NIMEKUWA nikisema kwamba tunahitaji kukua, na katika kukua tutende
na tuenende kama watu wazima wasiohitaji ulezi wa karibu wa baba mkali
wala uangalizi wa yaya.
Nimejaribu kuonyesha kwamba ingawaje mwanzoni mwa maisha yetu kama
Taifa tulihitaji baba mkali wa kutuelekeza katika hatua zetu za mwanzo
za kukua, hivi sasa hatumhitaji tena. Tunatakiwa tujitegemee,
tujielekeze kama jamii iliyokomaa na ambayo hainyonyi dole-gumba tena.
Kwa bahati mbaya, bado tunazo dalili nyingi mno za jamii inayonyonya
dole-gumba, jamii iliyoshindwa kukua na kukomaa, jamii changa ambayo
uchanga wake ni wa tabia zisizofanana na wingi wa miaka ya umri wake.
Katika mambo mengi ni jamii iliyovia.
Kinachotia hofu zaidi, kwa mtazamo wangu, ni kwamba hata katika yale
mambo ambayo kwayo tulikwisha kuonyesha kwamba tunaanza kukomaa,
tumefanikiwa kupata mbinu za kuturudisha uchangani.
Kwa mfano, miaka 50 ya Uhuru ni muda mrefu kwa jamii yo yote ile
kuwa inatambua ni yapi matatizo yake yanayoisababishia unyonge, na ni
nini inahitaji ili kujikomboa kutoka unyonge wa umasikini, ujinga na
maradhi.
Utambuzi wa aina hii ni jambo la msingi mno, hata kama ufumbuzi
utachukua muda mrefu ujao. Utambuzi huo unasaidia kuweka misingi ya
kimkakati na hatua za kwanza za mbinu za utekelezaji wa malengo hayo
ya kimkakati.
Tunajua kwamba misingi hiyo ilikwisha kujengwa na Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere akisaidiwa na wazalendo wa kweli waliokabidhiwa
majukumu wakati ule. Inawezekana kwamba wale vijana wasiopenda kuisoma
nchi yao watakuwa hawajui hawa wazalendo ni akina nani waliomsaidia
Nyerere kuweka misingi hiyo, lakini haiyumkiniki kwamba hata watu wa
rika langu nao wanajifanya hawajui au hawakumbuki. Binafsi naamini
kwamba hawataki, ama kwa sababu wanayo maslahi katika kutokumbuka au ni
kutokana ule uvivu wa kufikiri tuliojijengea.
Tungekubali kuzisumbua kumbukumbu zetu kidogo tu tungeweza
kuwatambua akina Amir Jamal, Amon Nsekela, Dickson Nkembo, Clement G
Kahama, Derek Bryceson, Obeid Katikaza, Gabrieli Mawala, Cleopa Msuya…
na wengine kama hao, pamoja na wale waliokuwa vijana, akina Bakari
Mwapachu, Omari Abebe, Basil Mramba, Mbaruk Mwandoro na kadhalika.
Baadhi yao wamekwisha kututoka, na baadhi ya walio bado hai wanaweza
kuonekana leo kama vile hawajawahi kuwa na thamani yo yote kwa sababu
zama zao zimepita. Hata hivyo ni watu waliofanya kazi kubwa ya kuweka
misingi fulani kama walivyoelekezwa na bosi wao, Nyerere.
Kazi waliyoifanya wakati ule ilitakiwa iendelezwe na kizazi cha
vijana wa leo, iboreshwe na ipelekwe kwenye viwango vya juu zaidi,
lakini kwa sababu za upuuzi ambao nimekuwa nikiujadili, hilo
halikufanyika, na wala sioni dalili kwamba watawala wetu wanalielewa
hilo.
Hali hii ya kutokuthamini urithi wetu imetufanya sasa tutafute
walezi wengine badala ya baba yetu, na walezi hawa ( ambao kwa hakika
hawawezi kuwa na uchungu nasi) wanatuona kama “mazuzu” wa kutumiwa na
watu wenye akili.
Wanatuona kama punguani kwa jinsi tunavyoweza kuendelea kuwa
“omba-omba” miaka 50 baada ya Uhuru wakati tunazo rasilimali ambazo wao
wanazimezea mate.
Nimewasikia, kwa mshangao mkubwa, watawala wetu wakitamka kwamba
hawajui ni kwa nini nchi yetu ni masikini baada ya miaka yote hii na
ikiwa na rasilimali zote hizi. Huko kutotambua ndiyo sababu mojawapo
kubwa ya hali tuliyo nayo.
Haiyumkiniki kwamba mtu anaweza kugombea uongozi wa nchi au jamii,
tena kwa juhudi kubwa na kwa kuahidi mambo lukuki, halafu baada ya kuwa
ameingia madarakani akatangaza kwamba wakati wote huo alikuwa hajui
matatizo ya jamii yake. Nini kilimsukuma kugombea?
Pasipo na shaka akilini mwangu, sababu moja kubwa iliyotufanya
tukwame kiasi hiki imekuwa ni upuuzi wa uongozi na udhaifu wa watawala,
vikiambatana na uwezo na utashi mdogo mno wa raia kuwasaili viongozi
watawala wao na kusaili kila kilichowazunguka.
Tumefanikiwa kujenga jamii ya watu wasio na uwezo wa kusaili mambo
ya msingi kabisa, na wasiotaka kuwasaili wale waliowakabidhi hatamu za
uongozi, hata pale hao waliokabidhiwa hatamu hizo ni dhahiri kwamba
wanazitumia vibaya; na matokeo yake ni kwamba wanawaumiza hao hao
waliowaweka madarakani, na hao wanaoumizwa hawana la kufanya.
Kukosekana kwa utamaduni wa kusaili mambo yanayotuzunguka ndiko
kunatufanya tuendelee kuamini kwamba binadamu anaweza kupaa kwa ungo;
mwili wa albino una nguvu za miujiza; mtu anaweza kugeuka fisi na fisi
akageuka mtu; kumbaka mtoto mchanga kunatibu Ukimwi…na ujinga mwingine
wa aina hiyo.
Jamii isiyosaili mambo ni jamii ya wajinga, na wajinga wakisha kuwa
wengi ndani ya jamii, hata weledi wachache ndani ya jamii hiyo hawafui
dafu: watanyongwa.
Ndiyo maana tunapiga kelele siku zote kuhusu elimu bora, na elimu
bora si ile ya kumeza “maarifa” bali ni ile inayomwezesha mtu kusaili
mambo yanayomzunguka, kuuliza maswali ili apate majibu na kuuliza
maswali kuhusu majibu anayopewa, na siku zote kuendelea kusaili hata
yale mambo aliyodhani kwamba aliyaelewa awali. Ndivyo wenzetu
walivyoendelea, na ndiyo sababu wako waliko nasi tunaendelea kurejea
tulikotoka.
Bila shaka tunahitaji kuondokana na upuuzi na ujinga tulimozama
iwapo tunataka kupiga hatua za kwenda mbele badala ya hizi za kurudi
nyuma tunazozipiga kwa kasi leo hii (kwa sababu ni kweli tunarudi nyuma
kwa kasi).
Mahali pa kuanzia ni mwanzo, na mwanzo daima ni uongozi wa
kisiasa. Siasa safi zitazaa mazingira safi ya watu kufanya kazi za
kuleta maendeleo katika nyanja zote. Siasa hovyo zitajenga mazingira
hovyo vivyo hivyo, ambayo yataendelea kutuzamisha katika upuuzi na
ujuha.
Siasa zetu hazina budi kuwa na misingi ya usaili wa masuala yote
yanayotuzunguka, na ziachane na unafiki wa wale wanaodhani kwamba
kutosaili jambo au mtu ndio uaminifu na nidhamu.
Tukumbuke, wale wanaodhani viungo vya mwili wa albino vinaleta
utajiri, au kwamba ungo ni helikopta, msingi wao mkuu ni kushindwa
kusaili mambo na watu.
Katika siasa kushindwa kuwasaili wale waliokabidhiwa madaraka ya
kuendesha jamii, au kushindwa kusaili miundo, mifumo na michakato
inayoendesha jamii, ni ushirikina mwingine ambao matokeo yake ni
kuidumaza jamii yetu. Htuna budi kupambana na dalili zo zote
zinazotusukuma kutokomoea zaidi katika nakisi ya usaili.
Ndiyo maana napingana moja kwa moja na baadhi ya mambo yanayotamkwa
na kufanywa na baadhi ya wakuu wa asasi za utawala nchini, ikiwa ni
pamoja na wakuu wa shughuli za Bunge.
Ni kama vile wakuu hawa wa Bunge, pamoja na Spika na wasaidizi wake,
wamo bungeni kuhakikisha watawala hawasailiwi, hawadadisiwi na
hawakosolewi. Niliangalia kwa mshangao mkubwa ubishi kati ya Spika na
mbunge aliyesema kwamba, pamoja na uzembe na upuuzi wa asasi nyingine,
alibaini pia “udhaifu wa Rais,” na hili likawa ni tatizo kubwa
lililositisha shughuli za Bunge kwa muda na likawa ni chanzo cha gumzo
nchini.
Mimi najiuliza, iwapo mbunge wa upinzani atazuiwa kusema kwamba
Rais, ambaye ni kiongozi wa chama tawala (ndiyo kusema chama
anachokipinga mbunge huyo) ni dhaifu sasa aseme nini? Amsifu Rais kwa
umahiri, ukakamavu na ushujaa? Apendekeze kwamba Rais abakie madarakani
maisha, na chama chake kisipingwe? Kazi ya mbunge wa upinzani ni nini
hasa?
Nadhani ni kutokana na ukali wa Spika kuhusu “udhaifu” wa Rais ndiyo
ofisa mwandamizi serikalini akasimama bungeni kwa ukali kumshambulia
mbunge aliyesema kwamba baadhi ya majaji hawafai na kwamba uteuzi wao
ulikuwa wa kutiliwa shaka.
Ndipo nikatambua kwamba tunalo tatizo la msingi kuliko nilivyodhani
mwanzo. Tatizo hilo ni la kifalsafa katika mfumo ambao msingi wake wa
kidhana ni kwamba mkubwa hatiliwi shaka, na mambo yalivyo ndivyo
yalivyo, na hakuna bora zaidi ya yalivyo.
Chanzo: Raia Mwema
Friday, July 20, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment