Mubarak atiwa kizuizini kwa siku 15
Via BBC
Mwendesha mashtaka wa Misri ameamuru kutiwa kizuizini kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Hosni Mubarak, kabla ya kufanywa uchunguzi juu ya madai ya rushwa na unyanyasaji.
Bw Mubarak, mwenye umri wa miaka 82, yuko hospitalini baada ya kuripotiwa kuwa na matatizo ya moyo. Televisheni ya taifa ilisema amri ya kutiwa kizuizini itatekelezwa kwa muda wa siku 15.
Watoto wake wa kiume Alaa na Gamal nao pia wametiwa kizuizini wakihusishwa na madai ya kuhusika na rushwa na ghasia.
Bw Mubarak aliachia madaraka mwezi Februari baada ya maandamano kufanyika ya kupinga utawala wake.
Tangu wakati huo, maelfu ya waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano kila Ijumaa kwenye eneo la wazi la Tahrir mjini Cairo, wakitaka ashtakiwe.
Takriban watu 360 wanadhaniwa kuuawa wakati wa maandamano, kufuatia polisi kufyatua risasi kwa ajili ya kuwatawanya waandamanaji.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema idadi hiyo ni kubwa zaidi.
Pia kuna madai yaliyoenea kuhusu rushwa na utumiaji mbaya wa madaraka katika kipindi cha miaka 30 ya uongozi wake.
Wednesday, April 13, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment