Monday, January 23, 2012

Mwandishi wa habari wa Mwananchi afariki dunia

Best Blogger Tips
Beatus Kagashe
 MWANDISHI wa habari wa Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL), Beatus Kagashe (31), amefariki dunia juzi usiku.Kifo cha mwandishi huyo aliyekuwa akiandikia gazeti la The Citizen, kilitokea katika Hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa saratani ya damu baada ya kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Aga Khan kwa miezi miwili.

Msemaji wa familia ya marehemu Gasper Mikimba alisema, Kagashe alifariki mnamo saa 2:45 usiku na kwamba familia iko katika mipango ya mazishi ambayo yatafanyika Bukoba mkoani Kagera. Alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda huko Jumanne na mazishi kufanyika Jumatano.

“Bado tunaendelea na mipango ya mazishi... lakini nadhani tutasafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani Bukoba siku ya Jumanne kwa ajili ya mazishi,” alisema Mikimba.

Alisema kifo cha Kagashe kimeacha mshtuko mkubwa katika familia,jamii pamoja na taifa kwa ujumla hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa bado kijana aliyetarajiwa kulijenga taifa lake.

Marehemu Kagashe alizaliwa Februari 23, 1981 mkoani Kagera na alipata elimu ya msingi katika Shule ya Bilele iliyoko Bukoba Mjini kati ya mwaka 1990 na 1996, alijiunga na Shule ya Sekondari Ihungo kuanzia mwaka 1997 mpaka 2000 kabla ya kujiunga na Shule Sekondari Mpwapwa kwa masomo ya kidato cha tano na sita.

Mwaka 2004, alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusoma kozi ya uandishi wa habari (Bachelor ofn Arts Journalism) katika Taasisi ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (IJMC) alipohitimu mwaka 2007. Alijiunga na masomo ya shahada ya uzamili katika masuala ya utawala (Masters in Public Administration) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2010 na kuhitimu Novemba mwaka jana.

Mhariri Mtendaji wa Gazeti la The Citizen, Bakari Machumu alisema amepokea kifo cha marehemu Kagashe kwa masikitiko makubwa. Alimwelezea kama kijana aliyekuwa mpenda watu na mwenye kusimamia alichokiamini.

“Tulidhani alikuwa anaendelea vizuri na matibabu... nimepata mshtuko kusikia kwamba Kagashe ameaga dunia. Nilikutana naye hospitali wiki moja iliyopita alionekana kuwa na nguvu ya kupambana na ugonjwa wake,” alisema Machumu.

Alisema idara yake imepoteza hazina ambayo Mwananchi Communications Limited ilikuwa imewekeza kwa manufaa ya kampuni pamoja na gazeti.

Alisema marehemu Kagashe alikuwa ni zao la utaratibu wa kusaka vipaji kutoka vyuo vya elimu ya juu, programu iliyoanzishwa na Kampuni ya Mwananchi mwaka 2007 akiwa miongoni mwa vijana watano wa kwanza wa kundi la kwanza la programu hiyo.

“Kagashe alitokana na mpango wa kusaka vipaji katika vyuo vya elimu ya juu...mamia ya wahitimu wa vyuo vikuu nakumbuka walijitokeza lakini Beatus Kagashe alikuwa miongoni mwa wanafunzi watano bora, hivyo kujiunga na kozi maalumu huko Nairobi,Kenya,” alisema Machumu.

Kagashe aliajiriwa aliajiriwa na Mwananchi Communications Limited, kampuni inayochapisha magazeti ya The Citizen, Mwananchi na Mwanaspoti mnamo mwaka 2008. Ameacha mjane, Doroster Kagashe na mtoto Emmanuel Mujuni ambaye ana umri wa mwaka mmoja.

Chadema wamlilia
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa majonzi na masikitiko makubwa, taarifa za kifo cha Kagashe.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Tumaini Makene imesema: “Kwa wale waliokuwa wakimfahamu marehemu Kagashe, watakubali kuwa alikuwa mmoja wa waandishi makini, waliokuwa wakiamini jamii ya Watanzania inaweza kufanya mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.”

Alisema kwa kutumia vema taaluma yake, akiongozwa na maadili ya tasnia ya habari, alishirikiana na Watanzania wenzake katika kuelimisha, kuhabarisha, kuhamasisha na kuburudisha umma, katika masuala mbalimbali kupitia kalamu yake.

“Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wafanyakazi wenzake na kuwaombea kwa Mungu awape moyo wa subira katika wakati huu mgumu wa majonzi kwa kuondokewa na mpendwa wao,” alisema Makene.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits