MKURUGENZI Mkuu Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
Mhandisi William Mhando amesimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi ya
shirika hilo kuanzia jana.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya
Wakurugenzi na kusainiwa na Mwenyekiti wake, Jenerali Mstaafu Robert
Mboma, Mhando amesimamishwa kazi pamoja na watendaji wakuu wengine wa
Tanesco ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya
ya madaraka.
Viongozi wengine wa Tanesco waliosimamishwa kazi
ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa
Mkuu wa Fedha Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi Harun
Mattambo.
Hata hivyo, Mhando alisema kupitia Shirika la Utangazaji
Tanzania (TBC 1) jana kuwa hana taarifa zozote kuhusiana na kusimamishwa
kwake.
Ingawa taarifa hiyo ya Mboma haikueleza nani anakaimu
nafasi iliyoachwa wazi na Mhando, lakini habari tulizopata kutoka vyanzo
vyetu ndani ya Wizara ya Nishati na Madini na Tanesco zinasema Kaimu
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji atakuwa Felschami Mramba ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Masoko na Usambazaji wa Tanesco.
Hatua hiyo
imetangazwa jana jijini Dar es Salaam kufuatia kikao cha dharura cha
Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco kilichofanyika Julai 13 mwaka huu,
ambacho kilijadili tuhuma mbalimbali dhidi ya menejimenti ya Tanesco.
Taarifa hiyo fupi imeeleza kuwa tuhuma dhidi ya Mhandisi Mhando ni nzito hivyo ni vyema zifanyiwe uchunguzi huru na wa kina.
“Hivyo,
Bodi iliazimia pamoja na mambo mengine kama ifuatavyo: Uchunguzi wa
tuhuma hizo uanze mara moja kwa kutumia uchunguzi huru na kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi William Mhando ili kupisha
uchunguzi huo na kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kazi nchini,”
inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mboma alibainisha bodi yake kufanya
kikao kingine cha dharura jana Julai 14, na kuamua kuwasimamisha kazi
watendaji hao mara moja ili kupisha uchunguzi huo.
“Pamoja na
uamuzi huo, Bodi imechukua hatua stahiki za kuhakikisha kwamba shughuli
za utendaji na uendeshaji wa Tanesco zinaendelea kama kawaida,” imesema
taarifa hiyo.
Awali saa 11 jioni jana waandishi wa habari
walijazana katika Ofisi ya Wizara ya Nishati na Madini iliyopo Mtaa wa
Ohio, ambapo hawakufanikiwa kuwaona wakurugenzi hao waliokuwa kwenye
kikao huku wakitakiwa kuondoka eneo hilo na kusubiri kwa mbali.
Waandishi
hao walilazimika kusubiri kwa takriban saa nzima ndipo alipotokea Ofisa
Habari wa Wizara ya Nishati na Madini aliyetambuliwa kwa jina la
Fadhili Kileo na kugawa nakala ya taarifa ya kikao hicho huku
wakurugenzi hao wakipanda magari yao na kuondoka bila ya kuzungumza na
waandishi hao hali iliyowakera waandishi.
“Jamani naomba
mtusamehe sana, hii siyo kawaida yetu, imekuwa ni dharura tu ndiyo maana
mnaona wakurugenzi wanaondoka,” alisema Kileo akiwasihi waandishi wa
habari waliokuwa wakilalamika.
Wakati hayo yakiendelea, Katibu Mkuu
wa wizara hiyo, Eliakim Maswi naye alikataa kuzungumza na waandishi wa
habari akisema kuwa hahusiki.
“Hapana mimi sihusiki, nendeni kwa hao viongozi waliokuwa kwenye kikao,” alisema Maswi.
Mhando aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Tanesco kuanzia tarehe 1 Juni, 2010.
Baada ya uteuzi huo, Mhando alisema atahakikisha wateja wote wa Tanesco wanakuwa na mita za Luku.
Kabla ya uteuzi huo, Mhando alikuwa ni Meneja Mkuu Usambazaji Umeme na Masoko katika shirika hilo.
Mhando alichukua nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Dk Idris Rashid ambaye alimaliza muda wake wa uongozi.
Wasifu wa Mhando
Mhando
aliajiriwa na Tanesco mwezi Oktoba mwaka 1987 kama Mhandisi wa Umeme na
baadaye alipandishwa na kuwa Mhandisi katika njia za umeme. Mwaka 1990
hadi 1992 aliteuliwa kuwa Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida.
Mwaka
1992 hadi 1994 alikuwa Meneja wa Mkoa wa Tanesco, Mkoa wa Mbeya.
Alipandishwa cheo mwaka 1995 na kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Kusini
Magharibi hadi mwaka 1999.
Ana elimu ya Shahada ya Uzamili
(Masters) katika masuala ya umeme aliyoipata mjini Havana nchini Cuba
mwaka 1987, pamoja na mafunzo mengine aliyoyapata katika vyuo mbalimbali
ndani na nje ya nchi.
Kwa muda mrefu Tanesco imekuwa katika
matatizo mbalimbali ya kiutendaji na utoaji huduma yaliyosababisha taifa
kuingia katika mgawo wa umeme na kudhoofisha maendeleo na ukuaji wa
uchumi.
Matatizo hayo ni pamoja na uchakavu wa mitambo ya Tanesco, hujuma za miundombinu na kuingiwa kwa mikataba mibovu.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wa kutoa ufafanuzi juu ya
taarifa iliyotolewa na Kamati ya Hesabu za Mashirika ya
Umma(POAC), kuwa kuna ubadhirifu ndani ya Tanesco Mei 7, mwaka huu,
Mhando alisema ikigundulika kuna ubadhirifu wowote uliofanyika katika
shirika hilo kutokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali(CAG) basi atakuwa tayari kujiuzulu.
Taarifa ya POAC
ilisema shirika hilo lilifanya ununuzi wa kati ya Sh300 bilioni hadi
Sh600 bilioni lakini Mhando alisema kuwa si kweli.
"Kama nimekosea niko
tayari kujiuzulu na mwajiri akiamua kunihamisha sina tatizo na
ninawaambia mimi sina miaka miwili kazini na shirika linapata hati safi
hilo mwelewe na mliseme," alisema Mhando.
Chanzo: Mwananchi
Saturday, July 14, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment