga kura wangu wa Kyela waache jazba,
wawe na subira juu ya matatizo yangu. Wiki ijayo nitakwenda kuzungumza
nao ili niweze kuwaeleza matatizo yaliyokuwa yananisumbua, lakini sasa
hivi niko fit,” alisema.
Mtaalamu auzungumzia
Mtaalamu
wa afya ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ugonjwa huo wa
‘Popular Scleroderma’ unasababishwa na chembechembe hai nyeupe
kushambulia kitu kigeni kilichoingia kwenye mwili na kusababisha
magonjwa ya ngozi.
Alisema chembechembe hizo zinaweza kusababisha
ngozi ya mwili kuharibika... “Ni magonjwa yanayosababishwa na
chembechembe hai nyeupe kujikataa zenyewe na kusababisha ugonjwa wa
ngozi na mifupa.”
Kauli hiyo ya Dk Mwakyembe kuhusu ugonjwa wake
imefungua ukurasa mpya hasa baada ya baadhi ya wanasiasa kuamini kuwa
hakuwa na tatizo jingine bali, amelishwa sumu. Tayari Mkurugenzi wa
Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba ambaye alitoa ripoti akisema Naibu
Waziri huyo hakulishwa sumu kama inavyodaiwa, amefanyia uchunguzi madai
hayo na kukabidhi jalada lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP
ili afungue kesi.
Kauli ya Sitta
Mmoja wa
wanasiasa waliodai kuwa Dk Mwakyembe amelishwa sumu, Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta alipoulizwa jana juu ya
kauli hiyo mpya ya Dk Mwakyembe alisema hana cha kuzungumza.
Januari
28, mwaka huu akiwa kwenye uzinduzi wa Programu ya Neno la Hekima
kutoka kwa Kiongozi iliyoanzishwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima la Kawe,
Dar es Salaam Sitta alisema Dk Mwakyembe amelishwa sumu.
Akizungumza
kwa utaratibu, Sitta alisema hana mengi ya kuzungumza kuhusu ugonjwa
unaomsumbua Dk Mwakyembe na kusisitiza kuwa isubiriwe ripoti kutoka
India ambako alikuwa akitibiwa.
“Dk Mwakyembe si anatibiwa
India?,” alihoji na kuendelea, “Nadhani umeshapata jibu, tusubiri… acha
huko India waendelee na uchunguzi wao, siwezi kusema lolote zaidi ya
hilo nililokuambia.”
Dk Mwakyembe alianza kuugua Oktoba 9, mwaka
jana na alitibiwa Apollo hadi aliporejea Desemba 11, mwaka jana.
Alirejea tena India kuendelea na matibabu hadi Ijumaa iliyopita
aliporudi na kusema kuwa amepona.
Matatizo yake ya kiafya
yamesababisha mvutano baina ya viongozi wa Serikali. Wakati Manumba
akisema ripoti kutoka Wizara ya Afya ilionyesha hakupewa sumu, waziri
mwenye dhamana na afya Dk Haji Mponda alimkana.
Pia Waziri
Nahodha ambaye ana dhamana na jeshi hilo la polisi, alikana ripoti hiyo
ya DCI Manumba na kutaka aulizwe mwenyewe alikoitoa huku akisema
uchunguzi alioagiza bado unaendelea.
Ugonjwa wa Scleroderma
Kwa
mujibu wa mtandao wa Johns Hopkins wa www.hopkinsscleroderma.org,
Scleroderma ni ugonjwa unaohusisha mfumo wa kinga ambao wakati mwingine
dalili zake zinaweza kuwa mtu kuwa na baridi yabisi na sugu. Ni ugonjwa
unaoathiri mwili, hasa muunganiko wa tishu na kuufanya kuwa mgumu.
Mfumo wa Kinga
Scleroderma
iko katika kundi la ugonjwa wa mfumo wa kinga. Hii ina maana kwamba
mfumo wa kinga wa mtu hufanya kazi kwa kujitegemea. Hulinda mwili dhidi
ya maadui mbalimbali kama virusi na maambukizi.
Kuwa na ugonjwa
huo wa mfumo wa kinga maana yake ni tishu au kinga kuvamiwa na wageni,
ama virusi au maambukizi mengine na hivyo kusababisha matatizo.Mtu
anapokuwa na scleroderma, seli huathirika kwa sababu katika hali ya
kawaida seli haipaswi kuwa na kitu kingine cha ziada katika mfumo wake
wa utendaji kazi na kama ikitokea hivyo, mtu huyo hujikuta katika
matatizo yanayosababisha mfumo wa mwili wake kutokuwa kama ulivyo
kawaida.
Unawezaje kuupata?
Watu wachache
hupata ugonjwa huu na hakuna anayejua unatokana na nini. Scleroderma ni
ugonjwa nadra. Chini ya watu 500,000 Marekani wanasumbuliwa nao na
hakuna anayejua kwa uhakika chanzo chake.
Baadhi ya wataalamu
wanabainisha kuwa watu kati ya saba wenye kusumbuliwa na ugonjwa huo ni
wanawake. Wenye kusumbuliwa zaidi na ugonjwa huo ni wale wenye umri wa
kati ya miaka 35 na 50. Hata hivyo, watoto wadogo na watu wazima zaidi
wanaweza kuupata.
Baadhi ya familia zimekuwa zikiathirika zaidi na
ugonjwa huu kuliko zingine. Ingawa scleroderma hauonekani kuathiri
kifamilia, lakini mara nyingi hutokea katika familia ambayo imewahi kuwa
na mtu mwenye magonjwa yanayokaribiana nao kama vile tezi au mengine
yanayofahamika kitaalamu kama arthritis rheumatoid au lupus ambayo
msingi wake ni kuathirika kwa mfumo wa kinga.
Dalili za awali
Kwa baadhi ya watu kuna dalili mbili za kwanza:
• Vidole kuwa vya baridi na wakati mwingine kubadilika rangi au mtu kuonekana mwenye msongo wa mawazo.
• Vidole na mikono kuwa migumu na kutoa magamba au unga
Mabadiliko
ya rangi ya kidole husababishwa na kupungua kwa uwezo wa mishipa ya
damu kupitisha damu ipasavyo. Hii hutokea kwa sababu ya madhara
yaliyotokea dhidi ya mishipa ya damu iliyoharibiwa kutokana na ugonjwa
huo.
Hali ya ubaridi na mabadiliko ya rangi huitwa raynaud’s
(hutamkwa ray-knowds). Watu wengi wenye hali hii wanaweza kudumu nayo
bila kuwa na ugonjwa wa scleroderma.
Athari tofauti
Athari
ya scleroderma inatofautiana sana kati ya watu. Wengi huanza kuona
dalili za vidole kubana na hata kuvimba. Kisha kwa baadhi ya watu
huchukua miezi sita wakati wengine hata zaidi ya mwaka ugonjwa
kujitokeza rasmi.
Chanzo: Mwananchi
Monday, March 19, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment