WABUNGE zaidi ya 100 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wanatarajia kushiriki maziko ya marehemu Regia Doto Mtema (32), Mbunge
wa Viti Maalumu (Chadema) yanayotarajia kufanyika leo nyumbani kwao
Ifakara, Morogoro.
Pia Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko katika ziara ya kikazi mkoani humo, anatarajia kushiriki maziko hayo.
Hayo yalibainika jana wakati wa utoaji heshima za mwisho kwa mwili
wa marehemu katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam ulioongozwa na
Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliiwakilisha Serikali huku upinzani
ukiwakilishwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Mwanasheria Mkuu Frederick
Werema, mawaziri na wabunge walishiriki.
Kati ya wabunge hao 50 waliteuliwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda
na watahudumiwa na Serikali wakiwemo wajumbe wote wa Kamati ya Uongozi,
wenyeviti wa kamati zote na wajumbe 10 wa Kamati ya Bunge ya
Miundombinu.
Wengine ni wabunge wote wa Mkoa wa Morogoro, wabunge sita
waliowakilisha CCM, wanne Chadema, watatu CUF na mmoja mmoja kutoka
NCCR-Mageuzi, UDP na TLP.
Wabunge wengine 50 walitokana na vyama vyao, makundi na taasisi
mbalimbali wakiongozwa na Makinda, Naibu Spika Job Ndugai na Naibu
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto .
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, Pinda aliwapa
pole Chadema kwa kuondokewa na Mbunge wao mwanamke mwenye uwezo mkubwa.
Alisema atamkumbuka sana kwani kila Alhamisi wakati wa kipindi cha
maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu aliuliza maswali, huku
akisisitiza kuwa si rahisi kwa Chadema kuziba pengo hilo la Mbunge
aliyekuwa na karama za pekee.
Alisema Rais Kikwete kabla ya kuanza ziara Morogoro alionesha nia ya kushiriki maziko hayo na kama ratiba haitambana atashiriki.
Makinda aliwataka wanawake kumuenzi Regia kwa kuthubutu kugombea nafasi za uongozi bila uoga.
“Regia ametuunganisha Watanzania kwa kutimiza upendo wa asili wa
Watanzania, kwani ni nyota iliyomulika Tanzania … kuishi wamoja licha ya
tofauti za kisiasa ambazo ni mapambio tu,” alisisitiza.
Makinda alisema Regia aliishi kwa upendo mpaka kwenye nyumba yake ya
Mbezi ambako alihifadhi watu wenye shida jambo lililoonesha kuwa
alikuwa Mbunge aliyejali matatizo ya watu na ndivyo wabunge
wanavyotakiwa kuishi.
“Katika mkutano uliopita wa Bunge ilikuwa kama ananiaga kwani
alinitumia karatasi ikisema ‘mama nakupenda … I love you so much’,”
alisema Makinda.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema Regia alijiunga
na chama hicho mwaka 2001, akiwa chuoni, huku akiamini na kusimamia
ukweli kwamba hakuna kazi mwanamume anaweza na mwanamke asiiweze.
Alisema ulemavu wake haukuwa kikwazo katika mapambano ndani ya
chama, ujasiri aliouonesha tangu awali alipofanya kazi makao makuu ya
chama kwa miezi miwili bila wazazi wake kujua.
Regia alikufa kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha eneo la Ruvu,
mkoani Pwani akitokea nyumbani kwake Mbezi-Makabe, Dar es Salaam, kwenda
Vigwaza akiwa na watu wengine saba akiwamo mama yake mdogo, Bernadeta
Mtema.
Taarifa za polisi wa Pwani zilidai kuwa alilipita lori na ghafla
kukutana uso kwa uso na lori lingine na alipojaribu kurudi upande wake,
alikosa mwelekeo na kupinduka na kupoteza maisha papo hapo huku wenzake
wakijeruhiwa.
Chanzo: HabariLeo
Tuesday, January 17, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment