Wednesday, August 15, 2012

Zitto awa mbogo

Best Blogger Tips
 MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), ameitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA), kufanya uchunguzi wa manunuzi ya mafuta ya kuzalisha umeme ambayo yanagharimu sh bilioni 42 za serikali kila mwezi.

Zitto ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Fedha, alisema kuwa sakata la mjadala wa ununuzi wa rada haliwezi kuisha kwa kufurahia chenji iliyorudishwa kwani bado taifa linahitaji kujua ukweli.

Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo mjini hapa jana, Zitto alisema manunuzi ya mafuta yamejaa mizengwe ya ufisadi uliokithiri, na kwamba licha ya kutaka Spika kuunda tume ya kuchunguza ufisadi huo na Kamati ya Bunge kutaka uchunguzi wa kibunge kufanyika, hakuna hatua zilizochukuliwa.

“PPRA haipaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna sh bilioni 1.4 kila siku, na yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje, hivyo kupoteza fedha za kigeni hovyo,” alisema.

Aliongeza kuwa, Wizara ya Fedha ambayo ndiyo wizara mama ya PPRA ambayo pia inasimamia uchumi wa nchi, inapaswa kuleta bungeni taarifa ya uchunguzi utakaofanywa na PPRA kuhusu manunuzi hayo.

“Takwimu zinaonyesha kuwa serikali inapaswa kutumia zaidi ya sh 42 bilioni kila mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya umeme. Manunuzi yenyewe ya mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri. Kambi ya upinzani inataka uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha umeme, ambayo yanachoma bilioni 42 za serikali kila mwezi,” alisema.

Kuhusu sakata la ununuzi wa rada, Zitto, alisema mjadala huo bado ni mbichi, kwani unahitajika ukweli kuwa taifa lilipata hasara kiasi gani pamoja na hatua stahiki kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa taifa.

Alisema sehemu ya malipo ya deni la taifa ni mkopo wa serikali iliyochukua kununua rada kutoka Kampuni ya BAE ya Uingereza na kuongeza kuwa, suala hilo limejadiliwa kwa upande mmoja wa ufisadi wa kupandisha bei na hatimaye kurejeshwa kwa chenji hiyo.

Zitto, alisema kuwa hiyo ilikuwa nusu ya ukweli kuhusu suala la rada, kwani serikali ilikopa dola milioni 40 kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununua rada hiyo.

“Mkopo huo ulikuwa na riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na Benki ya Dunia au IMF. Kambi rasmi ya upinzani inataka kujua kama mkopo huo umeshalipwa, na jumla tulilipa kiasi gani. Na chenji ya rada ilikuwa na thamani yoyote kifedha?” alihoji.

Zitto pia aligusia suala la udhibiti wa fedha haramu, akisema kambi hiyo imepata taarifa kuwa mmoja wa viongozi wa juu nchini na baadhi ya mawaziri wa serikali za awamu zilizopita, ni miongoni mwa wamiliki wa fedha hizo zipatazo sh bilioni 314.5.

Alisema sehemu kubwa ya fedha hizo zililipwa kampuni ya utafutaji mafuta wa gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

“Tunaitaka serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua baada ya taarifa hiyo kutoka Benki ya Taifa ya Uswisi ilipotolewa. Tunataka kuliambia taifa hatua itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote ambazo zimefichwa ughaibuni. Kambi ya upinzani italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha katika benki ya Uswisi iwapo serikai haitatoa taarifa rasmi kuhusu suala hili,” alisema.

Hata hivyo msimamo huo wa Zitto, ulimwibua Mbunge wa Simanjiro, Christpher ole Sendeka (CCM), aliyeomba mwongozo na kumtaka Zitto awataje kwa majina viongozi hao, kwani kuacha hivyo ni kuharibu taswira ya serikali na Bunge.

Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lisu, aliingilia kati akisema Sendeka hakupaswa kumkatisha Zitto wakati akizungumza na kusema kuwa iwapo ana wasiwasi na kauli hiyo kwa mujibu wa kanuni anapaswa kuthibitisha maelezo anayoyaona hayana ukweli kabla ya mtoa kauli kuthibitisha.

Aidha, Zitto alisema kuna taarifa nyingine zinazoonesha jinsi taifa linavyoibiwa kupitia kesi mbalimbali ambazo serikali imeshitaki au kushitakiwa kwenye mahakama za kimataifa.

Alitoa mfano wa kesi hizo ni ya IPTL na Standard Chartered Bank ya Hong Kong ambayo imechukua muda mrefu bila kuisha na kuliingiza taifa katika hasara kubwa.

Kuhusu deni la taifa, Zitto alitaka ufanyike ukaguzi maalumu, ili kubaini uhalali wa deni hilo ambalo hadi Juni mwaka huu lilifikia dola milioni 10,354.6.

Alisema ukaguzi ukifanyika, utawezesha kujulikana kama miradi ilitekelezwa kama inavyotakiwa au kuna mazingira yenye utata.

Kuhusu mishahara hewa, Zitto alisema watumishi hewa 9,949 ni wengi na kwamba inaonesha ni jinsi gani serikaki haipo makini katika suala hilo.

Aliitaka serikali kutumia fedha wanazolipwa watumishi hewa kuwalipa walimu na madaktari kwani ni nyingi.

“Siku zote sababu za serikali kutotimiza matakwa ya wafanyakazi katika sekta ya afya na elimu ni kwamba haina fedha. Lakini tunashuhudia sh bilioni 70 kila mwaka zikielekezwa kuwalipa watumishi hewa,” alisema.

Kwa upande wa mashirika ya umma, alisema kambi hiyo inataka kupata maelezo kuhusu sakata la uuzwaji wa hisa za shirika la UDA pamoja na kuhoji serikali imefikia wapi katika pendekezo la kulifanyia marekebisho Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), ili liweze kumiliki, kusimamia na kuziendesha hisa za serikali katika kampuni binafsi ambao umiliki wa serikali ni chini ya asilimia 50.

Akisoma maoni ya Kamati ya Fedha na Uchumi, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dustan Kitandula (CCM), alisema kuna haja serikali ikadhibiti deni la taifa kabla halijaongezeka zaidi.

Kitandula ambaye ni mbunge wa Mkinga, alisema kuwa serikali inapaswa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wake waliohusika katika ubadhirifu wa ulipaji mishahara hewa.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits