BAADA ya kimya cha muda mrefu, Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusuf
Makamba ameibuka na kusema kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi
kuletwa na Rais Jakaya Kikwete.
Amesema kuwa mbunge mzuri
anaweza kutoka chama chochote iwapo Watanzania watashirikiana naye
katika kuleta maendeleo ya eneo husika.
Makamba ametoa kauli hiyo
ikiwa imepita muda mrefu tangu aibuke katika kikao cha Halmashauri Kuu
ya chama hicho (Nec) na kumtuhumu Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye kwamba amekigeuza chama kuwa mali yake binafsi.
Katika kikao
hicho Makamba alisema hatua ya Nape kugeuza chama hicho kama taasisi
yake binafsi ndiyo ambayo imesababisha kikose mwelekeo.
Lakini
jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam muda
mfupi baada ya mwanaye, January ambaye ni Mbunge wa Bumbuli na Naibu
Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia kufungua mkutano wa wakazi
wa jimbo hilo, Makamba alisema maendeleo ya Watanzania yataletwa na wao
wenyewe, kwa kufanya kazi.
Huku akizungumza baadhi ya maneno kwa
lugha ya kisambaa na kunukuu baadhi ya vifungu vya biblia takatifu,
Makamba alisema Watanzania wamekuwa wavivu wa kufanya kazi na kwamba
kila kitu wanategemea kitafanywa na Rais Kikwete.
Makamba alisema kuwa kwa sasa kumezuka tabia ya baadhi ya Watanzania kuwatupia lawama viongozi kwa kushindwa kuwapa maisha bora.
Makamba,
alisema kuwa maendeleo hayawezi kuletwa na mbunge peke yake bali
kinachohitajika ni ushirikiano wa pamoja ili kuweza kutimiza lengo na
ahadi mbalimbali alizotoa.
Alisema kuwa anashangazwa na baadhi ya
Watanzania kuamua kumtupia lawama Rais Kikwete kuwa kashindwa kuleta
maisha bora wakati hawana umoja wa kuunganisha nguvu katika kutatua
changamoto zinazoikabili nchi.
“Hata kama CCM itaondoka madarakani
na kuingia Chadema bado Watanzania wataendelea kulia umaskini kwa kuwa
hatuna tabia ya kushirikiana na kufanya kazi,” alisema Makamba.
Makamba
alimwagia sifa mwanaye, January ambaye alikuwa akizindua Shirika la
Maendeleo Bumbuli (SMB)ambalo alilianzisha baada ya kuwa mbunge mwaka
2010, kusema kuwa kijana huyo ni mfano wa kuigwa na Watanzania kwa kuwa
katika kipindi kifupi cha uongozi wake jimboni humo ameweza kutekeleza
ahadi mbalimbali.
Alisema kuwa wananchi wa Bumbuli hawakufanya
makosa kumchagua mbunge huyo na kuongeza kwamba wanatakiwa kumpa
ushirikiano ili kulifanya jimbo hilo kupiga hatua kimaendeleo.
Kwa
upande wake, January wakati akiwakaribisha wakazi wa Bumbuli pamoja na
waliotoka mikoa jirani, alisema kuwa wamekutana ili kuangalia namna ya
kukabiliana na changamoto zilizopo jimboni humo.
Alisema kuwa
siku zote maendeleo huletwa na wakazi waliopo mbali na nyumbani hivyo
aliwaomba kuhakikisha kuwa na umoja ili kuondoa matatizo yaliyopo
jimboni humo ikiwa ni pamoja elimu, afya, miundombinu na maji.
Alisema kwa upande wake atahakikisha BDC, linawasaidia wakazi hao katika masuala ya ajira na elimu.
Alisisitiza
kuwa ili kuinua kiwango cha ufaulu katika jimbo hilo wamebuni njia ya
kupandisha ufaulu wa wanafunzi kwani kuanzia sasa wameanzisha kambi ya
wanafunzi zaidi ya 150 waliofanya vizuri katika mitihani yao ya mokono
ili kuwanoa zaidi, lengo likiwa ni kuhakikisha wanafanya vizru katika
mtihani wao wa mwisho.
Januari ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi
na Mawasiliano, alisema kuwa wamegundua kuwa baadhi ya wazazi jimboni
humo wamekuwa kikwazo cha wanafunzi kushindwa kufanya vema mitihani yao.
aliongeza
kuwa BDC imepata fedha kiasi cha Sh 730 milioni kwa ajili ya kukusanya
na kununua mazao ya mboga mboga yaliyopo jimboni humo, hatua ambayo
itasaidia kununuliwa kipato cha wakulima.
Alisema hatua hiyo
itakwenda sambamba na kukifufua kiwanda cha matunda cha Maweni ambapo
mkulima ataweza kuuza mazao yao huko na kuepukana na madalali na kwamba
vijana zaidi ya 120 watapata ajira.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, August 5, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment