Mbio za uspika zapamba moto
* Chenge, Ndugai wajitosa
* Jenista kuwania unaibu
MCHAKATO wa wana-CCM kuchukua fomu za kuwania nafasi ya Spika wa Bunge, umezidi kupamba moto, baada ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kuchukua fomu. Mbali na Chenge, ambaye ameshinda ubunge jimbo la Bariadi Magharibi, wengine waliochukua fomu jana ni Job Ndugai, aliyeshinda ubunge Kongwa, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bunge lililopita.
Wengine ni Kate Kamba, ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Benedict Lukwembe. Wana-CCM hao walikabidhiwa fomu na Katibu Mkuu wa Chama, Yussuf Makamba. Aliyekuwa Spika wa Bunge lililopita, Samuel Sitta, amechukua fomu kutetea nafasi hiyo. Pia aliyekuwa Naibu wake, Anne Makinda, naye anawania kiti hicho na Mwalimu wa Shule ya Sekondari Tambaza, Salimu Kungulilo. Makamba akiwakabidhi fomu kwa nyakati tofauti katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, alisema kutokana na Chama kutaka wana-CCM wengi wagombee, wameamua kuogeza siku za uchukuaji fomu.
“Mwisho wa kuchukua fomu ni Novemba 8, mwaka huu. Wanachama wote watatakiwa wawe wamemaliza kuchukua na kurudisha fomu,’’ alisema. Makamba alisema lengo ni kutoa nafasi kwa majina kupelekwa ngazi husika kwa ajili ya mchakato wa uteuzi, ambapo baadae Kamati ya Wabunge wa CCM itateua jina moja, litakalopelekwa ofisi ya Bunge. Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Chenge alisema amejitokeza kuwania nafasi hiyo kutokana na kuwa na uzoefu wa shughuli za Bunge. “Nina mambo mengi nataka kulifanyia Bunge, kwa kuwa ni kiungo muhimu kati ya mwananchi na serikali, hivyo naweza kuwa Spika na kulisimamia hili vyema,’’ alisema Chenge.
Naye, Ndugai alisema uwepo wake bungeni kwa vipindi vitatu unampa uwezo mkubwa wa kuendesha shughuli za Bunge.
“Nina uzoefu mkubwa. Nimekuwa Mwenyekiti wa Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Mazingira na Utalii na kamati nyingine za mabunge ya Jumuia ya Madola,’’ alisema Ndugai.
Wakati huo huo, Makamba alisema fomu za kuwania unaibu spika zimeanza kutolewa na Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama kwa gharama ya sh. 100,000. “Fomu za unaibu spika zimeshaanza kutolewa, lakini hizi ni kwa wabunge pekee, ambapo wabunge wanapaswa kuchukua fomu hizo,’’ alisema
Kwa upande wake, Jenista alisema fomu hizo zinapatikana Dodoma na Dar es Salaam, ambapo aliwataka wabunge wote wanaotaka kugombea waende kuchukua. Jenista aliyeshinda ubunge jimbo la Peramiho, alisema yeye atachukua fomu kuwania nafasi hiyo, kwa kuwa anataka kuendelea kulipa heshima Bunge la Tanzania kimataifa. Alikuwa Mwenyekiti wa Bunge lililopita.
Source: Uhuru
No comments:
Post a Comment