MIAKA
13 imekatika tangu alipofariki dunia. Hivyo, wenye umri wa miaka
isiyozidi 20 au zaidi, ni vigumu kumfahamu, kumkumbuka au hata kumsikia.
Maspika watatu waliomtangulia hawakuwa Waswahili, yaani Waafrika.
Ni hayati Adam Sapi ambaye majina yake kamili yalikuwa Chifu Adam Sapi Mkwawa, mmoja wa wajukuu wa aliyekuwa Chifu wa Wahehe wa Iringa, Mtwa Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga, maarufu kama Mkwawa.
Kwa taarifa yako mkoa wa Iringa umeweka rekodi kwa kutoa maspika wawili wa nchi hii, mwingine akiwa ni spika wa sasa, Anne Semamba Makinda ambaye ni wa kabila la Wabena kutoka mkoani humo.
Sapi alikuwa spika wa bunge la Tanganyika tangu Desemba 27, 1962, akashikilia nafasi hiyo kwa ufanisi mkubwa hadi Aprili 25, 1994.
Mwaka 1973 hadi 1975 aliuacha wadhifa huo kwa muda baada ya kuteuliwa na Rais Julius Nyerere kuwa Waziri wa Nchi wa Maendeleo ya Mji Mkuu (CDA).
Mtanzania huyo alivunja rekodi ya kushika wadhifa huo kwa muda mrefu zaidi na alifanikiwa kufanya kazi yake bila matatizo kwani alikuwa akisimamia bunge la chama kimoja ambalo lilikuwa la watu ‘dugu moja’.
Akijulikana kama Mtwa (Chifu), Sapi alikuwa Mwafrika wa kwanza nchini kupewa cheo cha heshima cha Kepteni wa jeshi la wakoloni wa Uingereza la King’s African Rifles (KAR) ambalo ‘Waswahili’ walilitamka kama ‘KEYA’ wakimaanisha ‘kei ei ara’.
Ni chifu Adam Sapi Mkwawa, aliyekuwa Mhehe wa Kalenga, muumini wa dini ya Kiislam ambaye alifariki dunia Juni 25, 1999 kutokana na shinikizo la juu la damu.
No comments:
Post a Comment