BODI ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited
(MCL), imemteua mwandishi wa habari mkongwe barani Afrika, Dunstan Tido
Mhando, kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni hiyo.Tido alianza kazi
rasmi jana, muda mfupi baada ya kumalizika kwa hafla ya kumkaribisha,
iliyofanyika katika ofisi za kampuni hiyo zilizoko Tabata Relini jijini
Dar es Salaam.
Tido anachukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa
na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Sam Shollei ambaye mkataba wake wa kazi
ulimalizika mwishoni mwa mwaka jana. Shollei kwa sasa ni mmoja wa
wakurugenzi wa kampuni ya Nation Media Group (NMG)
Kabla ya kujiunga na MCL, Tido alishafanya kazi ya uandishi wa habari ndani na nje ya nchi kwa zaidi ya miaka 30.
Amewahi
kufanyakazi katika iliyokuwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) kisha
kwenda nje ya nchi na kufanikiwa kupata heshima ya kuwa Mwafrika wa
kwanza, kuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC). Akiwa BBC, Tido aliingia katika historia ya habari kwa
kuwa mwandishi wa habari ambaye amefanya mahojiano ya ana kwa ana
marais wengi wa Afrika.
Mbali na BBC, Tido amewahi pia kufanya
kazi katika mashirika mengine ya habari ya nje ambayo ni pamoja na Idhaa
ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na Redio Deutche Welle (DW) ya
Ujerumani.
Akizungumza ofisini kwake Tabata Relini jana, Tido
alisema: "Ninafurahi kujiunga na kampuni ya Mwananchi na nitatumia
uzoefu wangu kuiinua kampuni kwa kuongeza kiwango cha weledi wa habari."
Kuhusu
historia yake, Tido alisema alianza kazi ya uandishi wa habari mwaka
1969 Redio Tanzania, akiwa mtangazaji, akabobea hasa katika michezo,
hasa mpira wa miguu.
"Niliwahi kutangaza mpira katika nchi nyingi
ikiwamo Uganda katika Kombe la Chalenji mwaka 1973, mashindano ya Nchi
za Jumuiya ya Madola mwaka 1974 na nilikuwa nasafiri na Taifa Stars
katika nchi kadhaa ikiwamo Nigeria, Sudan, Kenya na Malawi," alisema
Tido.
Wakati akiripoti kwenye Michezo ya Madola huko
Christchurch, New Zealand mwaka 1974, Tido alikuwa shuhuda wakati
mwanariadha wa Tanzania, Filbert Bayi alipovunja rekodi ya dunia ya mbio
za mita 1,500 alipomsambaratisha bingwa wa dunia wa wakati huo. "Mwaka
1976 nilichaguliwa kwenda kutangaza mashindano ya Olimpiki nchini
Canada, ingawa Tanzania ilijitoa na mwaka 1978 nilienda kutangaza
mashindano ya nchi za Jumuiya za Madola huko Edmonton, Canada, kabla
sijaenda nchini Kenya mwaka 1979 kutangaza mechi za Kombe la Chalenji na
Taifa Stars."
Katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1978
nchini Canada, Tido alitangaza moja kwa moja wakati Mtanzania Gidamis
Shahanga alipotwaa medali ya dhahabu kwenye marathon na Bayi alipata
medali ya fedha kwenye mbio za mita 1500.Tido alisema baada ya
mashindano hayo, alichukuliwa na kampuni ya High Fidelity Production Ltd
ya nchini Kenya akiwa mtengenezaji wa vipindi na baadaye kuanza kufanya
kazi ya uandishi wa habari kwa kujitegemea akiyawakilisha mashirika ya
BBC, VoA na Dutch Welle.
"Nilikaa Kenya kwa miaka kumi kuanzia
1980 hadi 1990, wakati huo nikiwa mwakilishi wa mashirika hayo katika
nchi zote za Afrika Mashiriki na Kati. Moja ya habari maarufu nilizowahi
kutangza nikiwa Kenya, ni ile ya kuibua taarifa ya kifo cha kutatanisha
cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Dr Robert Ouko
kunako mwaka 1990," alisema Tido.
Tido alisema mwaka 1990 hadi
2007, alijiunga na BBC na anajivunia kuwa Mwafrika wa kwanza kuliongoza
shirika hilo katika Idhaa ya Kiswahili na kufanikiwa kuongeza idadi ya
wasikilizaji kutoka milioni saba hadi milioni 21 kwa juma."Ilipofika
mwaka 2007, Rais Jakaya Kikwete alinifuata London, Uingereza, na
akanitaka nirudi nchini kuliongoza Shirika la Habari la Taifa (TBC),"
alisema, na kuongeza:
"Ninafurahi kuja Mwananchi, kampuni kubwa ya habari nchini na nitatumia
uzoefu wangu kutoa mchango wangu katika kukuza demokrasia ya kweli
nchini kwa faida ya Watanzania na taifa kwa ujumla."
Akizungumzia
ujio wa Tido, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo,
Theophil Makunga, alisema kampuni ya Mwananchi ina kila sababu ya
kufurahia kumpata mkurugenzi huyo mpya kwani atasaidia kuharakisha
mafanikio ya kampuni.
"Tumepata mtu makini na mwenye msimamo
katika taaluma ya habari na tunaamini atatusaidia sana. Hakika tumempata
mtu sahihi kwa wakati sahihi," alisema Makunga.
Chanzo: Mwananchi
Thursday, March 22, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment