BAADHI ya wagonjwa na madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH), wamesimulia adha wanazopata kutokana na kufukuzwa kwa madaktari
wanafunzi waliokuwa wamegoma na wameiomba Serikali ifanye kila
linalowesekana kunusuru hali hiyo.
Wakizungumza na gazeti hili
kwa nyakati tofauti jana, walisema mgomo huo umefanya hali katika
hospitali hiyo kuwa mbaya, kiasi cha baadhi ya wagonjwa kupoteza maisha
kwa kukosa huduma.
Mmoja wa wagonjwa hao Godliver Alfonsi
aliyetokea mkoani Kigoma alisema ana wiki moja tangu afike hospitalini
hapo lakini hajaweza kuonana na daktari.
"Tangu nije leo (jana)
tu ndio nawaona madaktari wakipita, lakini kwangu hawakupita kwa kuwa
muda ni mdogo na wameniahidi kuwa watakuja kwangu kesho (leo)," alisema.
Mama
wa mtoto Fatma Iddi katika wodi ya jengo la watoto, Hidaya Idrisa
alisema madaktari hawaonekani wodini hapo kama ilivyokuwa awali.
Alisema
kabla ya mgomo madaktari walikuwa wakikaa katika moja ya vyumba vya
wodi hiyo, hivyo ilikuwa rahisi kuwapata kunapotokea tatizo.
“Madaktari
hapa walikuwa hawaondoki kila wakati wapo na wakati wowote ukiwa na
shida unapata msaada lakini hivi sasa chumba chao kitupu, hawapo”
alisema Hidaya.
Hali katika wodi ya Kibasila pia ni mbaya na
muuguzi wa zamu katika moja ya wodi za jengo hilo alisema; "Inawachukua
muda wagonjwa kuonana na daktari kutokana na uchache wa madaktari."
“Mfano
daktari ambaye yupo sasa aliingia kazini jana (juzi) mpaka sasa
ninavyoongea hajaondoka maana yuko peke yake,” alisema muuguzi huyo.
Mgonjwa
mwingine hospitalini hapo ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema:
“Tangu asubuhi sijaonana na daktari sasa ni mchana (saa 12.30) na sina
tumaini la kupata huduma”.
“Kama ningekuwa mahututi pengine hata wewe mwandishi usingenikuta, tungekuwa tunaongea mengine hapa,” alisema mgonjwa huyo.
Mmoja
kati ya wanafunzi (jina limehifadhiwa), ambaye yupo katika mafunzo kwa
vitendo tatu mwezi Desemba mwaka jana hosipitalini hapo, anasema hali si
nzuri na kwamba ikiendelea hivyo huenda idadi ya vifo ikaongezeka.
“Idadi
ya vifo vya sasa huwezi kuvihusisha na mgomo moja kwa moja lakini sina
shaka kabisa kuwa vipo ambavyo vinachangiwa na hali hii,”alisema daktari
huyo mwanafunzi.
Alisema kwa sasa madaktari bingwa hawana
wasaidizi hali ambayo inawafanya wafanye kazi muda mrefu na kushindwa
kuwafikia baadhi ya wagonjwa.
“Madaktari wanachoka, hata sisi
wachache ambao tunasaidiana nao tunakuwa katika wakati mgumu” alisema na
kuongeza kuwa hali hiyo inawafanya wawazungukie wagonjwa hadi saa nane
mchana badala ya muda wa kawaida wa saa mbili asubuhi.
Madaktari
Katibu
wa Chama cha Madakitari Tanzania (MAT) Dk. Rodrick Kabangila alisema
tabia ya Serikali kuingiza siasa katika taaluma inaathiri huduma kwa
umma.
Alisema kila jambo hivi sasa linachukuliwa kisiasa kwa
kupiga porojo badala ya utekelezaji na kwamba sasa siasa zimeingia
katika taaluma ya udaktari na uuguzi.
Kabangila alisema serikali
inatumia mamilioni ya shilingi kuwatibu viongozi nje ya nchi lakini
inashindwa kutumia pesa hizo kuwalipa madaktari stahili zao na kununua
vifaa tiba vya kisasa.
Alisema Tanzania inaongoza kwa kupeleka
wagonjwa nchini India, sifa ambayo alisema si nzuri na kwamba hatari
zaidi viongozi serikalini wanajivunia hali hiyo.
Katibu huyo
alisema wamekaa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
viongozi wengine wa serikali na wamewataadharisha juu ya mwenendo huo.
Kabangila
alisema chama cha madaktari kitafanya mkutano wake mkuu Jumamosi ijayo,
ambao pamoja na mambo mengine utajadili masuala ambayo yamejitokeza
katika mgomo huo na kufikiria hatua zaidi za kuchukua.
Alisema
wanaishangaa wizara ambayo baada ya kulipa posho za madaktari wanafunzi
wamewaita wahusika wizarani na kwamba hatua hiyo ni kukwepa hoja ya
msingi.
Kauli ya Serikali
Madaktari hao 229
walianza mgomo Jumanne wiki iliyopira, wakiishinikiza Serikali iwalipe
posho zao za Desemba mwaka jana ambazo ni zaidi ya Sh179 milioni.
Kwa
mujibu wa madaktari hao, uamuzi huo ulifikiwa baada ya wizara kushindwa
kuwalipa posho zao kwa wakati hali iliyowafanya waishi kwa tabu.
Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, alikiri hali hiyo na
kusema kuwa imesababishwa na ukata ulioikumba wizara hivyo kushindwa
kuwalipa madaktari hao kwa wakati.
Dk Mponda alisema kwa kawaida
posho hizo hulipwa tarehe 22 ya kila mwezi na kwamba kiasi cha fedha
ambacho hulipwa ni Sh900 milioni kwa madaktari wanafunzi nchi nzima.
Pamoja
na maelezo hayo, serikali iliwapa barua za kujieleza madaktari wote
waliokuwa wamegoma licha ya kwamba baadhi yao walishaanza kurejea kazini
baada ya kuwa wamelipwa posho hizo.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, January 8, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment