WAKATI kashfa ya baadhi ya wabunge kuhongwa na kampuni za mafuta ili
yatetee mikataba yao haijapoa, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai ameibua
tuhuma nyingine nzito kwamba baadhi ya wawakilishi hao wamekuwa
wakiingia kwenye vikao wakiwa wamelewa pombe na sigara zisizo za
kawaida.
Katika siku karibuni, baadhi ya wabunge wamekuwa
wakinaswa na kamera wakiwa wamelala bungeni wakati vikao vinaendelea,
kwa maelezo ya uchovu, kauli ambayo huenda sasa ikaongeza mjadala
miongoni kama
kinachosababisha walale wakati vikao vinaendelea iwapo ni uchovu wa
kazi au ulevi.
“Kuna
wabunge ninavyohisi wanaingia bungeni wakiwa wamevuta sigara fulani
kubwa, kulamba vitu fulani au hata kupata bia mbili tatu,” alisema
Ndugai akihojiwa jana asubuhi katika kipindi cha medani za
siasa na uchumi cha Star tv.
Ndugai
alisema amekuwa akiona hali hiyo hasa Bunge la kuanzia mchana, bila
kueleza ni hatua ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na wawakilishi
hao wa wananchi wanapobainika wamelewa.
“Wabunge ni watu kama watu
wengine, wana tabia kama walivyo wanadamu wengine, wapo ambao kwa namna
ninavyohisi wanaingia bungeni hasa vikao vya kuanzia mchana wakiwa
wamepiga bia,” alisisitiza
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, mkoani Dodoma.
Ingawa
hakufafanua, inavyofahamika sigara yenye kulevya ni bangi,kulamba vitu
fulani vyenye kulewesha maana yake inaweza kuwa kuna baadhi ya wabunge
wanatumia dawa za kulevya, pia ulevi mwingine
wa kutumia bia.
Bila kueleza hatua ambazo Bunge linachukua kwa wabunge walevi,
Ndugai aliwataka wabunge kuweka maslahi ya taifa mbele na kujenga
tabia ya kuongea mambo wakiwa na ushahidi.
“Ni kwamba kuna wabunge wamekuwa wakizungumza mambo bila ushahidi,
hili jambo halikubali, wabunge wanapaswa kuzingatia sheria kama
walivyo Watanzania wengine, unapomtuhumu mtu lazima uwe na
ushahidi, lakini inasikitisha sana unakuta mbunge anasema jambo,
anamtaja mtu kwamba anahusika na hili na lile wakati hana hata chembe
ya ushahidi,” alisema.
Pia, aliwataka wanasiasa wote kujenga tabia za kuthamini yale ambayo yanafanywa na wanasiasa wengine.
“Nimekuwa
nikifuatilia mambo yanavyokwenda nchini, kuna wanasiasa wanakosea,
unakuta mpinzani amekuwa akisema mabaya tu kwa chama tawala, unakuta
tunaitwa mafisadi, siyo sahihi, kwa mfano Star tv kukawa na mtu mgoni,
ni tatizo la huyo haina maana kwamba wafanyakazi
wote ni wagoni. CCM ni taasisi kubwa, mambo haya yanaweza kutokea.
Lakini pia siyo kweli kwamba wanachama na viongozi wote wa upinzani ni wasafi,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Kuna wanasiasa wamekuwa na tabia ya kuona kila kinachofanywa na CCM
ni
ushetani, hiyo siyo sawa! Kwa mfano mimi jimboni nimefanya maendeleo
mengi. Wakati naingia Bungeni mwaka 2000 kulikuwa na shule chache mno za
sekondari, lakini sasa ziko zaidi ya 30, hata zahanati zilikuwa chache
sasa ni zaidi ya 40, ni kutokana na jitihada zangu na chama changu, mtu
anapokuja kusema hatujafanya kitu tunashindwa kumuelewa.”
Naibu
Spika huyo alikwenda mbali zaidi na kuwashauri viongozi wa Serikali
akiwamo Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa na utaratibu wa kupitia kauli
zinazotolewa na wanasiasa, kwa maelezo kuwa baadhi yao
wamekuwa wakitoa kauli nzito, au kukashifiana bila kuchukuliwa hatua.
“Unaweza
kukuta mwanasiasa anaibua kashfa nzito, lakini hachukuliwi hatua wala
kuulizwa, hiyo siyo sahihi. Wanasiasa tunapaswa kubishana kwa hoja, siyo
vinginevyo,” alisema Ndugai.
Ndugai alipoulizwa kuwa wabunge hao
hatua watakazochukuliwa kutokana na tabia zao, alisema suala hilo haina
haja ya kulizungumzia zaidi ila libaki kama alivyosema.
“Hilo siwezi kulizungumzia zaidi libaki kama nilivyozungumza na walioniomba nizungumze nao,” alisema.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment