MANISPAA ya Temeke imetoa orodha ya majina ya wananchi waliopewa viwanja
katika manispaa hiyo, ambayo inaonyesha kuwamo kwa vigogo wanaojumuisha
mawaziri, wabunge, watendaji wakuu wa Serikali pamoja na baadhi ya
watoto wa vigogo hao.Katika orodha hiyo, jumla ya watu 1,800 walipatiwa
viwanja hivyo, huku majina hayo ya vigogo yakiwa ni zaidi ya 50, ambao
baadhi wamejiandikisha wenyewe, wengine wake zao, ndugu na watoto wao.
Majina
hayo ambayo gazeti hili iliyaona jana, yamebandikwa kwenye ubao wa
matangazo wa manispaa hiyo, ili wananchi walioomba viwanja hivyo waweze
kuangalia kama wamo katika orodha ya waliopatiwa viwanja hivyo.
Baadhi
ya wananchi waliofika kusoma majina hayo walisikika wakilalamikia hali
hiyo, huku wakisema kuwa kinachoonekana ni vigogo kupendelewa na
kuwanyima wananchi wa kawaida.
Katika orodha hiyo, majina
yanayosomeka ni pamoja na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama; Naibu
Spika, Job Ndugai; Waziri wa Mawasiliano, Sanyansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mnyaa Mbarawa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Pereira Ame Silima.
Kwa upande wa Makatibu Wakuu wa Wizara wapo,
Dk Florence Turuka (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, Ramadhan Kijjah; Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi,
Omary Chambo na Dk Idris Rashid ambaye ni Gavana wa Zamani wa Benki Kuu
ya Tanzania (BoT).
Pia wamo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk
Didas Masaburi, Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Slaa; Kamishna wa
Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja na Kamanda wa
Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleinan Kova.
Wengine ni
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura),
Haruna Masebu; Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
Ludovick Utouh na Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili(MNH),Marina Njelekela.
Kwa upande wa wabunge wamo Dk
Augustine Mrema (Vunjo - TLP), Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo
Filikunjombe; Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Sylvester Koka; Mbunge wa
Kinondoni (CCM), Idd Azzan; Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Dk Cyril
Chami na Mbunge wa Singida Kusini (CCM), Mohamed Misanga.
Wengine
ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila; Mbunge wa
Igunga (CCM), Dk Peter Kafumu na Mbunge wa Bukene (CCM), Seleman Zedi.
Wabunge
wa Viti Maalumu (Chadema), Maulida Komu na Suzan Lyimo, Viti Maalumu
CCM, Dk Mary Mwanjelwa na Zakhia Meghji ambaye ni mbunge wa kuteuliwa.
Orodha
hiyo pia inaonyesha majina ya ukoo yanayofanana na majina ya baadhi ya
viongozi ambao ni Miraji Kikwete, Khalfan Kikwete, Juanita Mramba,
Suzan Mkapa, Zainab Mkomwa, George Rupia, Maimuna Mfutakamba, Mary
Membe, Pharles Ngeleja, Judith Kahama na Wilfred Mwanri.
Mkurugenzi apatwa kigugumizi
Mkurugenzi
wa Manispaa hiyo, Magreth Nyalile alipoulizwa kuhusu orodha hiyo
alisema kuwa, majina hayo hajayaona na kwamba waliobandika wamefanya
uamuzi huo bila ya yeye kuupitia.
“Majina yenyewe sijayaona,
hivyo basi siwezi kujua ni kina nani waliopewa viwanja hivyo, kwa sababu
wako zaidi ya 1,000, jambo ambalo litakuwa vigumu kwangu kubaini tatizo
hilo,” alisema Nyalile.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo
hawezi kusema lolote kwa sababu yuko nje ya ofisi kwa ajili ya shughuli
nyingine za ujenzi wa taifa.
Hata hivyo, Nyalile alisema mchakato
wa ugawaji wa viwanja hivyo ulifuata taratibu za kisheria na kwamba
hakuna mtu au kiongozi yeyote aliyependelewa, jambo ambalo linaweza
kusababisha mgongano wa hapa na pale.
Nyalile alisema kuwa kama
kuna viongozi walipewa kwa njia zisizo sahihi, au kwa rushwa wakati wa
uwasilishaji wa majina hayo, walipaswa kutoa taarifa kwa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili waweze kuchukuliwa hatua
za kisheria.
Wananchi walalama
Baadhi ya wananchi walikuwa
wakiangalia majina hayo katika ubao huo walidai kuwa, baadhi ya maofisa
wa halmashauri hiyo wamedaiwa kupewa rushwa wakati wa ugawaji wa
viwanja hivyo.
“Walitangaza kama kiini macho, lakini tayari
walikuwa na majina yao ili waweze kuwapatia na jambo ambalo
limejionyesha wazi kwenye majina ya watu waliopewa viwanja hivyo,”
alisema mwananchi mmoja (jina tunalihifadhi) na kuongeza:
“Kutokana
na hali hii, hatuna imani na viongozi wowote wa Serikali kwa sababu
inaonyesha wazi kuwa, kila mmoja anaangalia masilahi yake na si wananchi
wasio na kipato”.
Aliongeza kuwa, wananchi hawana imani na
viongozi wao, hivyo Serikali inapaswa kuingilia kati kwa sababu hali
hiyo inaweza kusababisha matatizo.
Mwananchi mwingine aliyekuwa
akifuatilia jina lake alisema: “Wewe unachokiona ni nini hapo kama siyo
yaleyale ya ubinafsi! Wewe unaamini kabisa kwamba kweli hawa viongozi
wetu hawana nyumba au hawana viwanja hapa Dar es Salaam.
Aliongeza:
”Kama manispaa walitangaza viwanja ili wajiuzie wangesema tu badala ya
kuchukua fedha zetu Sh30,000 halafu viwanja wakajigawia wenyewe.”
Mgawo wa Viwanja
Mapema
mwezi Juni mwaka huu, Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ilitangaza
kwamba imepima viwanja 1,800 katika eneo la Gezaulole ikiwa ni
mwendelezo wa utekelezaji wa Mradi wa Upimaji Viwanja.
Fomu za
maombi ya kununua viwanja hivyo zilianza kutolewa Juni 11 na kila
mwombaji alipaswa kulipia ada ya maombi ya kiasi cha Sh30,000 katika
ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke iliyopo mkabala na Uwanja
Taifa jijini Dar es Salaam.
“Fedha hizo hazitarejeshwa na
mwombaji atajaza nakala mbili za fomu ya maombi na kuzirejesha zikiwa
zimebandikwa picha 3 za ukubwa wa pasipoti. Mwisho wa kurudisha fomu
hizo ni tarehe 18.06.2012 saa 8 mchana,” linasomeka tangazo rasmi la
manispaa hiyo.
Wakazi wenye nyumba na mashamba ndani ya eneo la
mradi ambao walikuwa wametambuliwa kabla ya zoezi la upimaji kuanza, pia
walitakiwa kununua fomu za maombi kwa utaratibu uleule.
Chanzo: Mwananchi
Wednesday, July 25, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment