MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema amesema Sheria
ya Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), ni nzuri na kwamba
haipaswi kufanyiwa mabadiliko kama ambavyo imekuwa ikidaiwa.
Jaji
Werema aliliambia gazeti hili jana kuwa haoni haja ya sheria hiyo
kufanyiwa mabadiliko sasa kwa kuwa haina tatizo na ipo kutekeleza
misingi ya utawala wa Sheria.
"Mimi nakubaliana na Sheria hii ya
(Takukuru) kwamba iendelee kuwapo. Hakuna haja ya kuifanyia mabadiliko
sasa. Ni nzuri kwa kuwa inazingatia misingi ya utawala wa sheria,"
alisema Jaji Werema.
Kauli ya Jaji Werema inapingana na ile
iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah kwamba
sheria hiyo imekuwa ikiwakwaza kuwashughulikia wala rushwa wakubwa,
kwani majalada ya kesi zilizokwishafanyiwa uchunguzi yamekwama kwa
Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP).
Wiki iliyopita Dk Hoseah
alilalamikia sheria hiyo, hasa kifungu cha 37 na 57 akisisitiza kuwa ni
mbovu kwa kuwa vinamzuia kuwafikisha watuhumiwa wa rushwa kubwa
mahakamani. “Tusaidieni sheria hii ibadilishwe ili iweze kuturuhusu
kufanikisha kupambana na rushwa nchini,” alisisitiza Dk Hoseah.
Hata
hivyo, jana Werema alipinga dhana hiyo na kusema kwamba siyo sahihi
kuipa Takukuru mamlaka yote; kutuhumu, kupeleleza na kushtaki kwa kuwa
kufanya hivyo ni kinyume na demokrasia, Katiba na utawala wa sheria.
Kumrundikia mtu au taasisi moja mamlaka zote hizo, ni kinyume na misingi ya utawala bora, alisema.
"Haiwezekani
mtu (Dk Hoseah) akawa na mamlaka ya kupeleleza na kushtaki, halafu
Mahakama ikiwaachia huru watuhumiwa, atasema siyo mimi ni kosa la
Mahakama, We can't do that! (hatuwezi kufanya hivyo)," alisema Werema na
kuongeza:
"Mimi nakubaliana na kitu kimoja, kila mamlaka iwe na
kigingi. Iwe Mamlaka ya Rais, Bunge au Mahakama, lazima kuwe na chombo
cha ku-check and balance," alisema Jaji Werema.
Kauli hiyo ya
Jaji Werema imekuja siku chache tangu Mkurugenzi wa Mashtaka, (DPP)
Eliezer Felishi kukiri kwamba kazi ya kuwafikisha watuhumiwa hao
mahakamani ni yake, lakini kesi nyingi zinakwama.
DPP Feleshi
alisema ucheleweshaji wa kesi za rushwa kupelekwa mahakamani, unatokana
na kukosekana kwa ushahidi wa kutosha. "Ikifikia hapo, nalazimika
kuyarudisha mafaili hayo kwa Takukuru," alisema.
"Mimi nafanya
kazi kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali. Siwezi
kufanya kazi kwa sababu mtu fulani ametaka nifanye. Jambo hilo linaweza
kuniletea matatizo baadaye," alisema na kuongeza:
"Kutokana na
hali hiyo, siwezi kupeleka mahakamani jalada ambalo halijakamilika.
Sheria inanipa siku 60 niwe nimepeleka kesi mahakamani, lakini kama
ushahidi haupo cha kufanya ni kurudisha Takukuru faili.”
Madai ya Dk Hoseah
Awali
Dk Hoseah alisema anajua matarajio ya wananchi ni makubwa kwa Takukuru,
lakini sheria imewafunga mkono kwa kuwa hawawezi kuchukua uamuzi dhidi
ya kesi kubwa za ufisadi bila ushauri wa DPP.
“Sina mamlaka ya
kumpeleka mtuhumiwa wa rushwa kubwa mahakamani. Uwezo wangu ni kupeleka
walarushwa ndogondogo tu na kwamba kazi yangu ni kuchunguza tu,” alisema
Dk Hoseah na kuongeza;
“Sheria yetu imetufunga mikono kwa kuwa kumpeleka mtu mahakamani siyo uamuzi wangu, bali ya DPP.”
Awali
Dk Hoseah alisema sheria hiyo katika kifungu cha 57 inamzuia kuwapeleka
mahakamani watuhuhumiwa wakubwa wa rushwa, mpaka awafikishe kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP).
Kifungu hicho cha 57 (1)
kinasema kuwa shtaka lolote la kosa lililoelezwa kwenye Sheria ya
Takukuru lazima lifunguliwe kwa ruhusa ya maandishi kutoka kwa DPP.
Kifungu cha 57 (2) kinamtaka DPP ndani ya siku 60 kutoa au kukataa
ruhusa ya kushtakiwa.
Dk Hoseah alisema, hiyo ni moja ya
changamoto zinazoikabili taasisi yake na kwamba wananchi wasubiri
mabadiliko ya kiutendaji kama sheria itabadilika na kumruhusu kufanya
hivyo.
Maelezo ya Dk Hoseah yanaungwa mkono na sehemu ya taarifa
ya awali ya Mpango wa Nchi za Afrika wa Kujitathmini (APRM) ambayo
inaeleza kwamba kikwazo cha ufanisi katika vita ya rushwa nchini
Tanzania ni sheria inayowazuia Takukuru ipate kibali cha DPP kabla ya
kufungua kesi kubwa za rushwa.
“Ni wala rushwa wadogo wadogo tu
ndiyo wanaoweza kushtakiwa na Takukuru, lakini makosa makubwa ya rushwa
yanayohusu viongozi au watu wa karibu na viongozi wakubwa ni mara chache
sana kufunguliwa kesi mahakamani,” inasema sehemu ya taarifa hiyo na
kuongeza:
“Mfumo huu ni kama unainyima mamlaka ya kiutendaji
Takukuru na kimsingi, unakandamiza juhudi za chombo hiki kupambana na
rushwa”.
Hii siyo mara ya kwanza kwa ofisi hizi mbili kuvutana
kuhusu udhaifu katika sheria ya Takukuru, lakini mara zote Serikali
imekuwa ikisisitiza kwamba lazima mashtaka kwa watuhumiwa wakubwa wa
rushwa wapate yapate kibali cha DPP kabla ya kufikishwa mahakamani.
Chanzo: Mwananchi
Monday, August 20, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment