MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi imewaagiza madaktari walioitisha mgomo nchi nzima, kuusitisha mara moja.
Mbali na kusitisha mgomo huo, madaktari hao wameagizwa kutumia
vyombo vya habari ilivyotumia kutangaza mgomo huo, kuutangazia umma
kwamba mgomo huo haupo tena na kwamba wanarejea kazini.
Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya madaktari hao kuanza rasmi
mgomo wao wakishinikiza kujiuzulu kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, kama moja ya sharti la
kuendelea na mazungumzo na Serikali juu ya
madai yao mbalimbali ya maslahi.
Uamuzi wa Mahakama hiyo ulitolewa jana usiku na Jaji Regina
Rweyemamu baada ya kusikiliza maombi ya Serikali yaliyowasilishwa
mahakamani hapo Jumatano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema, kupinga mgomo huo uliotangazwa juzi na madaktari hao, kinyume
cha utaratibu.
Katika maombi yaliyowasilishwa mahakamani juzi chini ya hati ya
dharura, Jaji Werema, alidai kuwa mgomo huo ni hatari kwa maisha ya watu
na unafanyika wakati majadiliano yameanza kati ya madaktari na
Serikali na huku kukiwa na kesi Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA)
ambayo haijamalizika.
Pia alidai kuwa mgomo ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu kwani
madaktari hao wana kiapo cha taaluma yao, ambacho kinaeleza kuwa wao ni
sehemu ya taaluma ambazo haziruhusiwi kugoma.
Awali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alifungua kesi katika Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi, Jumanne iliyopita, lakini licha ya kupelekewa hati
ya kuitwa katka shauri hilo, madaktari hao hawakutokea na zaidi ya hapo
wakatangaza mgomo.
Kutokana na hilo, Serikali ililazimizika kwenda Mahakama Kuu
Divisheni ya Kazi chini ya hati ya dharura juzi kuiomba izuie mgomo huo.
Mbali na kugoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alidai madaktari hao
walikuwa na njia za kufanya kabla ya kugoma ikiwemo, kwenda Tume ya
Usuluhishi na Uamuzi au kwenda katika Kamati inayoshughulika Huduma
Maalumu.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni Chama cha Madaktari (MAT) na Jumuiya ya Madaktari ambayo
Serikali inadai kuwa ni batili kwa kuwa haijasajiliwa.
Katika kesi hiyo, Serikali iliwakilishwa na Wakili Mwandamizi, Edson
Mweyunge na walalamikiwa, MAT walihudhuria katika shauri hilo.
Mwishoni mwa wiki, madaktari walitangaza kuanza mgomo juzi baada ya
Serikali kukataa matakwa yao ya kujiuzulu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii, Dk. Hadji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete leo anatarajia kuzungumza na Taifa kupitia Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alisema jana kwenye maadhimisho ya Siku
ya Wanawake Duniani kimkoa kuwa Rais Kikwete atazungumza na
Watanzania wote kupitia wazee hao na kuwataka wafungulie vyombo vya
habari kumsikiliza.
“Naomba nitoe tangazo muhimu sana, wanawake wote na Watanzania wote kwa ujumla kesho
(leo) mfungue televisheni na redio zote, mumsikilize Rais Jakaya
Kikwete atazungumza na Taifa kupitia Wazee wa Dar es Salaam, tafadhali
mfanye hivyo,” alitangaza Sadiki aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo
ya wanawake iliyofanyika kimkoa katika Viwanja vya Mnazi
Mmoja, Dar es Salaam.
Sadiki alitoa tangazo hilo kwa msisitizo mara baada ya kuhutubia
hadhara hiyo ambayo pamoja na mambo mengine, yeye (RC) alizungumzia
suala la mgomo wa madaktari na kuhamasisha wanawake kushiriki katika
maoni ya Katiba mpya pindi mchakato utakapoanza.
RC Sadiki alisema Rais Kikwete atazungumza na wazee hao asubuhi,
lakini hakueleza atakutana nao wapi wala maudhui ya kukutana nao, ingawa
imekuwa ni kawaida ya kiongozi huyo wa nchi kukutana na wazee wa mikoa
mbalimbali ikiwemo ya Dar es Salaam na Dodoma na kupitia kwao,
huzungumzia masuala ya kitaifa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu
alipoulizwa kuhusu Rais kukutana na wazee hao wa Dar es Salaam, alisema
kama Mkuu wa mkoa ametangaza hivyo, basi anukuliwe alivyosema.
Kwa sasa, suala la mgomo wa madaktari ulioanza jana nchini kote
ndilo linalogonga vichwa kwa sasa na limetokea licha ya rai ya Serikali
kupitia kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwasihi madaktari hao kutogoma
kwa sababu matatizo yao yanashughuliwa.
Katika hatua nyingine, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na
Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (TUGHE), vimewanasihi
madaktari wanaogoma na kuwataka wazingatie kiapo chao cha kuhudumia
jamii na kurejea kazini.
Katibu Mkuu wa Bakwata, Shehe Suleiman Lolila, alisema jana kwamba
pamoja na madaktati hao kuwa na hoja ya msingi kuhusu madai yao, jambo
la msingi zaidi wangeweka maslahi ya Watanzania mbele.
“Tayari Serikali imeonesha dalili ya kuzungumza nao, kuhusu madai
waliyoyawasilisha, wangetumia fursa hiyo na kurejea kazini, kwa kuwa wao
bado wanabaki kuwa watu muhimu na kugoma kwao kunaweza kuleta maafa
makubwa katika jamii,” alisema.
Aliwataka kuangalia kiapo chao, lakini pia kujifunza kuwa na subira
wakati masuala yao yakishughulikiwa, kwani hata dini imeweka wazi kuwa
mtu anapokuwa na subira hupata mafanikio na thawabu kubwa.
Katibu Mkuu wa Tughe, Ali Kiwenge, alisema mgogoro wa madaktari kwa sasa unaumiza zaidi
wananchi hasa kisaikolojia.
“Kwa sasa mtu hata ukipigiwa simu tu ukaambiwa mtoto, baba au mama
anaumwa, unaanza kuwaza utafanyaje, kwa mgogoro huu nchi iko kwenye
wasiwasi mkubwa bila sababu za msingi,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholaus
Mgaya, alipotakiwa kutoa maoni na ushauri wake, alisema atazungumza na vyombo vya
habari leo kuhusu mgomo huo.
Kwa upande wa hali katika hospitali nchini, Taasisi ya Tiba ya
Mifupa ya Muhimbili (MOI) jana ilisitisha huduma za wagonjwa wa nje
kutokana na kupungukiwa madaktari.
Ofisa Uhusiano wa MOI, Almas Jumaa, alisema katika taasisi hiyo
wameathirika sana na mgomo kwani wamebaki madaktari 10 ambao ni wakuu wa
vitengo na Idara kati ya madaktari 72 waliopo.
Katika hospitali nyingine za Dar es Salaam, wagonjwa walirudishwa
nyumbani na kutakiwa kurudi hospitalini baada ya kusikia kwenye vyombo
vya habari kuwa huduma zimerejea.
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, wagonjwa walikutwa wamekaa nje kwenye viti vyao
huku ndugu wakitafuta jinsi ya kuwahamishia katika hospitali zingine za binafsi.
Aidha, RC Sadiki aliwaondoa hofu madaktari wanaoendelea kutoa huduma katika hospitali za
mkoa huo, licha ya kushinikizwa wagome, na kusema Serikali itawapa ulinzi, kwa kuwa wamekuwa wakipokea vitisho.
Aliwaomba waendelee kuokoa maisha ya Watanzania wenzao, kulingana na kiapo walichokula
kwa kuwa tayari Serikali imekubali kushughulikia madai yao hivyo kugoma si ufumbuzi.
Mikoani katika hospitali za Bugando Mwana, KCMC Moshi, Dodoma na Morogoro kulikuwa na
mgomo baridi.
Chanzo: HabariLeo
Friday, March 9, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment