WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amewataka
wanaotangaza kuwafahamu vigogo walioficha mabilioni ya fedha nje ya nchi
kuwataja mara moja ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao badala
ya kuisubiri Serikali kufanya hivyo.Kauli hiyo ya Sitta ambaye pia ni
Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), imekuja wakati baadhi ya wanasiasa,
wakiwamo wabunge kutishia kuwataja watu hao, lakini wakisisitiza kuwa ni
pale tu Serikali itakaposhindwa kufanya hivyo.
Utafiti
uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Fedha la Global Financial
Integrity, unaonyesha kuwa tatizo la utoroshaji wa fedha nchini
limekuwapo katika awamu zote za Serikali zilizoiongoza Tanzania, lakini
Awamu hii ya Nne imetia fora.
Utafiti huo uliofanywa kuanzia
mwaka 1970 hadi 2009, unaonyesha kuwa katika utawala wa Rais Jakaya
Kikwete, fedha zilizofichwa nje ya nchi ni Dola za Marekani 7,967.4
milioni (sawa Sh12.7 trilioni).
Akizungumza katika mahojiano maalumu,
kuhusu nini kifanyike ili kuiokoa Tanzania isiendelee kufilisiwa na
watu wachache, Sitta alisema anasikitishwa na watu hao kuogopa na
kuwaficha watu wanaofisadi mali za nchi na hasa pale inapokuwa wahusika
ni vigogo wa Serikali.
Alisema vigogo hao ni sababu ya watu
kupata kigugumizi katika hili akihoji : “Kwa nini linapokuwa ni suala
linalowahusu hawa wanaoitwa vigogo hawatajwi?”
Sitta ambaye
ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini katika awamu tofauti, alisema
haoni kama kuna kosa kumtaja hadharani mtu aliyeficha fedha nje ya nchi
huku akisababisha Watanzania kuendelea kukabiliwa na maisha magumu.
“Watajwe!
Kama ni Samuel Sitta ameficha fedha nje atajwe. Kwa kweli mimi sioni
kama kuna dhambi yoyote kumtaja,” alisema Sitta huku akisisitiza kwamba
huo ni msimamo wake binafsi unaotokana na uzoefu wake kwenye uongozi wa
nchi na siyo kwa mamlaka aliyonayo ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Alisema njia nzuri ya kukomesha tabia hiyo ni kuwataja
na vyombo husika kuwafikisha mahakamani kwa kuzingatia kuwa sheria ni
msumeno, haipaswi kubagua aliye mdogo au mkubwa kwa maana ya wadhifa
katika nchi.Sitta ambaye pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge alisema: “Swali
la kwa nini hawatajwi, ni jambo la kushangaza.”
Alisema amesikia
na kuwasoma baadhi ya wanasiasa wakitishia kuwa watawataja wahusika
iwapo Serikali haitafanya hivyo, lakini akasema haoni sababu yoyote ya
mtu kusita katika kuokoa taifa dhidi ya wizi wa fedha za umma.
“Haiwezekani
kwa mwanasiasa yeyote katika nchi maskini kama Tanzania au kiongozi wa
Serikali kuwa na utajiri wa mabilioni ya fedha.”
Alisema hata
kama anafanya biashara, siyo rahisi kuwa na utajiri wa kiwango hicho
hasa ikizingatiwa kuwa hutumia muda mrefu kulitumikia taifa.
“Sisi tunaofanya kazi serikalini, tunatoka saa moja usiku. Sasa muda huo wa kufanya biashara ni saa ngapi?”
Tuhuma
hizo ziliibuka bungeni Jumatano iliyopita baada ya Kambi ya Upinzani
kudai kwamba nawafahamu wahusika wa ufisadi huo na kutishia kuwataja
ikiwa Serikali haitafanya hivyo.
Naibu Kiongozi wa Upinzani
Bungeni, Zitto Kabwe alipokuwa akiwasilisha hotuba ya kambi yake kuhusu
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Fedha alisema miongoni mwa
wanaomiliki fedha hizo ni kiongozi wa juu nchini pamoja na aliyepata
kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na Benjamin
Mkapa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba kuna
Watanzania 27, wakiwamo wanasiasa na wafanyabiashara walioficha
mabilioni ya fedha huko Uswisi, huku mmoja wao akiwa anamiliki Dola za
Marekani milioni 56 (sawa na Sh89.6 bilioni).
Katika uchunguzi
huo ilibainika pia kuwa kiasi cha fedha kilichothibitishwa kumilikiwa na
Watanzania hao ni jumla ya Dola za Marekani 186 milioni (takriban Sh300
bilioni) kwa viwango vya sasa vya kubadilishia fedha ambavyo ni Sh1,600
kwa Dola ya Marekani.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa mbali na
kigogo anayemiliki Sh90 bilioni, wapo wengine wanne huku anayefuatia
akiwa anamiliki Dola 30 milioni (Sh48 bilioni), mwingine dola 20 milioni
(Sh32 bilioni) na wengine wawili kila mmoja anamiliki dola milioni 10
(Sh16 bilioni).
Hiyo inamaanisha kwamba vigogo watano tu
katika kundi hilo, wanamiliki Dola milioni 126 (Sh201.6 bilioni) sawa na
asilimia 67.74 ya fedha hizo, wakati wengine 22 waliobaki wanamiliki
Dola milioni 60 (Sh96 bilioni) sawa na asilimia 32.25.
Kwa hesabu
za kawaida, kiasi cha Sh300 bilioni, kinaweza kugharimia ujenzi wa
vyumba vya madarasa zaidi ya 33,300, ikiwa chumba kimoja kinagharimu
kiasi cha Sh9 milioni.
Katika orodha ya walioweka fedha nchini
humo, pia wamo wafanyabiashara wanaomiliki kiasi cha dola kati ya
milioni mbili na milioni saba. Kadhalika, wamo wawili waliowahi kuwa
mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere
ambao akaunti zao zina kiasi kisichozidi Dola 500,000 kwa kila mmoja.
Chanzo: Mwananchi
Monday, August 20, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment