KAMATI ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari wanaoendelea na mgomo nchi nzima
imesema hawajafunga milango ya mazungumzo na ujumbe wowote kutoka kwa
Waziri Mkuu.
Wameshangaa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kutowafuata walipo madaktari
wote kama alivyofanya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mwaka 2005
na badala yake juzi kuzungumza na waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Stephen Ulimboka alisema hayo jana
katika kikao cha madaktari hao walichokihamishia katika ukumbi wa
Starlight baada ya ukumbi wa Don Bosco kushindwa kuchukua madaktari wote
waliojitokeza jana.
Juzi Pinda, alisema haoni sababu ya kukwama kwa mazungumzo kati ya
Serikali na madaktari hao na kwamba yupo tayari kukutana na wawakilishi
wao na kutuma salamu popote walipo na wakisikia ujumbe wake, wafike
wamwone kabla hajaenda bungeni Dodoma, Jumamosi.
Awali walielezwa kuwa Jumanne, Pinda angefika kuonana nao, lakini
iliishia kuonana na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo na
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, katika kikao
walichokaa hadi saa tatu usiku bila mwafaka.
Kutokana na hatua hiyo, walimtaka Pinda afike na kuonana nao, kwani
wao wapo tayari kumsikiliza pamoja na ujumbe wake, ili kufikia muafaka
wa malalamiko yao na kuendelea kutoa huduma.
Wakati madaktari hao wakiendelea na kikao chao ambacho jana
kilifurika zaidi, huduma katika hospitali za Serikali zimezidi kudorora
na wagonjwa kurudishwa nyumbani huku wakitakiwa kurudi watakaposikia
tangazo kwenye vyombo vya habari.
Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Kitengo cha Watoto
hali ilizidi kuwa mbaya baada ya watoto wenye ugonjwa wa upungufu wa
damu - selimundu, kutakiwa kurejea nyumbani na kurudi Alhamisi ijayo.
Pia watoto wenye matatizo ya moyo walitakiwa kurudi wiki ijayo jambo
ambalo ni hatari, kutokana na kuwa watoto hao walitakiwa kusafiri wiki
ijayo, kwenda India kwa matibabu.
Muhonewa Mfaume, mama wa Hamida mwenye umri wa miaka miwili na nusu,
mwenye matatizo ya moyo na mkazi wa Kigoma aliyefikia Mwananyamala kwa
ajili ya matibabu ya mtoto wake, alisema aliishakamilisha tararibu zote
za Wizara ya Afya na alichobakiza ni kuonana na daktari ili ajaziwe fomu
itakayomwezesha kwenda kuchukua viza kwa ajili ya kwenda India.
Alisema cha kushangaza ni kuwa jana alifika kumwona daktari, lakini
akaambiwa arudi wiki ijayo, kutokana na maelezo kwamba madaktari wa
kumwandikia hawapo.
“Acha nirudi nyumbani nikaendelee kumwomba Mungu tufike hiyo Ijumaa
na Mungu ajalie wawe wamemaliza mgomo wao, kwani huyu mtoto kufika umri
huu ni neema ya Mungu, hawezi kukakaa wala kusimama, hata kuongea
anaongea kwa shida akizungumza sana anashindwa kupumua,“ alilalamika
mama huyo.
Katika kitengo hicho, mmoja wa madaktari wanafunzi wa mwaka wa nne,
alisema hali ni mbaya, kwani huduma zote za wagonjwa wa nje
zimesitishwa, labda kwa wenye hali mbaya sana na waliolazwa.
Alisema wanaofanya kazi sasa ni wao, walio katika mafunzo na
wahadhiri wanaofundisha Chuo Kikuu cha Muhimbili, ambao ni wataalamu wa
watoto, lakini hutoa huduma mara chache sana.
Katika Kitengo cha Wagonjwa wa Nje, ilionekana misururu mirefu ya
wagonjwa wakisubiri madaktari, huku ikionekana kuwapo madaktari katika
vyumba lakini wakidaiwa kuwa wanafunzi.
“Mimi ni daktari wa Kitengo hiki cha Wagonjwa wa Nje na wote tupo
kwenye mgomo, ninachoshangaa hao wanaotoa huduma wametoka wapi, kwani
siwatambui, hebu jaribuni kuwauliza,” alisema mmoja wa madaktari wa
hospitali hiyo aliyekataa kutaja jina.
Baadaye ilionekana wagonjwa hao wakirejeshewa fedha walizotoa kwa ajili ya vipimo na kumwona daktari.
Ramadhani Makuka wa Kimara anayesumbuliwa na tumbo, aliandikiwa na
daktari afike jana lakini alipofika aliandikiwa arudi Machi 22.
Hali mbaya zaidi, ilionekana katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya
Muhimbili (MOI) ambapo wagonjwa waliondolewa na kutakiwa kurejea mara
watakaposikia tangazo katika vyombo vya habari.
Mgonjwa wa mgongo, Rukia Hamis, mkazi wa Ununio alisema
amesikitishwa kwa baadhi ya maofisa kuwasumbua na kutumia gharama kufika
hospitali baada ya kuelezwa kuwa hakuna mgomo lakini kumbe upo.
Bryceson Sauli, aliyepata ajali ya mguu, alisema ifike mahali
wagonjwa nao waandamane kuhakikisha Serikali inawasikiliza madaktari,
ili waweze kupata haki zao za matibabu.
Huduma katika Hospitali za Amana na Temeke pia zilikuwa za
kusuasua, huku wakionekana idadi kubwa ya wagonjwa wa nje wakirejeshwa
nyumbani.
Dk. Ayub Kibao, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Amana
alisema wameamua kusitisha huduma za wagonjwa wa nje, baada ya madaktari
wanafunzi kuendesha mgomo.
Mgomo wa madaktari ulianza rasmi Jumanne na umeendelea kadri siku zinavyosonga mbele.
Chanzo: HabariLeo
Friday, January 27, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment