Vita kubwa ya kuwania uenyekiti wa
Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeonekana
dhahiri, baada ya vigogo wawili wenye nguvu kuchukua fomu za kuwania
kiti hicho.
Kuwepo kwa vita kali katika kinyang’anyiro hicho kunatokana na
kujitokeza kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne-Kilango Malecela, kuchukua
fomu hizo jana.
Mwenyekiti wa sasa wa UWT Taifa, Sophia Simba, juzi alikuwa wa kwanza
kuchukua fomu hizo kutetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika
Oktoba, mwaka huu.
Kilango ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM,
alichukua fomu hizo akiwa ameongozana na mumewe ambaye ni mwanasiasa
mkongwe nchini na ndani ya CCM, Mzee John Malecela.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana baada ya
kukabidhiwa fomu na Katibu Msaidizi Mkuu wa UWT, Martha Kanakamfumo,
Kilango alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa ndani ya CCM
kwa kuwa ana uwezo wa kuwaandaa wanawake kiuchumi na kisiasa.
“Wanawake katika ngazi ya wilaya wanapaswa kuandaliwa wawe kuwa na nguvu
za kiuchumi na kisiasa ili wapate na uwezo kutembea nyumba hadi nyumba
nyakati za uchaguzi na kukiletea chama chetu ushindi,” alisema Kilango.
Kuhusu uzoefu wake ndani ya UWT, Kilango alisema amewahi kuwa mwenyekiti wa umoja huo katika ngazi ya wilaya.
“Uwezo wangu wa kisiasa umetokana na uongozi wa Mwenyekiti wa UWT ngazi
ya wilaya, Wilaya ya Kinondoni. Kwa kifupi nguvu yangu ya kisiasa
inatoka ndani ya tumbo la UWT,” alisema Kilango.
Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,
alichukua fomu hizo juzi asubuhi katika ofisi za UWT mjini hapa.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hizo Simba, alisema ameamua kutetea
nafasi hiyo kwa mara nyingine ili amalizie mambo aliyoyaanza wakati wa
uongozi wake, ikiwemo ujenzi katika viwanja mbalimbali vya umoja huo
nchini.
“Kutokana na uzoefu nilioupata miaka minne iliyopita, tumekuwa kitu
kimoja katika kipindi chote, wanawake wenzangu wamenipa ushirikiano
mzuri wakati wa utekelezaji wa majukumu yangu ndiyo umenihamasisha
kugombea kwa mara nyingine nafasi hii,” alisema Sophia.
Sophia alisema katika kipindi chake cha uongozi, anajivunia kutembelea
mikoa yote nchini na kuzungumza na wanawake kuhusiana na mambo
mbalimbali ya maendeleo.
Sophia alisema iwapo atachaguliwa kuongoza kwa mara nyingine jumuiya
hiyo, ataendeleza waliyoyaanzisha ikiwemo Chama cha Ushirika wa Kuweka
na Kukopa (Saccos) ambacho kitazinduliwa Septemba, mwaka huu.
Ingawa bado vigogo zaidi hawajajitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi
hiyo, lakini kujitokeza kwa Sophia kutetea nafasi yake na Kilango
kujaribu kwa mara ya kwanza, ni sababu tosha za kukifanya kinyang’anyiro
hicho kuwa na ushindani wa hali ya juu.
Hali hiyo inatokana na Sophia kuwa na ushawishi kwa wajumbe wengi akiwa
kama mwenyekiti na vile vile kuungwa mkono na vigogo wa juu wa chama
hicho akiwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC).
Kwa upande wake, Kilango siyo mtu wa kupuuzwa kwa kuwa pia kama mbunge
na mjumbe wa NEC, ana ushawishi mkubwa na vile vile anaweza kunufaika
kutokana na umaarufu wa mumewe ambaye ni Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza
wa Rais mstaafu, Makamu Mwenyekiti Bara na mjumbe wa kudumu wa NEC na
CC.
Katika uchaguzi uliopita uliomwingiza madarakani, Sophia alimshinda
Janeth Kahama, mke wa mwanasiasa mkongwe nchini, George Kahama, huku
ukiwemo ushindani mkali.
Kimsingi, nafasi ya uenyekiti wa UWT ni nyeti sana ndani ya chama hicho
kwa kuwa mwenyekiti anakuwa mjumbe wa NEC na CC moja kwa moja, ambavyo
ni vikao vya kufanya mamuzi makubwa ya chama.
Kwa mfano, kinyang’anyiro hicho kitakuwa ni mwelekeo wa kupanga safu za
uongozi wa chama na dola kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012.
Kwa kujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, uchukuaji wa fomu kwa ajili ya uchaguzi huo utaendelea hadi Agosti 6, mwaka huu.
Chanzo: Ippmedia
Friday, August 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment