MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka
amerejea nchini jana akitokea Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa na
kulakiwa na mamia ya watu huku akisema haogopi lolote na yupo tayari kwa
kazi.
Dk Ulimboka aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius
Nyerere saa 8.15 mchana kwa ndege ya Shirika la South African Airways.
Baada
ya kumaliza taratibu zote uwanjani na kutoka nje, Dk Ulimboka alilakiwa
na umati mkubwa wa wananchi wakiwemo madaktari na wanaharakati ambao
walijaza karibu eneo kubwa la lango la abiria wanaowasili jambo
lililoonekana dhahiri kumsisimua kiasi hadi kufikia kububujikwa wa
machozi.
Dk Ulimboka ambaye alipelekwa Afrika Kusini akiwa hawezi
kutembea wala kula mwenyewe baada ya Juni 27 mwaka huu kutekwa na watu
wasiojulikana, kupigwa na kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili, kisha
kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam,
amerejea akiwa anatembea na mwenye afya njema.
Akizungumza uwanjani hapo, Dk Ulimboka alisema: “Nawashukuru
Watanzania kwa kuniombea, nawashukuru madaktari wenzangu, ndugu na jamaa
zangu kwa kunisaidia kupata matibabu hadi leo hii narudi nyumbani
nikitembea mwenyewe. Hivi sasa niko fiti na niko tayari kwa kazi
yoyote.”
Uwanja huo ulikuwa umefurika mamia ya wananchi wakiwemo
madaktari ambao walikuwa na shauku ya kumwona Dk Ulimboka, lakini wengi
hawakufanikiwa kumwona.
Wingi wa watu ulisababisha kutokea kwa
msuguano kati ya madaktari na waandishi wa habari. Wakati wanahabari
wakitaka kumwuliza maswali Dk Ulimboka, baadhi ya madaktari walikuwa
wakimzuia Dk Ulimboka kujibu maswali licha ya mwenyewe kuonekana kuwa
tayari kuulizwa.
Baadhi yao walifikia hatua ya kushika kamera za
waandishi huku wengine wakisema... “Mwacheni akapumzike bwana, kwa nini
mnamsumbua sumbua.”
Baadhi ya madaktari hao walifikia hatua ya
kutumia nguvu dhidi ya wapiga picha wa magazeti na televisheni na hivyo
kusababisha vurugu na kelele nyingi katika eneo hilo.
Muda wote
wakati Dk Ulimboka akielekea kwenye gari akiwa na maua mkononi
aliyokadhibiwa baada ya kuwasili uwanjani hapo, madaktari hao walikuwa
wakiimba nyimbo za kuhamasishana ukiwamo Wimbo wa Taifa huku wengine
wakisema: “Mtakufa nyie, lakini si Dk Ulimboka.”
Baada ya kupanda
gari aina ya Nissan Patrol nyeusi, madaktari hao na wanaharakati na
wananchi wengine wakiongozwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi
wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananileya Nkya walilisukuma gari
hilo hadi katika lango la kutokea katika uwanja huo.
Wanaharakati
Mbali na Nkya, kulikuwa na idadi
kubwa ya wanaharakati wengine wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mtandao wa
Jinsia Tanzania (TGNP, Usu Malya.
Wanaharakati hao walikuwa na
mabango yaliyoandikwa, “Dk Ulimboka karibu nyumbani uliumizwa kikatili
ukitetea afya bora kwa Watanzania.”
Bango jingine lilisomeka: “Dk Ulimboka damu yako ilimwagika na kuamsha ari kwa wananchi kudai za afya.”
Jingine, “Dk Ulimboka wewe ni mpigania haki ya afya bora kwa wananchi wote Mungu na Watanzania wote tuko nawe.”
Malya
akizungumza uwanjani hapo alisema kupona kwa Dk Ulimboka na kurejea
nchini ni uthibitisho kwamba Mungu amesikia sauti za wanyonge.
“Dk
Ulimboka alisimamia haki za madaktari na za Watanzania wote akitaka
huduma bora zipatikane kwenye hospitali za umma kwa ajili ya Watanzania
wote,” alisema.
Mkurugenzi wa Tamwa, Nkya alisema amefurahi
kumpokea Dk Ulimboka akiwa hai kwa sababu hali yake ilikuwa mbaya wakati
akipelekwa kwa matibabu nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu wa
Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema kurejea kwa Dk Ulimboka
akiwa amepona kunathibitisha kwamba nchi za wenzetu kuna vifaa vya tiba
za kisasa na dawa.
“Kurejea kwa Dk Ulimboka ni mapenzi ya Mungu,
huu ni uthibitisho kuwa hapa nchini hakuna vifaa tiba na dawa zinazoweza
kusaidia wananchi kama ilivyo kwa wenzetu,” alisema Dk Chitage na
kuongeza:
“Madaktari tumefarijika na hii imetupa nguvu licha ya
vitisho tunavyopata tutaendelea kupigania haki zetu, haya ni mapambano
ya muda mrefu, ”alisema.
Dk Chitage alisema kupona na kurejea
nchini kwa Dk Ulimboka ni uthibitisho kuwa watu wengi wasio na uwezo
wanapoteza maisha kutokana na kukosekana kwa vifaa tiba na dawa hapa
nchini... “Madaktari tupo, lakini tatizo ni vifaa na dawa, hiki ndicho
tunachopigania ni haki wananchi kupata huduma za afya nchini.”
Katibu
Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila
alisema kurejea kwa Dk Ulimboka kutasaidia kuwatambua watu waliohusika
katika tukio la kumteka, kumpiga na kumtupa katika Msitu wa Pande.
“Sisi
tumefurahi sana, Dk Ulimboka alisimamia haki za madaktari na sekta ya
afya kwa ujumla, kurudi kwake kunatupa nguvu ya kuendelea kudai haki za
madaktari na wananchi,” alisema.
Dk Ulimboka anarejea nchini huku Serikali na madaktari wakiwa hawajafikia mwafaka kuhusu madai yao.
Madai
ya madaktari hao ni hali bora ya mazingira ya utoaji afya nchini,
ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu,
posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa
kazini.
Safari ya Dk Ulimboka kwenda kwenye matibabu nchini
Afrika Kusini ilitawaliwa na usiri mkubwa alipoondoka nchini Juni 31
mwaka huu, akisindikizwa na Dk Pascal Lugajo na kaka yake, Dk Hobakile
Ulimboka na mke wake, Dk Judith Mzovela.
Kutekwa
Dk
Ulimboka alitekwa na kufanyiwa vitendi vya ukatili wakati akiratibu
mgomo wa madaktari uliokuwa ukiendelea na aliokotwa na msamaria mwema
akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya.
Kutokana
na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu waliituhumu Serikali
kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana na kuliagiza Jeshi la
Polisi kuwasaka waliohusika.
Akisimulia mkasa huo Dk Ulimboka
alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Juni 27 katika Klabu ya
Leaders, Dar es Salaam alikokuwa na daktari mwenzake na mtu mwingine
aliyekuwa amemwita hapo (Leaders).
“Mara, katikati ya maongezi
tukaona huyo mtu aliyeniita anaongea na simu. Ghafla tukiwa tunasema
tuagane, wakaja watu kama watano hivi na bunduki, wakasema wewe na yule
bwana mko free (huru), tunakuchukua wewe (Dk. Ulimboka). Sijakaa sawa,
nikaona nimeshaburutwa nikaanguka kwenye lami, wakaniinua na kuniingiza
kwenye gari nyeusi, lakini ilikuwa haina namba.”
Wakati Dk
Ulimboka alipokuwa akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya
Kikwete alisema Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa
kuwa alikuwa kiungo muhimu katika majadiliano baina ya Serikali na
madaktari.
Rais Kikwete alisema hayo katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
“Dk
Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na
madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo
hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya.
Kulikuwa na rai ya kutaka
asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa
anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na
Serikali,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk
Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama
na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.
Kauli ya Rais
Kikwete kuhusu mgomo wa madaktari inafanana na ile iliyokuwa imetolewa
awali na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisema wanatambua kuwa Serikali
nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa shaka kuhusu kilichomtokea Dk
Ulimboka, lakini ameshangazwa na hisia hizo akisema haoni sababu ya
Serikali kufanya hivyo.
Dk Ulimboka alisafirishwa kwenda Afrika
Kusini Juni 31, mwaka huu kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi baada ya
jopo la madaktari waliokuwa wakimhudumia, kueleza mabadiliko ya hali ya
afya yake, yaliyosababisha figo kushindwa kufanya kazi.
Ulinzi nyumbani
Nyumbani kwao, eneo la Ubungo Kibangu kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa nje ya nyumba huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Vijana
wasiopungua watatu wakiwa wamevaa kawaida walikuwa wamekaa jirani na
lango la kuingilia wakiratibu nyendo za wanaopita na wanaotaka kuingia
katika nyumba hiyo iliyopo karibu na Shule ya Msingi Ubungo Kibangu.
“Watu
walikuwa wengi hapa lakini wametakiwa kuondoka ili kutoa nafasi kwa
dokta kupumzika na hakuna ambaye anaruhusiwa kuingia kwa sasa labda kama
ni daktari mwenzao,” alisema kijana mmoja anayeishi jirani.
Awali,
mama mmoja ambaye alifahamika kama ndugu wa familia hiyo anayeishi
karibu na nyumba ya Dk Ulimboka alipoulizwa nyumbani kwa kiongozi huyo
wa madaktari alihoji anatafutwa na nani na hata mwandishi
walipojitambulisha alimtaka aondoke na kurejea alikotoka.
“Baba
wewe nenda nyumbani kwako tu, usitake kujua zaidi,” alisema mama huyo
majibu ambayo yalionekana kufanana na ya majirani wengi wa daktari huyo.
Chanzo: Mwananchi
Monday, August 13, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment