UPATIKANAJI wa huduma za afya nchini uliendelea jana isipokuwa katika
Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza na Amana Ilala, Dar es Salaam huku
Muhimbili huduma zikitolewa kwa kusuasua.Jana, ilikuwa siku ambayo
madaktari hao walitangaza kuanza mgomo nchi nzima wakishinikiza madai
yao ya kutaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu
wake, Dk Lucy Nkya wajiuzulu au wawajibishwe licha ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kuwasihi wabadili msimamo huo kwa maslahi ya wananchi.
Hata
hivyo, akizungumzia na waandishi wa habari muda mfupi baada ya
kumalizika kwa mkutano wa madaktari uliofanyika Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi
alisema wamekubaliana kurejea kwenye mgomo kuanzia jana mchana hadi hapo
dai lao la msingi la kuwajibika au kuwajibishwa kwa mawaziri hao
litakapotekelezwa.
“Madaktari wanasikitika kutoa taarifa kuwa sasa
wanarejea kwenye mgomo na utakuwa kwa nchi nzima hadi dai lao
litakapotekelezwa. Wanawaomba wananchi kuelewa kuwa lengo lao ni kutaka
kuboresha huduma za afya nchini. Uzorotaji wa huduma za afya nyote
mnaufahamu, hata wakilazimishwa hakuna kitakachoendelea tunaomba nia ya
madai yetu yasipotoshwe.”
Alisema hayo akipinga kauli ya Waziri
Mkuu, Pinda aliyoitoa juzi kwamba madai hayo ya kutaka Dk Mponda na Dk
Nkya wang’olewe ni mpya na kusema imewafanya pia watilie shaka
utekelezwaji wa madai mengine.
“Madaktari wamesikitishwa na kauli
ya Waziri Mkuu Pinda kuwa dai la madaktari kutaka Waziri, Dk Mponda na
Naibu wake, Dk Nkya ni jipya. Hii si kweli dai hilo lipo kwenye madai
yote ya madaktari na yeye alilipata katika nyaraka zake zote
alizokabidhiwa. Hata kauli yake aliyoitoa Februari 9, mwaka huu
inaonyesha anatambua dai hilo na kuonyesha nia ya kulitatua.”
Alisema
kinachofanyika sasa ni kushinikiza kutekelezwa kwa dai la kwanza kati
ya matatu waliyokubaliana na wawakilishi kutoka serikalini ambalo ni
hilo la kuwajibika au kuwajibishwa kwa viongozi hao.
Serikali imejiandaa
Akizungumzia
mgomo huo jana, Pinda aliwaambia waandishi wa habari, Dar es Salaam
kwamba Serikali imejipanga kukabiliana nao.Alisema juzi alipozungumza na
waandishi ofisini kwake, tayari Serikali ilikuwa na mipango yake na
ilichokuwa ikisubiri ni kuona matokeo ya mgomo huo kuanzia jana.
“Serikali
imejipanga kukabiliana na mgomo huo. Pale jana (juzi) nilipozungumza na
waandishi ofisini kwangu sikutaka kueleza mipango yote na kila kitu,
lakini tulikuwa tunawasubiri tu wagome,” alisema Pinda.
Hata
hivyo, alisema ni matumaini yake kwamba bado milango ya mazungumzo iko
wazi na jambo hilo linaweza kupatiwa suluhu bila mgomo na kuwataka
madaktari waendelee na kazi.
Alisisitiza kwamba ni makosa
kitaaluma kwa daktari kugoma na kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na
hatia: “Ningewashauri madaktari waendelee na kazi.”
Dar es Salaam
Jana
katika Hospitali ya Amana kulizuka vurugu baada ya wagonjwa na jamaa
zao kuvamia mlango wa mapokezi huku wakitishia kuvunja vioo vya majengo
ya hospitali hiyo baada ya kuelezwa kuwa hapakuwa na huduma.
Hali
ilionekana kuwa mbaya hadi wanamgambo wa Manispaa ya Ilala walipofika.
Hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya wahudumu wanaopokea wagonjwa na
kuwaandikisha kabla ya kuonana na madaktari kuwaeleza wagonjwa kuwa
huduma zimesitishwa.
Kauli hiyo iliwafanya baadhi ya wagonjwa wa
nje kuondoka hospitalini hapo na baadhi yao wakiendelea kubishana na
wahudumu hao, jambo ambalo lilileta tafrani.
“Sisi tuna makosa
gani kwa nini tuambiwe huduma zimesitishwa. Sisi tunaonewa tumetangaziwa
tangu jana (juzi) kwamba kuna mgomo lakini wanaoumia ni sisi,” alisema
Justine Mushi.
Alipoulizwa kuhusu mgomo huo, Kaimu Mganga Mkuu wa
Amana, Dk Christopher Mnzava alikanusha akidai huduma zinaendelea kama
kawaida lakini alielezwa kwamba wahudumu wa mapokezi wamesema kwamba
zimesitishwa.
Alifika mapokezi na kuonana na wagonjwa ambao
walimweleza walivyoambiwa kuhusu kusitishwa kwa huduma na kutakiwa
waondoke lakini Dk Mnzava alisema hizo ni kauli zilizotolewa baada ya
kutokea vurugu na si kutokana na mgomo wa madaktari.
Katika
Taasisi ya Mifupa Muhimbili, (Moi) utoaji wa huduma ulikuwa wa kusuasua
na baadhi ya madaktari walisema walikuwa katika maandalizi ya kuanza
mgomo.
Bugando
Madaktari waliopo katika mafunzo ya vitendo Bugando jana walitangaza kuanza mgomo kuungana na wenzao.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumaliza kikao cha
kujadili mgomo huo, mmoja wa madaktari ambaye hakupenda kuandikwa jina
lake gazetini alisema wameamua kurejea katika mgomo wao mpaka hapo madai
yao yatakapotekelezwa na Serikali.
Jana hospitalini hapo
kulikuwa na tangazo lililokuwa likieleza kuanza kwa mgomo huo ambalo
hata hivyo, uongozi wa Bugando umesema ni la kihuni na haulitambui.
Ofisa
Tawala wa hospitali hiyo, Joachim Wangabo alisema mgomo huo ni batili
na kwamba watafuatilia kila hatua kujua ni nani wameingia katika mgomo
ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.
“Naomba niseme Bugando hakuna
mgomo, haya matangazo yanabandikwa tu na wahuni, ofisi yangu
inafuatilia kujua waliogoma. Wakibainika tutawachukulia hatua,” alisema.
Hata
hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Omary Salehe alisema
waliogoma ni wanafunzi 65 walioko katika mafunzo ya vitendo na kwamba
licha ya mgomo wao, huduma zinaendelea kutolewa na madaktari bingwa
licha kuwepo na hatihati ya kuzidiwa kutokana na kuongezeka kwa
wagonjwa.
Hali ya upatikanaji wa huduma hospitalini hapo jana
ilikuwa imezorota kwa kiasi kikubwa na katika baadhi ya maeneo hapakuwa
na huduma kabisa.
Mmoja wa wagonjwa, James Paul alisema alikuwa
amepangiwa kufanyiwa upasuaji leo, hivyo alitakiwa afike jana kwa ajili
ya kulazwa lakini aliambiwa aondoke na arejee baada ya wiki tatu.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, March 7, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment