Bunge halina uwezo kutunga katiba mpya
Via Mwananchi
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halina uwezo wa kutunga Katiba mpya, bali kuifanyia marekebisho iliyopo."Bunge la Jamhuri halina uwezo wa kutunga Sheria ya Katiba hili ni jambo la msingi sidhani Zanzibar na watu wake kama watakubali kuvunja Katiba," alisema.
Masoud alisema hayo jana akitoa mchango wake katika mjadala wa maoni ya Muswada wa Sheria wa Mapitio ya Katiba unaoendeshwa na Kamati ya Bunge, Sheria na Katiba ya Bunge la Muungano
uliofanyika katika Hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Alisema msingi wa hoja yake unatokana na Kifungu cha 98(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano kinachoeleza. Kifungu hicho kinasema: "Muswada wa Sheria kwa ajili ya kubadilisha masharti yoyote ya Katiba hii au masharti yoyote ya Sheria yoyote yanayohusika na jambo lolote kati ya mambo yaliyotajwa katika Orodha ya Pili kwenye Nyongeza ya Pili iliyoko mwishoni wa Katiba hii, utapitishwa tu iwapo utaungwa mkono kwa kura za Wabunge ambao idadi yao haipungui theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar."
Orodha hiyo ya pili kwenye nyongeza ya pili iliyoko mwishoni wa Katiba inaeleza mambo ambayo mabadiliko yake yanahitaji kuungwa mkono na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania bara na theluthi mbili ya wabunge wote kutoka Tanzania visiwani moja likiwa mambo ya muungano ambalo suala la Katiba ni mojawapo.
Alisema Bunge lililopo sasa haliwezi kutunga Katiba mpya, bali kazi yake ni kurekebisha hivyo linatakiwa liwepo Bunge jingine ambalo litakuwa maalumu kwa ajili ya kutunga Katiba.
Akiwasilisha madhumuni na sababu za muswada huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alisema umependekeza kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya nchi ya mwaka 2011 na unakusudia kuanzishwa kuweka masharti ya uanzishaji wa tume pamoja na sekretari kwa madhumuni ya kuendesha na kusimamia mchakato wa mabadiliko ya hayo.
Mchakato wa mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine, utaangalia chimbuko na uhusiano wa katiba iliyopo kwa kuzingatia uhuru wa wananchi na mfumo wa siasa.
Alisema pindi muswada huo utakapopitishwa na kuwa sheria, utakuwa na utaratibu wa kisheria utakaomwezesha Rais kuunda tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba na kuunda Bunge la Katiba kwa madhumuni ya kutunga Katiba mpya.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma amesema muswada wa marekebisho ya Katiba ya Muungano una upungufu mwingi ukiwemo kutoshirikishwa kwa Serikali ya Zanzibar ambayo alisema haikushirikishwa kikamilifu ili kutoa maoni yake na wala haukupelekwa katika Baraza la Wawakilishi kupata maoni ya Baraza, hivyo haukustahiki kupelekwa Bungeni kujadiliwa kwani umekosa ridhaa za pande mbili.
“Muswada huo ni vyema kurudi serikalini na ukafanyiwe marekebisho na badala yake upelekwe katika Baraza la Wawakilshi ili upate ridhaa ya nchi mbili zilizoungana,” alisema Hamza.
Endelea kusoma habari hii.........................
Friday, April 8, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment