"NI saa 12:45 asubuhi, bado kiza kimetanda katika eneo hili la Msitu wa
Mabwepande. Mbele yangu namwona mtu akiwa amekaa chini, pembeni ya
barabara akiwa amelowa damu mwili mzima.
"Ninapomkaribia nasikia
sauti ya mtu huyo ikisema kwa taabu; naomba msaada jamani… naomba msaada
jamani, hivi ndivyo anavyoanza kusimulia Juma Mgaza Abdallah, mtu wa
kwanza kumwona Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven
Ulimboka baada ya kutekwa, kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Mabwepande
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Abdallah, anasema mara
baada kumwona daktari huyo akiwa katika hali hiyo, alijaribu kumkokota
kumtoa eneo hilo, lakini alishindwa kutokana na hali mbaya aliyokuwa
nayo.
Baada ya hapo, aliamua kusubiri mtu mwingine apite eneo hilo ili amwombe wasaidiane kumpeleka Kituo cha Polisi Bunju.
Anasema
muda mfupi baadaye aliona gari likija mbele yao, akalinyooshea mkono
kulisimamisha. Liliposimama, akamweleza dereva hali aliyokuwa nayo Dk
Ulimboka na kwamba anahitaji msaada wa haraka.
Abdallah ambaye
hadi wakati huo alikuwa hamfahamu mtu ambaye alikuwa akimsadia kuwa ni
kiongozi wa madaktari kutokana na sura yake kuvimba, anasema
walimwingiza katika gari hilo na kumpeleka Kituo Kidogo cha Polisi
Bunju.
Anasema, Dk Ulimboka wakati huo alikuwa akiendelea kuvuja
damu katika baadhi ya majeraha yake huku akiwa hana suruali na kubaki na
bukta tu, huku akizungumza kwa taabu.
Kituo cha Polisi Bunju
Baada ya kumfikisha kituoni hapo, walitoa maelezo namna walivyomwokota na kumsaidia kumfikisha hapo.
Polisi
baada kumhoji Dk Ulimboka, aliwatajia namba ya simu ya rafiki yake
aitwaye Dk Deo. Walipompigia na kumweleza tatizo hilo, aliamua moja kwa
moja kwenda Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, kutoa taarifa hizo na
hatimaye kuandamana na watu kadhaa kutoka hapo akiwamo Mkurugenzi wake,
Hellen-Kijo Bisimba.
Wawasili kituoni
Mratibu wa Mtandao
wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania wa kituo hicho, Onesmo
Olengurumwa, anasema waliwafika Polisi Bunju saa 3:36 asubuhi na kumkuta
Dk Ulimboka akiwa amekalishwa kwenye benchi huku damu ikiwa imeganda
kwenye majeraha mwilini.
Olengurumwa anasema waliwahoji polisi
waliokuwa kituoni hapo kwa nini wakae na mtu aliyeumia kiasi hicho muda
mrefu bila ya kuita gari la wagonjwa kumchukua ili kuwahi kupatiwa
matibabu.
Olengurumwa anasema polisi walisema kwamba, walikuwa wanawasubiri ndugu zake wafike.
Baada
ya muda mfupi, akiwa ameingizwa kwenye gari kupelekwa hospitali, Dk
Ulimboka aliomba maji ya kunywa akisema ana kiu sana, lakini alipopewa,
alikunywa kidogo akashindwa.
Anasema wakiwa njiani, alikuwa
akilalamika kuwa anasikika maumivu makali huku akisisitiza kuwa tukio la
kutekwa na kupigwa lilikuwa la kumuua.
"Jamani hawa watu
walitaka kuniua walikuwa wamepanga kuniua," alisikika mara kwa mara
akisema Dk Ulimboka wakati anapelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
kupatiwa matibabu.
Maelezo ya Dk Ulimboka
Baada ya Dk
Ulimboka kuokotwa aliweza kuzungumza na kurekodiwa muda mfupi baada ya
kutolewa msituni na mazungumzo yake yalikuwa hivi;
“Nilikamatwa
na watu hao usiku wa Jumanne nikiwa maeneo ya Leaders Club, Kinondoni na
daktari mwenzangu baada ya kupigiwa simu na mtu mmoja ambaye alidai
kuwa anafanya kazi Ikulu.
“Kuna jamaa mmoja anafanya kazi Ikulu,
kama siku tatu mfululizo alikuwa akitaka kukutana na mimi ila
nilishindwa kukutana naye kwa kuwa nilikuwa na kazi nyingi na wakati
mwingine mpaka usiku,” alisema Dk Ulimboka.
Huku akizungumza kwa taabu kutokana na mdomo wake kuvimba, alisema siku hiyo mtu huyo alimpigia tena simu na kumtaka wakutane.
“
Jana (Jumanne) alinipigia simu na nikamwambia daktari mwenzangu twende
tukaonane naye, wakati huo alitueleza kuwa alikuwa maeneo ya Kinondoni
Stereo,” alisema Ulimboka na kuongeza:
“Tulipofika maeneo hayo
tukampigia simu na akatueleza kuwa alikwisha ondoka, baadaye tukamweleza
sehemu tulipo mimi pamoja na mwenzangu.”
Alisema kuwa, wakati anakutana na mtu yule maeneo ya Leaders Club, hakuwa na amani.
“Kwa kweli siku ile nilivyoonana na mtu yule sikuwa na amani kabisa ya kukaa eneo lile,” alisema Dk Ulimboka.
Alisema kuwa wakati wakiendelea na maongezi ya kawaida, bado aliendelea kuwa na mashaka na mtu yule.
“Katikati
ya maongezi nikaona ameanza kuzungumza na simu, kila tukitaka kuagana
alikuwa akizungumza na simu, sijui nini kilikuwa kinachelewesha sisi
kuagana,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“ Ghafla walitokea watu kama watano na kusema kuwa hawana tatizo na mtu yeyote katika eneo hilo isipokuwa mimi.
Wakati sijakaa sawa, waliniburuza hadi barabara ya lami kwa kuwa eneo hilo lilikuwa karibu na barabara.”
Aliongeza,
“Nilipowauliza wananipeleka wapi, wakaniambia kuwa mimi nasumbua sana
na nitajua hukohuko, waliniingiza katika gari jeusi, lakini halikuwa na
namba. Niliwauliza kosa gani nimefanya? Hawakunijibu kitu na kusema, we
twende utajua hukohuko.’’
Alisema alipokuwa ndani ya gari hilo
watu hao walimpiga na kwamba walipofika maeneo ya Victoria, walichukua
sweta nyeusi na kumfunga usoni, jambo lililomfanya ashindwe kuona
kinachoendelea ikiwa ni pamoja na alikokuwa akipelekwa.
“Walinipiga
mateke ya mbavuni, wakati mwingine walitumia vitako vya bunduki, kila
nilipokuwa najaribu kuangalia ninapokwenda nilishindwa,” alisimulia Dk
Ulimboka.
Alisema kuwa watu hao walimpeleka katika nyumba moja
ambayo hakujua iko sehemu gani ambapo walimshusha na kuanza kumshambulia
kwa mateke mfululizo kila sehemu ya mwili. Wakati huo, wote
walimshinikiza awaambie nani yupo nyuma ya mgomo wa madaktari.
“Tangu
saa sita usiku mpaka saa 9:00 alfajiri walikuwa wananipiga tu, kuna
wakati nilijaribu kukimbia wakapiga risasi juu nikasimama na sikuweza
kukimbia tena,” alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
“Nilisimama,
wakaendelea kunipiga, niliwasikia wakisema ama wanichome sindano ya sumu
nife au kunikanyaga na gari. Baadaye wakaanza kuning’oa meno na kucha
kwa kolea huku wakinilazimisha kusema nani yupo nyuma ya mgomo wa
madaktari."
Alisema kuwa, watu hao walikuwa na bunduki kubwa ambayo hakuweza kuitambua ni aina gani.
“Waliniambia kuwa ninajua ninachokifanya hivyo wanaweza kunichoma sindano ya sumu nife au wanikanyage na gari nife,” alisimulia.
Dk
Ulimboka alisema kuwa awali hakuwa na shaka na watu hao kwa kuwa
alidhani ni polisi, lakini baadaye alishindwa kuwaelewa kwani watu hao
walimchanganya.
“Sikuweza kuwatambua ila naweza kusema ni askari,
walipokuwa wananipeleka niliwauliza mnanipeleka wapi na wakati huo
nilikuwa sioni mbele ila ilikuwa kama maeneo ya Mwenge hivi,” alisema Dk
Ulimboka.
Alisema kuwa baadaye alipoteza fahamu na hakuweza kuona chochote zaidi ya kusikia sauti za watu hao kwa mbali.
“Nilikuwa
sioni na nilipoteza fahamu nikawa nasikia tu wakinibeba, gari
lilitembea muda mrefu, sikujua ni wapi tunakwenda, kumbe ndio huko
Mabwepande,” alisema.
Alisema kuwa walifika maeneo ya barabara ya vumbi na baadaye wakamshusha na kumbeba hadi msituni.
“Waliniburuza
na kuniacha huko na muda wa saa kumi alfajiri ndipo nikazinduka na
kuanza kujiburuza kuelekea barabarani ambako nilisaidiwa na mtu mmoja
ambaye simtambui,” alisema Dk Ulimboka.
Chanzo: Mwananchi
Sunday, July 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment