KWA mara ya pili, wana CCM Jimbo la Arumeru Mashariki wamedhihirisha
kuwa chaguo lao ni Siyoi Sumari baada ya kumchagua kwa kura 761 na
kumtupa mbali mpinzani wake, William Sarakikya aliyepata kura 361 katika
uchaguzi wa marudio uliofanyika jana.Matokeo hayo ni kama ushindi kwa
mojawapo ya kambi ndani ya CCM inayohusishwa na Waziri Mkuu
aliyejiuzulu, Edward Lowassa dhidi ya wanachama waliopo katika makundi
mengine, ambayo yalikuwa yakipinga kwa nguvu zote kupitishwa kwa jina la
Siyoi.
Vyombo mbalimbali vya habari kwa wiki nzima sasa,
vimekuwa vikiripoti kuhusu mgawanyiko ndani ya chama hicho tawala
kutokana kuwa na misimamo inayokinza kuhusu nani atakayepeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi huo mdogo.
Siyoi alianza kuzua
mtafaruku ndani ya CCM pale suala la uraia wake lilipozua utata ndani ya
kikao cha Sekretarieti ya chama hicho, hivyo kusababisha kutolewa kwa
mapendekezo kwamba aenguliwe katika kinyang’anyiro hicho.
Kundi
linalomtetea limekuwa likilalamikia kile linachodai kwamba ni kuwapo kwa
njama za kumtosa mshindi huyo kwa sababu kadhaa za kimakundi.
Hata
hivyo, Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichokutana chini ya Mwenyekiti,
Rais Jakaya Kikwete kiliamuru kurudiwa kwa uchaguzi baina ya Siyoi na
Sarakikya, kwa maelezo kwamba katika wagombea wote sita hakuna aliyekuwa
amepata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa.
Habari zaidi zilidai
kuwa, hata baada ya kutolewa kwa uamuzi wa kurudiwa kwa uchaguzi huo,
mmoja wa vigogo wa CCM alituma mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu kwenda
kumshawishi Siyoi ajitoe kwenye kinyang’anyiro hicho, jitihada ambazo
hazikufanikiwa kwani alikataa.
Matokeo ya kura
Matokeo
ya uchaguzi huo yaliyotangazwa Saa 11:30 jioni na Makamu Mwenyekiti wa
CCM, Pius Msekwa, Sumari aliibuka na ushindi huo wa silimia 67.8 kati ya
kura halali 1,122 zilizopigwa, dhidi ya asilimia 32.2 za mpinzani wake
anayedaiwa kupigiwa chapuo na viongozi wa chama na Serikali kuanzia
ngazi ya Wilaya, Mkoa hadi taifa.
Jumla ya kura 1,124 zilipigwa ambapo mbili ziliharibika na kura halali kubakia 1,122.
Akitangaza
matokeo hayo, Msekwa alilazimika kuanza kwa kumtangaza mshindi hali
iliyofanya ukumbi kukosa usikivu kwa wapenzi, mashabiki na wafuasi wa
Siyoi kuanza kushangilia.
Msekwa alisema ameridhishwa na upigaji kura na matokeo hayo yameonyesha imani kubwa waliyonayo wana Arumeru kwa mgombea huyo.
Baadhi
ya wana CCM walidai kuwa kauli tata za Msekwa na Naibu Katibu Mkuu wa
CCM (Bara), John Chiligati katika ufunguzi wa mkutano mkuu maalum wa
Wilaya ya Arumeru jana zilimponza, Sarakikya baada ya wajumbe kuamua
kupiga kura za hasira wakipinga kile walichodai kushinikizwa kumchagua
mtu aliyeelezwa anatakiwa na mfumo (system), wa Serikali na uongozi wa
chama.
Awali wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ufunguzi
wa mkutano huo uliohudhuriwa na idadi kubwa ya maofisa wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), maofisa usalama wa taifa na
askari kanzu kutoka Jeshi la Polisi, Msekwa na Chiligati waliwataka
wajumbe kutumia vyema kura yao kumchagua mtu atakayemudu na kuhimili
vishindo vya upinzani kutoka vyama vingine vitakavyosimamisha wagombea.
“Ndugu
wajumbe napenda kuwakumbusha jambo moja muhimu kabla ya kupiga kura,
leo hatuchagui mbunge, mnachofanya ni kupiga kura za maoni. Mgombea
atateuliwa na kikao cha Kamati Kuu Machi 3, mwaka huu,” alisema
Chiligati.
Wakati Chiligati akisititiza hoja hiyo, Msekwa
alikuwa akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na maneno aliyokuwa
akiyasema Naibu Katibu Mkuu huyo huku baadhi ya wajumbe wakiguna.
Msekwa
aliyetumia muda mwingi kuzungumzia historia yake ya uongozi ndani ya
chama kuanzia TANU hadi CCM aliwataka wajumbe kutoangalia uswahiba wala
ushawishi wa aina yoyote katika maamuzi yao bali wahakikishe
wanayemchagua anastahili kupeperusha bendera ya chama hicho tawala na
kukiletea ushindi.
Katika uchaguzi wa awali wa kura za maoni uliofanyika Februari 20, mwaka
huu, Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia
Sumari aliyefariki hivi karibuni aliongoza kwa kupata kura 361
akifuatiwa na Sarakikya alijinyakulia kura 259.
Wagombea wengine
na kura walizopata katika uchaguzi wa awali kwenye mabano ni pamoja na
Elirehema Kaaya (205), Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa Arusha (AICC), Elishilia Kaaya (176), Antony Msami (22) na
Elishiankira Urio aliyeambulia kura 11.
Msami tayari amehamia
Chadema alikochukua fomu kuomba uteuzi wa kupeperusha bendera ya chama
hicho na kuambulia kura 8 katika uchaguzi wa kura za maoni ndani ya
chama hicho zilizopigwa juzi eneo la Maji ya Chai wilayani Arumeru.
Kamatakamata ya Takukuru
Katika
hatua nyingine, kitendo cha kuwakamata baadhi ya viongozi na makada wa
chama hicho juzi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa
lengo la kumsaidia mmoja wa wagombea jana kilibadilisha upepo miongoni
mwa wapiga kura ambao wengi walidai kitendo hicho kililenga kumnufaisha
mmoja wa wagombea na hivyo kuazimia kuonyesha hasira yao kwenye sanduku
la kura.
Miongoni mwa viongozi na makada wa CCM aliyekamatwa kwa
kudaiwa kujihusisha isivyo halali katika kampeni za Siyoi ni pamoja na
Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kwa jina la ‘Askofu’
aliyesema baada ya kutiwa mbaroni kwa maagizo ya watu aliowaita wakubwa,
alihojiwa kwanini anamfanyia kampeni mgombea huyo na aliyemtuma kufanya
hivyo.
Ingawa kamanda wa Takukuru Mkoa wa Arusha, Mbengwa
Kasomambuto alikataa kuwataja viongozi wengine walioshikiliwa juzi kwa
mahojiano, waandishi wetu waliofika ofisi za taasisi hiyo walimshuhudia
mmoja wa waliogombea katika awamu ya kwanza ya kura za maoni pamoja
katibu wa UVCCM katika moja za Wilaya za Mkoa wa Arusha wakihojiwa na
maafisa wa idara hiyo ya dola.
Katika orodha hiyo pia walikuwapo
madiwani wawili wa Kata za Arumeru na jana eneo lote la mkutano ulijaa
maafisa wa Takukuru, na askari kanzu waliokuwa wakiranda kila kona na
kujisogeza kwenye kila kundi la watu zaidi ya wawili walioonekana
kuzungumza kwa lengo la kunasa mazungumzo yao.
Maofisa wa
Takukuru jana waliendela na kamatakamata hadi muda mfupi kabla ya
matokeo ambapo mmoja wa kada maarufu wa vijana wa CCM wilayani Arumeru,
Ally Majeshi alitiwa mbaroni kwa mahojiano baada ya kudaiwa kutajwa na
baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa juzi.
Shamrashamra
Baada
ya matokeo, Siyoi alitoka ukumbini akiwa amebebwa juu juu na wafuasi
wake kwa umbali wa zaidi ya kilomita mbili huku watu wanaoaminika kuwa
wafuasi wa Sarakikya wakiwa wamebaki eneo la ukumbi wa mkutano katika
makundi wakijadiliana.
Akizungumzia matokeo hayo, Sarakikya
alikubali kushindwa na kumpongeza mgombea mwenzake akimtakia kila la
kheri katika uchaguzi ujao wakati mshindi akiwashukuru wajumbe kwa imani
waliyoonyesha kwake akiwataka kuanza kampeni za kutafuta ushindi wa
CCM.
Chanzo: Mwananchi
Thursday, March 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment