NCHI imetikiswa. Mgomo wa walimu ulioanza jana katika sehemu mbalimbali
nchini, umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya elimu huku kukiwa na
taarifa za matukio yasiyokuwa ya kawaida yaliyoambatana na mgomo huo
usio na ukomo.
Katika sehemu mbalimbali nchini, walimu
waliripotiwa kugoma kwa kutoingia madarasani na wengine walifika kazini
na kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka hali iliyosababisha
wanafunzi kurandaranda ovyo katika sehemu za miji iliyo karibu na shule
hizo.
Mjini Dodoma ,wabunge jana walimbana Naibu Spika, Job
Ndugai wakitaka shughuli za Bunge zisitishwe ili kujadili mgomo wa
walimu ambao umeanza rasmi jana nchi nzima, na kuziacha shule nyingi
zikiwa na walimu wakuu na wakuu wa shule pekee.
Hata hivyo,
Ndugai alisema Bunge lisingeweza kujadili suala hilo kwani tayari
Serikali ilikuwa imelifikisha mahakamani baada ya kushindwa kuafikiana
na walimu katika ngazi ya usuluhishi.Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa amesema Serikali itafuta
mishahara kwa walimu walioitikia mwito Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
wa kushiriki mgomo ambao alisema siyo halali.
Katika mkutano wake
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Dk Kawambwa pia aliwaonya
walimu ambao alisema wamekuwa wakiwabughudhi wenzao ambao waliamua
kwenda kazini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo akiwa Mjini Morogoro aliwaagiza wakuu wa shule za
msingi na sekondari mkoani humo kuandaa orodha ya majina ya walimu
wasiofika kazini Julai 30 na waifikishe kwa maofisa elimu wa wilaya
kabla ya saa 2:00 asubuhi ya Julai 31.
Waandishi wetu katika
sehemu mbalimbali nchini pia waliripoti kwamba katika baadhi ya shule,
wanafunzi waliruhusiwa kurejea nyumbani mapema kwa maelezo kwamba
hakukuwa na masomo.Hali hiyo ilizua kizaazaa kwani katika baadhi ya
mikoa wanafunzi walicharuka na kuitisha maandamano hadi katika ofisi za
maofisa elimu wa wilaya, wakitaka Serikali iingilie kati mgomo huo ili
waendelee kusoma.
Kadhalika, baadhi ya viongozi na watendaji wa
Serikali walinukuliwa wakitoa matamko ya kuwasihi au kuwaamuru walimu
warejee madarasani, kauli ambazo hata hivyo, hazikubadili uamuzi wa
walimu hao.
Wanafunzi waandamana
Maandamano ya wanafunzi
yaliripotiwa katika Mji wa Tunduma, Mbeya ambako polisi walitumia mabomu
ya machozi kuwadhibiti wanafunzi.
Wanafunzi wa shule mbalimbali
za msingi katika Wilaya ya Mbozi mkoani humo waliandamana wakidai haki
ya kufundishwa. Hata hivyo, maandamano hayo yaliingiliwa na vibaka ambao
baadaye walivunja ofisi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kuiba mali
kadhaa kisha kuchoma nyaraka zilizokuwemo.
Tukio hilo lilitokea
asubuhi wakati wanafunzi wa shule 14 za msingi zilizopo katika
halmashauri ya Tunduma walipojikusanya na kufanya maandamano hadi
nyumbani kwa diwani na baada ya kumkosa walielekea kituo cha polisi na
baadaye ofisi katika hizo.
Katika manispaa ya Temeke, Dar es
Salaam zaidi ya wanafunzi 400 wa shule nne za msingi wameandamana hadi
katika Ofisi ya Ofisa Elimu wa Manispaa hiyo kupinga mgomo huo.
Wanafunzi wao ambao waliandamana walitoka katika Shule za Msingi Bwawani, Mbagala Kuu, Mtoni Kijichi na Maendeleo.
Wilayani
Tarime, Mara wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi jana waliandamana
hadi Ofisi ya Ofisa Elimu wa Wilaya hiyo na zile za CWT, wakidai haki
yao za kupata elimu baada ya walimu kugoma kuingia madarasani na kisha
kuwataka wanafunzi kurejea nyumbani.
Wanafunzi hao walisikika
wakiimba na baadaye kuzungumza mbele ya Ofisa elimu wa Wilaya, Emmanuel
Johnson kwamba kitendo cha walimu kugoma kufundisha kinawaathiri wao,
hivyo waliitaka Serikali kuwalipa walimu madai yao ili waendelee na
kuwafundisha.
“Watoto tunataka haki zetu, Watoto tunataka kupata
elimu, watoto tunataka kusoma tunaomba walimu walipwe madai yao
tuingie madarasani, watoto tusinyimwe haki yetu ya kupata elimu walimu
wanapogoma waathirika ni sisi wanafunzi Serikali tatueni mgomo wa
walimu,” walisema wanafunzi hao.
Johnson aliwatuliza wanafunzi hao na
kuwaahidi kwamba atatatua tatizo hilo, hivyo kuwataka kurejea shuleni
leo kuendelea na masomo.
Mkoani Pwani mgomo wa walimu
ulisababisha maandamano yaliyowahusisha wanafunzi wa shule za msingi
kadhaa katika Wilaya za Kisarawe, Mkuranga, Bagamoyo na Kibaha waliokuwa
wakiishinikiza Serikali kusikiliza madai ya walimu ili wao waweze
kupata haki yao ya kufundishwa.
CWT wanena
Kaimu Katibu Mkuu
wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Olouch alisema mgomo wa
walimu umefanikiwa kwa asilimia 90 nchi nzima na kwamba walimu katika
mikoa mbalimbali hawakwenda kazini ikiwa ni hatua ya kushinikiza kupewa
haki yao.
“Tunawashukuru walimu kwa kuunga mkono azimio lao
ambalo walilipigia kura la kufanyika kwa mgomo na kubaki nyumbani bila
ya kwenda kazi hadi pale Serikali itakaposikiliza matatizo yao” alisema
Oluoch na kuongeza:
“Mgomo huu ambao umeanza leo (jana)
hautahusiana na Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika usiku wa
kuamkia Agosti 26, mwaka huu.”
Oluoch alisema kikomo cha mgomo huo
ni pale itakapotolewa taarifa na Rais wa CWT, Gratian Mukoba na si mtu
mwingine yeyote wala Serikali.
“Walimu wanatakiwa kutambua kuwa
mgomo huu utaendelea hadi pale Rais Mukoba atakapowatangazia
kinachoendelea hivyo kwa hivi sasa waendelee na mgomo huu,” alisema
Oluoch.
Serikali yang’aka
Akizungumzia mgomo huo Dk Kawambwa
alisema: “Tutatumia sheria kwa kushikilia malipo ya mishahara kwa walimu
wanaogoma na tutatumia pia sheria kuwaadhibu walimu wanaowabughudhi
wenzao kwa kuwalazimisha wagome.”
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya
Kazi ya mwaka 2004 ambayo vyama vya wafanyakazi vinaitumia kufanikisha
migomo, Kifungu cha 83(4) kinaeleza kwamba mfanyakazi hatapaswa kulipwa
mshahara katika kipindi chote ambacho itatokea amegomea utoaji huduma
kwa umma.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Dk
Kawambwa alisema Kuwa Serikali itahakikisha kwamba inawalinda walimu
wote ambao hawaungi mkono mgomo huo aliodai ni haramu kwa kuwa suala
hilo kwa sasa linashughulikiwa mahakamani.
Katika hatua nyingine,
Dk Kawambwa aliwaonya wazazi kuhakikisha kwamba watoto wao hawatumiwi
na wagomaji kwa kuhimizwa kufanya maandamano na vurugu.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment