SIKU moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo,
William Mhando, na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi
mabaya ya madaraka, siri nzito imefichuka kuwa ni janja za serikali
kutaka kuficha udhaifu na uzembe wake katika kuliwezesha shirika hilo.
Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Robert Shemhilu, Ofisa
Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun
Matambo, walisimamishwa na bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jeneralai
mstaafu, Robert Mboma ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Hata hivyo Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkurugenzi huyo ametolewa
kafara kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri kiutendaji na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, lakini na vilevile
katibu mkuu huyo anatumia udhaifu wa serikali kwa TANESCO kumwadhibu ili
kuepusha mjadala mzito wakati hotuba ya bajeti yao itakaposomwa bungeni
hivi karibuni.
Inasemekana sababu inayotolewa na Katibu Mkuu ni kwamba Mhando
alimdharau kwa kutompa taarifa kabla ya TANESCO kutangaza mgawo wa umeme
wa hivi karibuni. Kwa mantiki hiyo, akamlima Mhando barua akisema
anahujumu shirika. Hata hivyo, wananchi na watumishi wa TANESCO wanajua
kuwa anayehujumu TANESCO ni serikali, ambayo inalinyima shirika hilo
pesa ilizoahidi kwa ajili ya miradi ya uzalishaji na usambazaji wa
umeme, na kulizuia shirika hilo kuuza umeme kwa faida, kwa sababu za
kisiasa.
Inasemekana hatua dhidi ya Mhando inatokana na woga wa waziri na
katibu mkuu juu ya mjadala mkali unaotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa
kujadili bajeti ya wizara yao. Mhando anatolewa kafara kisiasa, lakini
taarifa zinasema naye amejibu barua ya katibu mkuu kueleza jinsi
asivyohujumu shirika hilo. Habari zaidi baadaye.
Katika barua ya Maswi kwa Mhando yenye Kumb.Na. SAB. 270/ 286/01/2 ya
Julai 12, mwaka huu, anasema: “Nimesikitishwa na kitendo chako cha
kuanza mgawo wa umeme bila kupata kibali cha maandishi kutoka kwangu
kama nilivyokueleza katika barua yangu niliyoambatanisha.”
Maswi anaongeza: “Hiyo siyo tu ni dharau bali inaonyesha kuwa mgawo
huo wa umeme unafanywa kwa makusudi kwa lengo la kuihujumu serikali.
Aidha, ukiwa kama kiongozi mkuu wa shirika, unaonekana umeshindwa
kutekeleza majukumu yako ya kusimamia shughuli za shirika inavyostahili.
“Kwa barua hii unipe maelezo kwa nini uliamua mwenyewe kuanza mgawo wa
umeme bila kunifahamisha kama inavyotarajiwa, kwa makusudi kabisa
uliamua kuanzisha mgawo mikoa yote bila sababu ya msingi ilhali ukijua
ni wakati wa Bunge na ili serikali ishambuliwe,” ilisomeka barua hiyo.
Hata hivyo, katika barua yake ya utetezi Mhando anakataa kuhusika na
hujuma huku akieleza bayana kile kilichotokea hadi kusababisha mgawo na
kwamba hata Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi alipewa taarifa juu ya
tatizo hilo.
“Taarifa hii nilimpa pia mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika.
Hali hii ilijitokeza kutokana na ukweli kwamba vituo vya kuzalisha
umeme vya IPTL na Symbion Dodoma havikuwa na mafuta ya kutosha kuzalisha
umeme, na vile vile kulikuwa na upungufu wa gesi asili katika vito vya
TANESCO,” alisema Mhando katika barua yake.
Anakataa kuwa hajashindwa kufanya kazi yake hiyo licha ya kuifanya
kwenye mazingira yenye changamoto kubwa. “Serikali ingeidhamini TANESCO
kupata mkopo wa sh bilioni 408 mapema iwezekanavyo, kuondoa kodi kwenye
mafuta yanayotumika kufua umeme na kupata ruzuku ya sh bilioni 80 toka
serikalini ifikapo Julai mwaka huu matatizo ya umeme yangelikuwa
historia!”
Mhando anaweka wazi kuwa mkopo huo wa sh bilioni 408 ambao ulitegemewa
kupatikana mapema tangu mwishoni mwa 2011 mpaka sasa haujapatikana
kutokana na ucheleweshaji wa dhamana ya serikali na msamaha wa kodi
kwenye mafuta yanayotumika kufua umeme pamoja na ruzuku ya sh bilioni 80
toka serikalini haijapatikana kama ilivyoahidiwa.
Ni katika mazingira hayo wadadisi wa mambo wanaona kama serikali
inataka kufunika kombe la kushindwa kutimiza wajibu wake kwa shirika
hilo na hivyo kumbebesha lawama Mahando ili isiadhibiwe na wabunge.
Kufuatia utata huo wa kusimamishwa kwa vigogo hao, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe
Zitto, aliliambia gazeti hili jana kuwa wameita kikao cha kamati na
kuiita bodi ya TANESCO ili ijieleze na vile vile watakuwepo Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali, Ludovic Uttoh na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma
(PPRA).
“Nitatoa taarifa baada ya kikao. Tunataka uwajibikaji lakini hatutaki
uonevu, nimeagiza mwenyekiti wa bodi ya TANESCO aje kujieleza kwenye
kamati kuhusu tuhuma hizo,” alisema Zitto.
Naye waziri kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alisema kuwa
kusimamishwa kwa Mhando na watendaji wengine wa shirika hilo ni mbinu ya
serikali ya kuficha udhaifu na uzembe unaoikabili.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema hali
hiyo inachagizwa na suala zima la ufisadi hali inayotishia nchi kurudi
katika mgawo wa umeme kama inavyodhihirika hivi sasa.
Alisema taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa
umeme zimekuwa zikijadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya wizara hiyo
hata baraza la mawaziri bila kuchukuliwa hatua muafaka.
“Hii ni kauli rasmi kama waziri kivuli kitendo cha kumsimamisha Mhando
na wenzake ni kumtoa kafara ya kuficha udhaifu na uzembe wa serikali
juu ya tishio hili la nchi kurejea katika mgawo,” ilisema sehemu ya
taarifa hiyo.
Aliitaka serikali kutoa kauli ya kwa nini waziri na naibu wake walitoa
taarifa potofu bungeni kuwa hakuna tishio la mgawo wa umeme, na juu ya
mkakati wao aliouita ni dhaifu waliokuwa wakiufanya kupunguza mgawo
katika kipindi cha Bunge ili kuficha udhaifu na uzembe uliokithiri.
Chanzo: Tanzania Daima
Monday, July 16, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment