SIMANZI nyingine imelikumba Bunge la Tanzania, kufuatia kifo cha Mbunge
wa Arumeru Mashariki (CCM), Jeremiah Solomon Sumari (60),aliyefariki
dunia usiku wa kuamkia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili
alikokuwa amelazwa kwa muda mrefu akipatiwa matibabu.
Kifo cha
Sumari kimetokea siku moja tu, tangu kufanyika kwa mazishi ya Mbunge wa
Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema aliyefariki dunia kwa ajali ya gari,
Jumamosi iliyopita katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.
Sumari alianza kuugua kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, hali ambayo ilimfanya aende kampeni katika mazingira magumu.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtoto wa kwanza wa
marehemu, Sioi Sumari alisema baba yake alipatwa na mauti katika
hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alipokuwa amelazwa.
“Baba amefariki saa 8.30 usiku katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu,” alisema Sioi.
Alifafanua kuwa, marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumatatu ijayo kijijini kwake katika jimbo la Arumeru Mashariki.
Mtoto huyo wa marehemu alisema baba yake utaagwa kesho (Jumamosi ) jijini Dar es Salaam, kabla ya kusafirishwa kwenda Arusha.
Ofisi
ya Bunge Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema ofisi ya Bunge
imepokea kwa masikitiko msiba huo kwani umetokea muda mfupi tangu
waliporejea kutoka kwenye maziko ya Mtema.Hata hivyo, alisema kutokana
na hali hiyo shughuli za Bunge zitaendelea kama zilivyopangwa na kwamba,
zitasimamishwa siku ya kuaga mwili wa marehemu.
“Leo (jana) na
kesho tutaendelea na shughuli za bunge kama kawaida, lakini siku ya
kuaga tutasitisha shughuli ili kutoa fursa kwa wabunge kushiriki kwenye
mazishi ya marehemu Sumari,” alisema Dk Kashililah. Alisema kwa sasa
wanafanya taratibu za mazishi ya marehemu kwa kushirikiana na familia
yake.
Alifafanua kwamba kutokana na hali hiyo, bunge limepata
pigo kubwa baada ya kuondokewa na wabunge wawili katika kipindi kimoja,
jambo ambalo limesababisha wabunge kushikwa na butwaa.Naibu Spika wa
Bunge, Job Ndugai alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge itakutana leo
kujadili namna ya kuratibu mazishi ya mbunge huyo.
Alisema kuna uwezekano mbunge huyo akaagwa katika ukumbi wa Karimjee, kama ilivyofanyika kwa mbunge wa Chadema Regia Mtema.
“Tunasikitika sana kwa kuwapoteza wabunge wawili ndani ya muda mfupi,” alisema Ndugai.
Kikwete amlilia
Kwa upande wake, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge, Anne Makinda kutokana na kifo cha Sumari.
Taarifa
ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilimnukuu Rais Kikwete ikisema;
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana kutokana na taarifa
za kifo cha Mheshimiwa Jeremia Solomon Sumari….”
“Alikuwa kiongozi
aliyewatumikia vema wananchi wa Jimbo lake la Uchaguzi la Arumeru
Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhifa wake wa Waziri kwa umahiri
na uhodari mkubwa.”
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Kikwete
alisema kutokana na kifo cha Sumari, wananchi wa Arumeru Mashariki
wamepoteza kiongozi wa kutegemewa. “Kwa moyo dhati, natuma salamu za
rambirambi na pole kwa familia ya marehemu Jeremia Sumari kwa kumpoteza
kiongozi na mhimili madhubuti wa familia,” taarifa hiyo ilimnukuu Rais
Kikwete. Alifafanua akisema; “Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja
nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa na namuomba Mwenyezi Mungu,
mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya marehemu Jeremia Solomon Sumari
mahali pema peponi, Amina.”
Lowassa amlilia
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa alisema taifa limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na Sumari.
“Alikuwa
mchapakazi sana.., hii imesababisha kuteuliwa kuwa Naibu Waziri katika
serikali ya awamu ya nne, kutokana na umahiri wake,” alisema Lowassa.
Lowassa
aliongeza kwamba, kutokana na hali hiyo, wananchi wa Arumeru Mashariki
wamekosa mwakilishi wa kutetea maslahi yao bungeni.
Historia yake
Sumari alizaliwa Machi 2 mwaka 1943, katika kijiji cha Akeri wilayani Arumeru mkoani arusha.
Alipata
elimu yake ya msingi katika shule ya Meru Magharibi kati ya mwaka 1950
na 1957. Kati ya mwaka 1958- 1964 alisoma katika shule ya sekondari ya
Old Moshi, mkoani Kilimanjaro na baadaye aliendelea na elimu ya juu
nchini Uingereza.
Taarifa zinaonyesha kuwa, Sumari alipata elimu
ya masoko kwa ngazi ya cheti ACCA, CIS, (Certificatein Marketing and
Lincesed Broker lr), nchini Uingereza na baadaye kupata CPA nchini.
Kwa upande wa utumishi wake, mwaka 1996 mpaka 2004 alikuwa Mkurugenzi wa Bodi ya Boko la Disa Dar es Salaam (DSE).
Kisiasa , kuanzia mwaka 2005 mpaka mauti yalipomkuta alikuwa Mbunge wa jimbo hilo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya CCM.
Januari
4 mwaka 2006, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo
ya Vijana na mwaka 2008 mpaka 2010 alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa
Fedha na Uchumi.
Chanzo: Mwananchi
Thursday, January 19, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment