Sunday, July 1, 2012

Alhaji Mwinyi: Mengi ana sifa kama za Mtume

Best Blogger Tips
 Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, amesema Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP Limited, Dk Reginald Mengi, ana sifa za kuitumikia jamii kama alivyokuwa Mtume Mohammed S.A W.

Amesema Mtume Mohamed S.A W alikuwa na sifa za kuwapenda na kuwashughulikia masikini na kuwasaidia wahitaji pasipo kujali tofauti zao.

“Umekuwa mstari wa mbele kuwasaidia masikini lakini hasa wenye ulemavu, unachanganyika na kula nao, hauwakimbii, unawaheshimu na kuumizwa na mapungufu ya maumbile yao, hauwabezi, hauwadharu,” Alhaj Mwinyi alisema.

Alhaj Mwinyi alisema hayo jana akihutubia kwenye hafla ya kumtunuku Dk Mengi, Tuzo ya Iliyotukuka ya Huduma kwa Jamii, iliyotolewa na Kamati ya Amani ya Viongozi Mkoa wa Dar es Salaam.
“Sifa hizo ndizo alikuwa Mtume Mohamed S.A W ambaye umma wa Waislamu unamheshimu,” alisema Alhaj Mwinyi ambaye hivi sasa ana miaka 87.

Aliongeza, “Waislamu wanavutiwa sana kwa tabia zako ndio maana tumeamua kukushukuru hadharani… tunamuomba Mwenyezi Mungu akuzidishie neema na rehema zake, akukinge na maadui na kukupa heri na fanaka.”

Alhaj Mwinyi alisema kutokana na hali hiyo, Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini iliamua kumtunukia zawadi ya dua ambayo haiwezi kushikwa ama kufanyiwa mzaha na binadamu yeyote, kwa maana matokeo yake yanatoka kwa Mungu.

 Mwenyekiti wa kamati hiyo, Alhad Mussa Salum, alisema hatua ya kumtunuku Dk Mengi tuzo hiyo, ilitokana na kujiridhisha na jitihada za Dk Mengi kwamba anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa kwa michago yake kwenye jamii.

Salum alisema ukarimu wa Dk Mengi unamuwezesha kuitazama jamii pana zikiwemo taasisi za dini ambapo ameshashiriki kuichangia misikiti, makanisa na madrasa.

Alisema pamoja na kutambua uzito wa tuzo hiyo kuwa dua kama ilivyoelezwa na Alhaj Mwinyi, viongozi hao walikutana juzi na kuamua kutoa tuzo ambayo Alhaj Mwinyi alimkabidhi Dk Mengi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Dk Mengi alisema tukio hilo linapaswa kuwagusa watu wenye uwezo wanaofanya matendo ya huruma na kuwasaidia wahitaji.

Aliifananisha jamii ya watu wenye uwezo kiuchumi kuwa sawa na bomba la maji linalotumika kusafirisha bidhaa hiyo ili iufikie umma.

“Kama una uwezo kiuchumi ujue kwamba Mwenyezi Mungu amekuteua uwe kama bomba, ili hayo unayoyapata ukagawane na wasiokuwa na uwezo huo,” alisema.

Pia Dk Mengi alisema binafsi anatumia muda mwingi kufikiria na kutamani kama angeweza kuutokemeza umasikini na upungufu mwingine ili watu wanaoishi maisha magumu na yenye mateso wakombolewe na kuishi maisha bora.

Dk Mengi alisema nia ya kutokomeza umasikini nchini inapaswa iambatane na ukweli wa mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu na utendaji usioridhisha wa viongozi wa umma.

“Haya yote ni baadhi ya vyanzo vikubwa vya umasikini na hali ngumu ya maisha kwa wananchi,” alisema.
Alisema wananchi wana imani na serikali ya Rais Jakaya Kikwete hasa kwa kuwachukulia hatua waliokuwa mawaziri, wakatajwa bungeni kwa ubadhirifu tofauti kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Dk Mengi alimpongeza Alhaji Mwinyi kwa jitihada zake zilizochochea umoja na mshikamano nchini, huku akifungua milango iliyofanikisha kukua kwa uchumi.

“Mwinyi ni mnyenyekevu asiyebagua yeyote na amekuwa ni rafiki wa kweli tangu akiwa kwenye madaraka ya urais na baada ya kustaafu,” alisema.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits