MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewasafisha aliyekuwa Balozi wa
Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Ofisa Utawala wa ubalozi
huo, Grace Martin waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na
kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 Milioni.
Kutokana na uamuzi huo, Profesa Mahalu amesema anamshukuru Mungu akisema, yaliyotokana ni kwa sababu Mungu amempenda.
“Mungu
amenipigania sana na haki imetendeka, sasa hivi nakwenda kanisani
kumshukuru Mungu, nanyi nawaambieni mkasome Zaburi 17,” alisema Profesa
Mahalu kwa furaha na kukumbatiana na mawakili na ndugu zake.
Profesa
Mahalu na Martin walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya
kula njama na kuiibia Serikali na kuisababishia hasara ya Euro
2,065,827.60, katika mchakato wa ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania
nchini Italia.
Hata hivyo, jana Mahakama hiyo iliwaachia huru
ikisema kuwa upande wa mashtaka katika kesi hiyo namba 1 ya mwaka 2007,
umeshindwa kuthibitisha mashtaka hayo bila kuacha mashaka.
Akisoma
hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ilvin Mugeta aliyekuwa
akisikiliza kesi hiyo alisema kuwa katika ushahidi uliotolewa na
mashahidi wote saba wa upande wa mashtaka, hakuna ushahidi wa moja kwa
moja unaowatia hatiani washtakiwa hao.
Alisema ushahidi uliopo ni
wa mazingira tu ambao ulikuwa umesimamia katika nyaraka mbalimbali
zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kuhusiana na
mchakato wa ununuzi wa jengo hilo.
Katika hukumu yake, Hakimu
Mugeta alirejea na kusisitiza ushahidi uliotolewa na Rais wa Awamu ya
Tatu, Benjamin Mkapa akimtetea Profesa Mahalu kuwa ni msomi mzuri,
mchapakazi, mwadilifu na mwaminifu.
Pia hakimu Mugeta alihoji
ilikuwaje hata mshtakiwa wa pili, Martin akaunganishwa katika kesi hiyo
kwa kuwa nyaraka zote zilizowasilishwa mahakamani hapo ambazo ndizo
upande wa mashtaka ulizitumia katika mashtaka zilikuwa zinamhusisha
mshtakiwa wa kwanza tu.
“Mwishowe napenda kusema kwamba
nimeshindwa kufahamu ni kwa nini mshtakiwa wa pili alishtakiwa na ndiyo
maana katika hukumu hii sikugusia ushahidi wake wa utetezi,” alisema
Hakimu Mugeta na kuongeza:
“Kwa kuhitimisha ninasema kwamba
upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka bila mashaka yote
katika makosa yote sita na washtakiwa wote wanaachiwa huru katika makosa
yote.”
Wakati akisoma hukumu hiyo,Hakimu Mugeta alianza
kuchambua ushahidi wa upande wa mashtaka na ushahidi wa utetezi kisha
akaanza kuainisha ushahidi huo jinsi ulivyoweza au ulivyoshindwa kuwatia
hatiani washtakiwa hao kwa kosa moja baada ya lingine.
Kwanza,
Hakimu Mugeta alisema anawaachia huru katika kosa la pili la wizi na kwa
sababu hiyo hata kosa la kwanza la kula njama ili kutenda kosa hilo
likawa limekufa kwa kuwa makosa hayo yote yanategemeana.
Akizungumzia
kosa la kula njama, Hakimu Mugeta alisema dhana ya kosa hilo upande wa
mashtaka uliegemea kwenye uwepo wa mikataba miwili ya ununuzi wa jengo
hilo.
“Siko tayari kutumia dhana yao hiyo isipokuwa kama
nitashawishiwa kupita mashaka yote kwamba matumizi ya mikataba miwili
kununua jengo la ubalozi lenyewe tu inaunda kosa la jinai,” alisema
Hakimu Mugeta.
Aliongeza kuwa upande wa mashtaka ulijielekeza kwenye kutambua kama kulikuwa na kibali cha kutumia mikataba miwili au la.
“Sidhani
kama hili linahusiana katika mazingira ya kesi hii. Hii ni kwa sababu
kama utumiaji wa mikataba miwili ni kosa la jinai, hakuna kibali ambacho
kingeweza kuhalalisha hilo isipokuwa tu kwa kubadilisha sheria
husika,”alisisitiza Hakimu Mugeta.
Hakimu Mugeta alirejea
ushahidi wa utetezi wa Mkapa kuwa hata kama lengo la muuzaji wa jengo
hilo lilikuwa ni kukwepa kodi ya nchi yake, hilo ni tatizo la mwenye
jengo na nchi yake na kwamba matakwa ya nchi yalikuwa ni kupata jengo la
ubalozi.
Hakimu Mugeta alisema kwa mujibu wa kielelezo cha 5 cha
upande wa utetezi [exhibit D5], taarifa ya mthamini kutoka Wizara
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, thamani ya jengo hilo ilikuwa ni
Dola za Marekani 5.5milioni.
Alisema hata hivyo, tathmini ya
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bei ya jengo hilo
ilikuwa ni Euro 3,098,741.38 na kwamba ndiyo maana ilituma kiasi hicho
ambacho ndicho kilicholipwa kwa mnunuzi.
Kuhusu shtaka la wizi,
Hakimu Mugeta alisema kuwa hakuna ushahidi unaonyesha kuwa baada ya
kiasi hicho cha pesa kulipwa kwa mwenye jengo kupitia akaunti mbili
tofauti za benki za mwenye jengo, baadaye Mahalu alikwenda benki
kuzichukua pesa hizo kwa matumizi yake binafsi.
Alisisitiza kuwa
mshtakiwa wa kwanza alipewa mamlaka ya kununua jengo hilo kwa bei
iliyoonyeshwa katika kielelezo hicho cha 7 cha upande wa mashtaka yaani
Euro 3,098,741.38.
Hakimu Mugeta alisema kwa maoni yake ni kwamba
ikiwa mshtakiwa baada ya Serikali kukubali bei hiyo ya ununuzi wa jengo
hilo, kutoa pesa, na kumpa mshtakiwa wa kwanza nguvu ya kisheria,
utaratibu wa malipo ulipaswa kufuata taratibu za Italia.
Alisema
hayo ni masharti ambayo muuzaji alimpa mshtakiwa wa kwanza na kwamba
shahidi wa pili upande wa utetezi, Mkapa alisema kuwa mahitaji ya nchi
yalikuwa ni kupata jengo.
Hakimu Mugeta alisisitiza kwamba kwa
mujibu wa ushahidi wa upande wa mashtaka na hata wa utetezi, taratibu
zote za ununuzi wa jengo hilo zilifuatwa na kwamba ndiyo maana wataalamu
walitumwa kwenda kufanya uthamini.
Kutokana na makosa hayo
kutokuthibitishwa na upande wa mashtaka, Hakimu Mugeta pia alitupilia
mbali kosa la kuisababishia hasara Serikali akisema kuwa pia upande wa
mashtaka umeshindwa kulithibitisha.
Utetezi wa Mkapa
Wakati
wa utetezi wao, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye ununuzi wa
jengo hilo ulifanyika wakati wa uongozi wake alipanda kizimbani na
kumtetea Mahalu na mwenzake, akidai kuwa mchakato wa ununuzi wa jengo
hilo ulifuata sheria.
Mkapa katika ushahidi wake wa utetezi licha
ya kudai kuwa mchakato huo ulifuata taratibu na kwamba ni yeye
aliyebariki, pia alimmwagia Mahalu sifa nyingi akidai kuwa ni kiongozi
mwadilifu na mwaminifu katika historia yake ya utumishi wa umma.
Akiongozwa
na mmoja wa mawakili wanaomtetea Mahalu na mwenzake, Wakili Alex
Mgongolwa, Mkapa alieleza mchakato wote wa ununuzi wa jengo hilo na
malipo yake kwa kuwa lilinunuliwa kwa maagizo Serikali yake.
Wakati
upande wa mashtaka ukidai kuwapo kwa uhujumu uchumi kutokana na kuwapo
kwa mikataba miwili wakati wa ununuzi wa jengo hilo, Mkapa alidai kuwa
aliifahamu mikataba hiyo yote na malipo kufanyika kupitia akaunti mbili
tofauti.
Alienda mbali zaidi na kueleza kushangazwa kusikia kuwa
aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo, Martin Lumbanga katika
ushahidi wake alidai kuwa hakujua mchakato wa ununuzi wa jengo hilo,
akieleza kuwa haujui ni kwa nini Lumbanga alisema hivyo.
Mbali na
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo wakati wa
ununuzi wa jengo hilo, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyekuwa waziri wake,
Mkapa alisema wizara nyingine zilizohusika ni Wizara ya Ujenzi na Wizara
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Alidai kuwa wizara zote hizo zilituma wataalamu wake kwenda kufanya tathmini ya thamani ya jengo hilo kabla ya ununuzi wake.
Alisisitiza
kuwa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wakati huo, Kikwete
bungeni juu ya ununuzi wa jengo hilo ni sahihi.
Pamoja na mambo
mengine taarifa hiyo inaeleza kuwa jengo hilo lilinunuliwa kwa Sh2.9
bilioni na kwamba hati za umiliki wake zilishawasilishwa wizarani na
kupelekwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali [CAG].
“Maneno
hayo ni sahihi. Hayo ndiyo ninayoyajua mimi,” alidai Mkapa na kuongeza
kwamba hajawahi kupata malalamiko kutoka Italia kuhusu ukiukwaji wa
sheria wakati wa mchakato wa ununuzi wa jengo hilo wala kwa mmiliki
akidai kuwa alilipwa pungufu ya makubaliano.
Akijibu swali la
Wakili Mgongolwa kama alishapata malalamiko yoyote kutoka kwa CAG kuhusu
ununuzi wa jengo hilo, alijibu kuwa hajawahi kupokea malalamiko hayo.
Akijibu
swali la Wakili wa Serikali, Ponsiano Lukosi kama aliwahi kuuliza ni
kwa nini mwenye jengo alitaka alipwe kupitia mikataba miwili Mkapa
alijibu kuwa hakuuliza kwa kuwa alichokuwa anahitaji ni kupata jengo.
Kuhusu
kama lengo la mwenye jengo kutaka kulipwa kwa mikataba miwili lilikuwa
ni kukwepa kodi ya Serikali ya nchi yake, Mkapa alijibu:
“Hilo ni tatizo lake na nchi yake, mimi nilikuwa nataka nyumba na nimepata nyumba, nasema Alhamdulilah”.
Pia
Mkapa alisema kuwa anamshangaa sana wakili wa Serikali kudai kuwa pesa
hizo kulipwa kwa awamu mbili Mahalu alikuwa na lengo za kuzichukua na
kuzitumia kwa masilahi yake.
“Mimi nitashangaa sana kusikia hivyo na hasa nitakushangaa wewe maana Profesa [Mahalu] mimi namwamini.”, alisisitiza Mkapa.
Maoni nje ya mahakama
Baada
ya hukumu hiyo kutolewa, mawakili waliokuwa wakimtetea Balozi Mahalu na
mwenzake, Martin waliizungumzia hukumu hiyo kwa nyakati tofauti.
Wakili
Mabere Marando, baada ya Hakimu Mugeta kuwaachia huru wateja wake saa
7:27 mchana alisema kuwa ana furaha kubwa kwa kuwa Mahakama imetenda
haki.
“Hukumu hii iliyotolewa leo kweli ni ya kihistoria kwa
sababu ni hukumu ya haki, hakimu amejitahidi kueleza hoja na zote ni za
muhimu na kwamba hapakuwepo na sheria ya kumshtaki Mahalu,”alisema
Marando huku akiwa ni mwenye tabasamu.
Wakili Alex Mgongolwa ambaye naye pia alikuwa akiwatetea kina Mahalu, alisema kuwa ana furaha kwa kuwa haki imetendeka.
“Kwa kweli haki imeonekana kutendeka na imetendeka; Mahakama imetenda haki,”alisema Mgongolwa huku akicheka.
Naye Martin alisema: “Namshukuru Mungu kwa kushinda kesi hii.”
Wakati
hayo yote yakiendelea mahakamani hapo, ndugu wa Mahalu na Martin
walikuwa na furaha huku wakituma ujumbe mfupi kweye simu zao za mkononi
wakiwajulisha wenzao juu ya tukio hilo.
Katika utetezi wao,
upande wa Jamhuri ilileta jumla ya mashahidi saba ambao ni aliyekuwa
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Martin Lumbanga,
Stewart Migwano, Marco Papi, Kapteni Abubakari Ibrahim, Mkongoti, Kyando
kutoka Takukuru na nyaraka mbalimbali.
Utetezi wa Mahalu
Awali
akitoa utetezi wake katika mahakama hiyo, Mahalu alidai kuwa alipofika
katika Ubalozi huo wa nchini Italia alikuta ofisi zikiwa na hali mbaya
hali iliyosababisha kutoa fedha zake mfukoni na kununua thamani zenye
hadhi ya ofisi ya ubalozi.
Akiongozwa kutoa utetezi wake na
wakili wake Marando na Mgongolwa alidai kutokana na kuikuta ofisi hiyo
ikiwa na hali hiyo mbaya alilazimika kutoa fedha zake mfukoni kwa ajili
ya kununulia samani za ofisini.
Mahalu alidai kuwa Aprili 1,
mwaka 2000 ndiyo siku aliyofika rasmi mjini Rome nchini Italia ikiwa ni
siku chache baada ya Mkapa kumteua kuwa Balozi ambapo alieleza majukumu
yake yalikuwa ni kulinda na kuyatetea masilahi ya Tanzania na wakati
akiwa Balozi wa Italia pia wakati huo huo alikuwa ni balozi wa nchi tisa
ambazo ni Greece, Turkey, Serbia, Slovenia,Croatia, Macedonia,
Montenegro.
Alieleza jukumu lake jingine ni kupokea maelekezo
kutoka hapa nchini kuhusu kukuza uhusiano baina ya nchini na nchi na
kwamba yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa masuala yote ya utawala wa ofisi ya
ubalozi na kwamba masuala yote ya utawala yalikuwa yakiletwa kwake na
maofisa wa ubalozi na Serikali kwa ujumla.
“Nilipofika Italia
nilikuta hali ni mbaya inasikitisha kwani ubalozi wa wetu nchini Italia
ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na nilipoteuliwa mimi kwenda huko
ndiyo nikawa nimeenda kuufungua ubalozi huo uanze kufanya kazi. Na
wakati nafika hapo kila kitu cha ubalozi kilikuwa kimeondolewa na
kurudishwa nchini kikabaki kiofisi kidogo tu kwa ajili ya kushughulikia
masuala ya kilimo na mwaka 1997 ndiyo Serikali ilimpeleka msimamizi wa
ofisi hiyo.”
Alidai kuwa baada ya kukuta hali hiyo alichukua
hatua ya kumweleza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo, Balozi Kibeloh na kwamba
aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo kwa kipindi hicho alikuwa Jakaya Kikwete
ambaye kwa sasa ndiye Rais wa nchi ambaye naye alifika katika ofisi za
ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya.
Alidia Kikwete aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.
Aliendelea
kueleza mbali na Kikwete, pia aliyekuwa Makamu wa Rais , Dk Ali Mohamed
Shein naye alitembelea ofisi hizo za ubalozi na kushuhudia ubovu ule na
akamuahidi mshtakiwa huyo kuwa akirudi nchini atafikisha tatizo hilo
ili taratibu zifanywe za kupatikana jengo kubwa la ubalozi.
Profesa
Mahalu alieleza kuwa baada ya kumweleza matatizo hayo ya ubalozi Katibu
Mkuu, Balozi Kibeloh, alikubaliana naye akasema ni muhimu kwa Serikali
kutafuta jengo jipya na kwamba Mei 2001, alipewa taarifa na balozi huyo
kuwa Rais Mkapa atakwenda Brussels kwa ziara ya kikazi na kwamba yeye
mshtakiwa akamwomba tena katibu mkuu huyo amruhusu akamweleze Mkapa
matatizo hayo pindi atakapofika Brussels na katibu mkuu huyo alimruhusu.
“Niliporudi mjini Rome Italia, nilimjulisha kwa barua Katibu
Mkuu Balozi Kibeloh mazungumzo yangu na Rais Mkapa na balozi huyo naye
akanijibu kuwa atazidi kulifuatilia jambo hilo na kuliweka kwenye bajeti
ya Wizara ya Mambo ya Nje na kwa sababu hiyo ilikuwa ni sera ya wizara
yake ya kutaka ofisi za ubalozi wetu nje ya nchi zinunue majengo yao
hivyo hoja hiyo itapelekwa bungeni na haitapingwa. ”alidai Profesa
Mahalu.
Mshtakiwa huyo aliendelea kueleza kuwa wakati akisubiri
ahadi hiyo ya Katibu Mkuu huyo, mwanzoni mwa Juni 2001, Katibu Mkuu huyo
alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya
kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na Bunge na
kuongeza kuwa Katibu Mkuu alimtaka mshtakiwa huyo na maofisa wengine wa
ubalozi kuanza kutafuta majengo.
Alidai kuwa baada ya kupokea
habari hiyo njema kutoka kwa Katibu Mkuu, yeye mshtakiwa alimwandikia
barua ya kumshukuru Mei 4 mwaka 2009 ambayo nakala yake aliomba mahakama
iipokee kama kielelezo na Hakimu Mugeta aliipokea kama kielelezo cha
kwanza.
Utetezi wa Grace
Mei 8, mwaka huu, Martin ambaye
alikuwa Ofisa wa Utawala aliieleza mahakama hiyo ya Kisutu kuwa Balozi
Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro 2 milioni, bali alileta
faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa
shukrani.
Akiongozwa na Wakili Marando kujitetea dhidi ya tuhuma
zinazomkabili, Martin alidai kuwa kwa ufahamu wake Balozi Mahalu
hakuisababishia Serikali hasara kwa kuwa ununuzi ulileta faida na nchi
kupata jengo zuri na fedha hazikupotea na anastahili shukrani.
Aliendelea
kuiomba Mahakama itupilie mbali tuhuma hizo na kwamba madai ya kuwa
Balozi Mahalu alitumia risiti ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania
nchini Italia kuidanganya Serikali kuwa mwenye nyumba amelipwa fedha
siyo ya kweli.
Chanzo: Mwananchi
Thursday, August 9, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment