VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge
Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya
makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.CCM
ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni
zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia
alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na Chadema itawatumia
viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe
na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.
Wakati huohuo, Kamati Kuu
(CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya
chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.
Mwenyekiti wa
Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho,
wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age
Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua
jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama
chochote.
Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu
wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa
kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano
miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine
vya siasa ambavyo hakuvitaja.
Alisema mara nyingi mipasuko
ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea
kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa
wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na
mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au
ukwasi wa mtu.
“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba
uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na
uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye
kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.
Akitangaza
uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha
wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na
Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya
wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888
zilizopigwa kwenye kura za maoni.
“Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema.
Katika
kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa
aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata
kura chini ya 20.
Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.
Nasari ashukuru
Akitoa
shukrani mbele ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama chake, Nasari
aliwaomba wafuasi, wapenzi na wanachama wote wa Chadema kushikamana na
kuwa tayari kwa mapambano ya haki, kuhakikisha wanaibuka na ushindi
mnono kwenye uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
"Wao
(CCM), najua watatumia dola na fedha, lakini sisi tusihofu kwani tuna
Mungu anayetupigania kwa sababu mapambano yetu ni kudai haki dhidi ya
uovu.
Kwa pamoja tukishirikiana kuondoa hofu kwani tutashinda," alisema Nasari.
CCM
Kwa
upande CCM Kamati Kuu (CC) ya chama hicho jana ilimteua Mwenyekiti
mstaafu ambaye pia ni Rais mstaafu wa awamu ya Tatu , Mkapa, kuongoza
kampeni za kumnadi Mgombea Ubunge wa chama hicho, Siyoi Sumari katika
jimbo la Arumeru Mashariki.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri
Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alisema kikao cha kamati hiyo kilichoketi jana,
kilipitisha jina la Siyoi kuwania nafasi hiyo iliyoachwa na baba yake,
Jeremia Sumari aliyefariki usiku wa Januari 18 mwaka huu.
Nape
alieleza kwamba, kamati hiyo pia imemteua Katibu wa Idara ya Uchumi na
Fedha ya chama hicho, Mwingilu Nchemba kuratibu kampeni hizo.
Katika
uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga ambao CCM ilishinda, Mkapa ndiye
aliyefungua kampeni hizo huku, Nchemba akiratibu kuanzia mwanzo hadi
mwisho.
Akizungumzia tuhuma za rushwa ambazo zimekuwa zikiripotiwa
katika mchakato wa uteuzi, aliitaka Takukuru kuhakikisha wanakamata
mtandao mzima uliohusika na utoaji rushwa.
Kauli ya Siyoi
Sumari,
aliambia Mwananchi Jumapili kuwa kwamba pamoja na kufurahishwa na
uamuzi wa Kamati Kuu ya CCM kupitisha jina lake kupeperusha bendera ya
CCM wilayani Arumeru Mashariki, chama hicho kinapaswa kutoa ushirikiano
wa dhati kuhakikisha kinatetea jimbo hilo.
Hata hivyo,
alisisitiza kwamba changamoto zote alizozipitia katika mchakato wa
uteuzi , zikiwemo tuhuma mbalimbali za rushwa ni misukosuko ya kisiasa
ambayo haiwezi kuepukwa zaidi ya kukabiliana nayo.
“Nashukuru
chama kwa kupitisha jina langu, lakini changaomoto zote nilizokuwa
nikipitia naamini ni misukosuko tu ya kisiasa, lakini tusahau yaliyopita
sasa tusonge mbele kunyakua ushindi,” alisema Sumari
UVCCM
Katika
hatua nyingine Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM ) wilayani
Arumeru, imefurahishwa na uamuzi uliofanywa na CC ya CCM kumpitisha
Siyoi kupeperusha bendera ya chama hicho na kueleza kwamba kilio cha
wanachama wa CCM wilayani humo, sasa kimesikilizwa.
Hata hivyo,
wakati jumuiya hiyo ikiupokea ushindi huo kwa furaha, Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa(Takukuru) imeendelea na kamata kamata yake
ambapo safari hii ilimshikilia na kumhoji kwa muda Katibu Hamasa wa
umoja huo wilayani Arumeru Mashariki, John Nyiti kisha kumwachia huru.
Mwenyekiti
wa Jumuiya hiyo, Esther Maleko alisema mbali na kilio cha wakazi wa
jimbo hilo kusikika juu ya mgombea wao, umoja wao umejipanga kikamilifu
kuingia ulingoni kuhakikisha ushindi unapatikana.
Hekaheka za
uchaguzi wa jimbo hilo wakati zikiendelea baadhi ya makada wa CCM na
UVCCM wilayani humo wameendelea kukumbwa na misukosuko baada ya viongozi
wake akiwemo Nyiti kushikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kujihusisha
na vitendo vya rushwa wilayani humo.
Nyiti alipoulizwa juu ya taarifa hizo kwa njia ya simu alikiri kukamatwa na maofisa wa Taasisi hiyo.
Kamanda
wa Takukuru mkoani Arusha, Mbengwa Kasumambuto alipoulizwa na gazeti
hili juu ya taarifa hizo hakuweza kukiri wala kukataa juu ya kuhojiwa
kwa kada huyo na kudai kwamba wanaohojiwa na Taasisi hiyo wako wengi na
wengine wanahojiwa kama mashahidi, hivyo alidai si vyema kuwataja
majina kwa kuwa bado wanakamilisha uchunguzi wao.
Hali ilivyo ndani ya vyama
Makundi
ya vigogo wa CCCM ambao wanajipanga kugombea Urais mwaka 2015,
yametajwa kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama hicho katika uteuzi
wa mgombea wa Ubunge Arumeru Mashariki.
Mpasuko wa makundi hayo, inaelezwa unaweza kuchangia chama hicho kupoteza jimbo hilo.
Sumari
amekuwa akiungwa mkono na kundi la Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward
Lowassa huku wagombea wengine, walikuwa wakiungwa mkono na kundi la na
vigogo wa chama hicho wanaojipambanua kuwa ni wapiganaji dhidi ya
ufisadi.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili jana katika mahojiano
maalumu baadhi ya viongozi wa CCM na makada wa Chama hicho, wameeleza
mpasuko huo ni mkubwa tofauti na wengi wanavyofikiri.
Asantaeli
Erio alifafanua kuwa, kwa sasa baada ya Sumari kupitishwa, kundi la
vigogo wa CCM na Serikali huenda wakasusa kumpigia kampeni hasa kutokana
na kubainika wazi kutomuunga mkono na siri za hoja zao kuvuja.
Wafuasi wa Sarakikya
Kundi
la wafuasi wa aliyekuwa mgombea wa ubunge wa CCM, William Sarakikya na
Elishilia Kaaya jana, walieleza kutokubaliana na maamuzi ya Kamati Kuu
kupitisha jina la Sumari kuwania jimbo hilo.
Mmoja wa wafuasi hao, Emanuel Kanangira alisema wanapinga uteuzi wa Sumari na leo wanatarajia kurejesha kadi za CCM.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, March 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment