Monday, January 16, 2012

Akina Professor Jay, Sugu na uongozi wa taifa

Best Blogger Tips
Ahmed Rajab
JUZI nilikuwa nikiangalia mahojiano katika stesheni moja ya televisheni ya lugha ya Kifaransa. Aliyekuwa akihojiwa alikuwa Youssou N’Dour, mwimbaji maarufu wa Senegal aliyetangaza kwenye mahojiano hayo kuwa ataugombea urais wa nchi yake katika uchaguzi utaofanywa Februari 26, mwaka huu.

Katika mahojiano hayo mwimbaji huyo, mwenye umri wa miaka 52, alitamka haya: “Mimi sikusoma lakini nimezingatia yaliyofanywa na waliosoma tangu uhuru nikaingiwa na mori wa kutumia haki yangu na kutoa mchango wangu kwa wananchi wa kawaida. Nimetafakari nikaona nina wajibu wa kuingia katika kinyanganyiro hiki.”

Ingawa mwaka jana Chuo Kikuu cha Yale kilichoko Marekani kilimtunukia shahada ya heshima ya udaktari wa muziki  N’Dour,  kama alivyosema mwenyewe, si mtu aliyesoma. Sana sana amesoma katika shule ya msingi na hakuingia shule ya sekondari.

Alipotimiza umri wa miaka 12 tayari alikuwa akipanda kwenye majukwaa kuwatumbuiza mashabiki wa muziki.  Kabla ya kuwakusanya wanamuziki kadhaa walio na ustadi katika fani hiyo na kuanzisha kundi lake la Étoile de Dakar (Nyota ya Dakar), N’Dour alikuwa mmoja wa wanamuziki wa kundi la Orchestra Baobab na kabla ya hapo Star Band.

Ingawa hakusoma hivyo Youssou N’Dour alitumia kipaji chake kisicho kifani kwa kusoma katika shule ya maisha na kuyafanya maisha yake yawe kivutio. Tangu aanze kujitafutia riziki kwa kuimba ameutumia muziki kuwa ngazi ya kujijenga, sio yeye tu bali pia Waafrika wenzake na taifa lake. Leo hii amefanikiwa kuitangaza Senegal katika ulimwengu wa burudani na kuipatia sifa duniani. 

Ameshirikiana na waimbaji walio wanaharakati maarufu kama Bob Geldof na Bono kusaidia katika kampeni za kupambana na maafa, tangu ya ukame, njaa, magonjwa, umasikini na madeni ya nchi za Magharibi yanayobebwa na nchi zetu.

Pamoja na yote hayo, N’Dour ameanzisha miradi binafsi huko kwao Senegal ya studio ya kisasa ya muziki, steshini ya redio, nyingine ya televisheni na gazeti, akiwaajiri jumla ya vijana wasiopungua 4,000.

Wengi wanajiuliza ni wanamuziki wangapi maarufu barani Afrika  walioweza kufanya alau nusu ya aliyofanya N’Dour. Jibu hakuna.

Kwa muda wa takriban robo karne tangu akiasisi kikundi chake hakuna mwanamuziki wake hata mmoja aliyemuacha mkono. Hili pia ni la kupigiwa mfano. Ni jambo linalodhihirisha  uadilifu wake N’Dour kwa wale anaowaongoza, iwe kimuziki au kibiashara.

Kujitokeza kwake kuwania urais kumeshaanza kuwatia kiwewe wanasiasa wakongwe tangu Rais Abdoulaye Wade, mwenye umri wa miaka 86, hadi baadhi ya wapinzani wake.

Hofu ya Wade, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kidemokrasia cha Senegal, sio kwamba N’Dour ataweza kushinda moja kwa moja katika duru ya mwanzo, la  hasha. Kinachomtia wahka ni umaarufu wa N’Dour unaoweza kusababisha uchaguzi kuingia duru ya pili. Hiyo ni duru ambayo Wade anaihofia. Anahofia kwamba endapo uchaguzi utaingia duru hiyo na wapinzani wake wakashikana kumuunga mkono mgombea mmoja basi hatoweza kufua dafu.

Nilikutana na Wade kwa mara ya kwanza mwishoni mwishoni mwa mwaka 1999, nilipokuwa nikihariri Jarida la Africa Analysis na miezi kadhaa kabla hajachaguliwa kuwa Rais. Aliletwa ofisini mwangu na Balozi Gaby Sar, aliyekuwa Balozi wa Senegal mjini  London, jambo lililonifanya nimpe heko balozi huyo kwa ustaarabu wake wa kisiasa na Serikali yake kwa uvumilivu wake. Ni nadra kumuona balozi wa kiafrika akimhudumia kiongozi wa upinzani, akimpangia miadi na akifuatana naye na serikali yake isikereke kwa hayo. 

Wakati nilipoonana naye, Wade alikuwa amekwishagombea urais mara nne na mara zote akibwagwa na Rais Abdou Diouf. Nilipokutana naye nilimuonea huruma na sikudhania katu kwamba miezi michache tu baadaye, atatimiza ndoto yake na hatimaye kumshinda Diouf. Nilimuona kuwa ni mtu myenyekevu na haikunipitia kwamba ana ujeuri anaouonyesha sasa.

Wade ni mtu aliyesoma; tena amesoma sana. Kwa hakika ni msomi kwani kuna tofauti kati ya mtu aliyesoma na msomi. Unaweza ukasoma masomo ya juu na kupata mashahada ya juu na usiwe msomi. Na unaweza kuwa msomi bila ya kupata cheti hata kimoja cha masomo.

Wade ana shahada mbili za udaktari — wa sheria na wa uchumi.  Alikuwa akifundisha sheria Ufaransa na nchini Senegal aliwahi kuwa mkuu wa kitivo cha sheria na uchumi katika Chuo Kikuu cha Dakar.
Alipokuwa kiongozi wa upinzani, Wade alikuwa akiukosoa sana  utawala wa chama cha Kisoshalisti wakati wa muasisi wake, Léopold Senghor na baadaye wakati wa uongozi wa Diouf. Nadhani Senghor alimng’amua mapema Wade kwani akimwita ‘sungura’.

Siku hizo Wade alikuwa akipigania sana utaratibu wa rais kutawala mihula miwili tu. Lakini katika kuhakikisha anakuwa tofauti na wengine akataka kipindi kiwe cha miaka saba badala ya mitano kama alivyofanya Paul Kagame, nchini Rwanda. Wade aliyeahidi kuiheshimu Katiba sasa ameivunja ahadi yake na ameibadili Katiba.

Alipoulizwa na mmoja wa wananchi wenzake mbona amekwenda kinyume cha ahadi aliyoitoa alipoingia madarakani alijibu: “Kweli niliyasema hayo wakati ule, lakini sasa nimebadili nia; tatizo likowapi ?”
Tatizo kubwa linalomkabili Wade hivi sasa ni zile shutuma zinazomuandama za utumiaji fedha za umma kwa ubadhirifu, ufisadi, kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, ukiukwaji wa haki nyingine za kibinadamu na upendeleo wa kuwapa kazi jamaa zake. Mwanawe wa kiume, Karim amemteua kuwa waziri na binti yake, Sindjely amempa kazi ya kuwa msaidizi muhtasi wa Rais. 

Wade anawakebehi wanaosema kuwa yeye ni mzee na huenda asimalize kipindi chake kwa kuhoji kuwa ikiwa babu zake na baba yake waliishi na kufika umri wa miaka 100 ushei, kwa nini naye asifike umri huo.
Hivi sasa gumzo kubwa nchini Senegal ni juu ya uzee wake. Papo hapo kujitokeza kwa Youssou N’Dour kumeanzisha mjadala mwingine kwamba mtu asiye na elimu ya juu hawezi kuwa rais. Suala hili limeanzisha mtindo mpya barani Afrika. Nakumbuka nchini Tanzania, Augustine Mrema alilazimika haraka haraka ajiandikishe chuo kikuu kimoja cha Marekani apate shahada kwa njia ya mtandao ili aweze kugombea urais.

Cha kushangaza ni kuwa raia wa kawaida anaweza kugombea udiwani, ubunge au  hata kuwa waziri bila ya kujali kama ana shahada au elimu ya juu lakini ikija katika kugombea urais anaangushwa. Raia huyo anageuzwa wa daraja la pili na haki yake kukandamizwa.

Hata hivyo, tukitafakari hebu tujiulize hao wanaojiona kuwa ni wasomi au waliosoma pamoja na mashahada waliyonayo wameweza kweli kutimiza matarajio ya raia wa kawaida? Historia inatuonyesha kuwa wengi wao ndio walioharibu zaidi. Wamekosa muelekeo, uadilifu na nia safi ya kulitumikia taifa.

Siku hizi waliosoma wanaingia katika siasa ili wapate madaraka waweze kupora mali ya taifa. Angalia tu mishahara na marupurupu wanayojipa wabunge; yalinganishe hayo na mishahara duni ya watumishi wa kawaida serikalini.  Ndio maana ukaona kwamba leo madaktari, wanahiyari wawe wabunge na mawaziri wakati kuna uhaba wa  madaktari hospitalini. Wahadhiri nao vivyo hivyo wakati kuna uhaba  wa waalimu.
Linalochoma zaidi ni kuwaona wanasayansi wa vipawa vya juu wakizitupilia mbali taaluma zao wakikimbilia kwenye uwanja mchafu wa tope za kisiasa kwani siasa nchini mwetu zimegeuzwa kuwa hivyo. Ndio maana zinanuka.

Lakini si lazima ziwe hivyo. Na ndio maana wanachomoza wanasiasa wapya mithili ya Youssou N’Dour wanaoingia katika siasa kichwa upande kwa lengo la kuzisafisha siasa chafu. Wanaingia katika siasa wakiamini kwamba uongozi ni uwezo na busara na sio lazima kusoma kwingi.

Bila ya shaka hakuna anayetaka kiongozi mbumbumbu. Anayetakiwa ni kiongozi atayeweza kuongoza nchi kwa hekima na uadilifu. Anayetakiwa ni kiongozi imara atayeweza kuamua na kutekeleza uamuzi wake bila ya kuyumbishwa na majambazi wa kisiasa.

Ikiwa waimbaji wa Bongo Flava kama akina Professor Jay (Joseph Haule) na Sugu (Joseph Mbilinyi-Mbunge wa Mbeya Mjini) au hata Bob Junior na Ali Kiba watataka uongozi na wakaonyesha watakuwa na sera safi za kuongoza nchi kwa maadili ya utawala bora kwa nini wananchi wasiwachague? 
Tayari katika uchaguzi uliopita wapiga kura wa Mbeya (Mjini) walimchagua Sugu wa CHADEMA awe mbunge wao akimshinda mwalimu wake wa zamani wa shule, Benson Mpesya aliyekuwa mgombea ubunge mzito kutoka CCM.

Tupime maendeleo yaliyoletwa na vongozi wetu katika sekta za afya, elimu na kilimo. Tuangalie jitihada zao za kukabili njaa na kuondosha umasikini na tusiangalie tu barabara wanazozijenga. Siku hizi imegeuka  nyimbo watu kusema waziri au rais fulani amefanya mengi. ‘Angalia barabara kutoka mahala fulani hadi fulani.’

Sahibu yangu mmoja kutoka Liberia aliwahi kuniambia: “Afrika tunayapima zaidi maendeleo ya mwanasiasa kwa kuangalia kilomita ya barabara aliyojenga, badala ya sekta nyingine.”  Na mara nyingi barabara hizo huzijenga kwao.

Sitoshangaa ikiwa kutapita mizengwe nchini Senegal ya kumzuia Youssou N’Dour asiwe mgombea wa urais. Tayari wanaojiona kuwa ni wasomi wameshaanza kumbeza kuwa hawezi kuzungumza Kifaransa kwa ufasaha, kana kwamba Kifaransa chake ndicho kitakachofanikisha kupatikana elimu bora, matibabu bora na kupambana na umasikini. Lakini wasomi wetu wamezoea;wanaposhindwa kutoa hoja za maana hata kasumba kama hizi huzitumia.
Chanzo: Raia Mwema

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits