Pangua pangua CCM yawasomba vigogo
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), imetangaza safu mpya ya uongozi wa juu wa chama hicho watakaoongoza Sekretarieti yake na Kamati Kuu (CC) huku vigogo wengi wakianguka na kisha kutoa siku 90 kwa watuhumiwa wa ufisadi kujiondoa wenyewe NEC ya chama hicho vinginevyo watawajibishwa.
Katika uteuzi huo, Wilson Mkama amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu, nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Yusuf Makamba. Mkama atasaidiwa na Naibu Makatibu Wakuu (Bara na Visiwani), John Chiligati na Vuai Ali Vuai. Katibu mpya wa Itikadi na Uenezi ni Nape Nnauye, huku, Mwigulu Mchemba akichaguliwa kuongoza Idara ya Fedha na Uchumi. Mkuu wa Oganaizesheni ni Asha Abdallah Juma na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Januari Makamba.
Waliochaguliwa kuunda Kamati Kuu ni Abdulrahman Kinana, Zakia Meghji, Dk Abdallah Kigoda, Pindi Chana, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constancia Buhiye, William Lukuvi na Steven Wassira.
Kwa upande wa Zanzibar, waliochaguliwa ni Dk Hussein Mwinyi, Dk Maua Daftari, Samia Suluhu Hassan, Shamsi Vuai Nahodha, Omar Yusuf Mzee, Profesa Mbarawa Mnyaa na Muhammed Seif Khatib.
Mwenyekiti wa CCM kwa madaraka ya kikatiba aliwateua wajumbe 10 kuingia NEC ambao ni Anna Abdallah, Peter Kisumo, Mwingulu Mchemba, Wilson Mkama, Januari Makamba, Juma Shamhuna, Dk Emmanuel Nchimbi na Haji Omar Kheri.
Miongoni mwa majina yaliyokuwa yamependekezwa ni Kingunge Ngombale-Mwiru, Beno Malisa, Mussa Azzan Zungu, Shamsa Mwangunga, Profesa Athman Kapuya, William Kusila na Anthony Diallo.
Akizungumzia kile ambacho kimekuwa kikitajwa kama kujivua gamba kwa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alisema mkutano huo umefikia uamuzi kwamba wote wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi wajiondoa wenyewe kwenye uongozi chama na iwapo watakaidi watawajibishwa.
Rais Kikwete alisema hatua zilizochukuliwa kujiuzulu kwa Sekretarieti na Kamati Kuu, ni za mwanzo na hakuna tena sababu ya chama kusubiri ushahidi kama ilivyokuwa mwanzo.
Akifunga kikao cha NEC-CCM, jana usiku mjini hapa, Rais Kikwete alisema hivi sasa hatua zitakuwa zinachukuliwa haraka dhidi ya watuhumiwa pindi hali inapoanza kuchafuka kwenye jamii: “Tumeanza kuchukua hatua na huu ni mwendelezo, tunaowatambua tuwabane kwa kuwataka wajiuzulu na pale wanapokataa tusichelee kuwawajibisha.”
Alisema wamekubaliana kuzingatia maadili na kwamba kumekuwapo na utovu wa maadili ambavyo ni miongoni mwa mambo yaliyopoteza haiba ya chama.
Kuhusu daftari la wanachama, Rais Kikwete aliwataka watendaji wa chama hicho kuliandaa vizuri na uchaguzi utapokaribia lifungwe kwa sababu lilitumika vibaya katika uchaguzi uliopita na limewaongezea watu walionuna.
Alisema wamekubaliana kuunda baraza la ushauri la wazee, ambalo litakuwa na ajenda zake badala ya sasa kuitwa na kufuata ajenda za NEC au CC: “Tumekubaliana ngazi yetu muhimu ni shina na tawi na wajumbe wa NEC watakuwa wanachaguliwa wilayani ambako ndiko watu waliko,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Turudi kwenye masharti na matakwa ya Katiba yetu, tumeteleza mahali wagombea wananunua kadi wanakwenda wanawagawia watu ambao wako tayari kuwapigia kura wao, tumekuwa na mkusanyiko wa watu wasio waumini.”
Alisema kazi iliyopo mbele yao hivi sasa ni kujenga chama na kwamba wamekubaliana kujibu matusi ya wapinzani badala ya kutuma ujumbe mfupi wa simu kwake.
Pia alisema wamekubaliana kuzunguka kueleza ukweli wa Muswada wa Mabadiliko ya Katiba, ili kuondoa upotoshaji unaofanywa na wapinzani.
Awali, aliyekuwa katibu mkuu Makamba akiaga alisema Sekretarieti aliyokuwa akiiongoza imejiuzulu kwa maslahi ya chama huku akibainisha kwamba alikataa kujiuzulu peke yake.
Alisema anakwenda kutayarisha makao na walioingia watambue kuna siku watamfuata, huku akitoa mifano ya Yesu alivyokuwa akiaga wanafunzi wake: “Hata nyinyi mtastaafu mtatukuta tumewatayarishia makao,” alisema.
Alimtaka Rais Kikwete kutomsahau na kwamba pale atakapoona anafaa kama ni kwenda kujibu matusi yupo tayari kufanya hivyo.
Taarifa zilizopatikana jana zilisema kwamba Rais Kikwete leo atazungumza na watumishi wote wa CCM waliopo Makao Makuu ambao morali ya watumishi hao ilikuwa umekufa.
Source: Mwananchi
Monday, April 11, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment