MBIO za kuwania nafasi za uongozi wa juu wa Jumuiya za Chama cha
Mapinduzi (CCM), imeshika kasi huku taarifa zikionyesha kwamba kambi
zinazowania urais wa 2015 ndani ya chama hicho, kila moja inajipanga
kuhakikisha inaweka watu wake.
Wakati katika Umoja wa Wanawake
(UWT) hadi jana mchuano ulikuwa ukionyesha kuwa mkali kati ya Waziri wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Same
Mashariki, Anne Kilango Malecela hali ni tofauti kwa Umoja wa Vijana wa
chama hicho (UVCCM).
Hadi jana katika mbio za kuwania nafasi ndani
ya UVCCM, vijana wanne walikuwa wamechukua fomu kuwania nafasi ya
uenyekiti na wengine 16 wakiomba nafasi ya makamu mwenyekiti wa jumuiya
hiyo ngazi ya taifa huku Katibu Mkuu wa Umoja huo, Martine Shigella
akisema wanafahamu mikakati hiyo ya kambi za urais.
Kwa upande wa
UWT, Kilango anaonekana kusimama kundi la makada wa CCM wanaojipambanua
kupambana na ufisadi, huku Simba akiwa na kundi jingine tofauti na hilo
lakini, pia lenye malengo ya urais wa 2015.
Baadhi ya vyanzo vya
habari kutoka ndani ya CCM, vilisema mbali ya nafasi hiyo ya juu ya UWT,
kinyang’anyiro hicho pia kipo katika nafasi za wenyeviti wa mikoa.
Tayari
vita hiyo ya kambi za urais iko pia katika mikoa ambako kila kambi
inajipanga kuweka mtu wake, huku katika Mkoa wa Tabora vita ikitarajiwa
kuwa kali zaidi kati ya Margareth Sitta na mgombea wa kambi ya
watuhumiwa wa ufisadi.
UVCCM
Kwa upande wa
umoja huo wa vijana, kambi hizo zimekuwa zikiumana kuhakikisha kila moja
inaweka mtu wake katika nafasi ya uenyekiti, makamu na ujumbe wa Baraza
Kuu.
Hadi jana waliokuwa wakiwania nafasi za uenyekiti wa UVCCM
Taifa ambao tayari walikuwa wamerejesha fomu ni Thabit Jecha Kombo,
Sadifa Juma Khamis na Rashid Simai Msaraka.
Katika nafasi ya
Makamu Mwenyekiti ni Paul Makonda, Ally Salum Hapi na Agustino Matefu.
Makonda alirejesha jana na kuzungumza na waandishi akiahidi kupambana na
mafisadi.
Wanaowania nafasi za Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
Taifa (Nec), kupitia UVCCM ni Theresia Mtewele, Halima Bulembo, Olivia
Sanare, Ahmed Nyangani, Santo Tena, Vaileth Sambilwa, Faidha Salim na
Augustino Samwiya.
Katika nafasi za Ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa ni, David Mwakiposa, Mteweke Bulembo na Ester Mambali.
UVCCM
ni ngome muhimu kimkakati kutokana na kuwa na vijana wengi wanaoweza
kufanikisha ajenda mbalimbali ndani na nje ya vikao vya chama na
jumuiya.
Uchaguzi huo wa UVCCM unafanyika wakati, kiti cha
mwenyekiti kikiwa wazi tangu mwaka 2010 baada ya aliyekuwa mwenyekiti
wake, Yusuf Hamad Masauni kuong’olewa akituhumiwa kudanganya umri na
tangu wakati huo nafasi yake ilikuwa ikishikiliwa na Makamu wake, Beno
Malisa.
Taarifa ya Sekretarieti ya chama hicho iliyowasilishwa
katika kikao cha NEC mjini Dodoma mapema mwaka huu ilieleza kuwa makundi
ya urais 2015 ndiyo yanayosababisha mpasuko ndani ya chama hicho.
Shigella: Tunajua
Akizungumzia
mikakati hiyo ya vigogo wanaotaka urais kumwaga fedha ili kujiweka
mazingira mazuri ya kuwa na watu wao ndani ya UVCCM, Shigella alisema
wanajua mipango hiyo na kuonya kwamba kama kuna mgombea ambaye ametumwa
na genge la watu wanaotarajia kuwania urais 2015, ajue anapoteza muda
kwa sababu hatapitishwa.
Alisema jumuiya hiyo haijawahi kuwa na kiongozi aliyepandikizwa na mtu yoyote.
Alisema
watatumia njia mbalimbali kuwabaini watu wa aina hiyo, hasa kwa
kuitumia Kamati ya Usalama na Maadili ya jumuiya hiyo na kuwafanyia
usaili wagombea na kuangalia historia zao.
“Kwa hiyo, kama kuna
wanaowania nafasi za urais mwaka 2015 ambao wametuma vijana kutafuta
nafasi UVCCM wafahamu kuwa hawatafanikiwa kwa kuwa tumejiandaa
kukabiliana nao,” alisema Shigela.
Makonda na ufisadi
Kwa
upande wake Makonda ambaye jana alikuwa wa mwisho kurejesha fomu kwa
wiki iliyoisha jana, aliwaambia waandishi wa habari kuwa tatizo la
rushwa na ufisadi kwa baadhi ya watu ndani ya UVCCM ndilo lililomsukuma
kuwania nafasi hiyo.
Alisema historia ya UVCCM kutoka Tanu Youth
League imejengeka katika misingi ya uadilifu na uzalendo, lakini katika
siku za karibuni kumekuwa na baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi ambao
wamekuwa wakibomoa misingi hiyo na kujenga ya kwao ya kifisadi.
“Hii
ndiyo changamoto ambayo imenifanya nijitose katika kinyanganyiro hiki,
si vizuri kuhama chama kikiwa na matatizo. Njia sahihi ni kutafuta
uongozi ili kukabiliana nayo. Tukiwa na viongozi bora tutakuwa na
uchungu wa namna ya kutatua matatizo ya vijana, kama uchumi na hata
mikakati ya ajira,” alisema.
Alisema wakati rushwa ilitajwa kama
adui wa haki katika moja ya ahadi 10 za Mwana-TANU, sasa hivi imekuwa
ikitumika kama haki ya kupata uongozi hivyo vijana wanyonge wasiokuwa na
fedha za kutoa rushwa kukosa nafasi za kuongoza.
Nape: Tumejipanga
Katibu
wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye alisema
hafahamu kama kuna vijana wanaowania nafasi mbalimbali kwa lengo la
kuwasaidia vigogo kwenye mbio za urais mwaka 2015.
“Ndiyo kwanza
unaniambia, sina habari hizo. Katika CCM tunachoangalia ni kwamba
wanaowania nafasi hizo ni kutojihusisha na rushwa vinginevyo hawatakuwa
na sifa za kuchaguliwa,” alisema Nape.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, August 5, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment