WANASAYANSI mbalimbali wanaoendesha tafiti mbalimbali za kutafuta
tiba na chanjo ya Ukimwi, wameitangazia dunia kuwa hatua waliyofikia
sasa wanauona ugonjwa huo ‘siyo hatari tena’ kwa sababu wanazo silaha
zote za kuweza kukabiliana nao.
Ila wakasema,
kinachowakwamisha ni ukosefu wa fedha ambazo zinahitajika katika
kuendeleza tafiti na kuweka sera mpya za kukabili Virusi Vya Ukimwi
(VVU) duniani.
Hayo yalibainika kwenye siku ya
pili ya Mkutano wa 19 wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini
Washington DC, Marekani na unahudhuriwa na watu zaidi 22,000 miongoni
mwao wakiwamo wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano
dhidi ya ugonjwa huo toka karibu kila kona ya dunia.
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kitengo cha
Habari cha Mkutano huo na gazeti hili kufanikiwa kupata nakala yake,
ilieleza kwamba jopo la wanasayansi nguli duniani walikiri kuwa
wamefanyia VVU utafiti wa kutosha ndiyo maana wanatamba kuwa
wamefanikiwa katika kuvidhibiti.
“Kwa sasa
tunazo silaha zote za kisayansi kumalizia mbali gonjwa hili la Ukimwi.
Kilichobaki ni kutumia kikamilifu utaalamu huu katika fursa hii tuliyo
nayo,” alisema Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano
dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira.
Kiongozi
huyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Mkutano huo akitokea nchini Uganda,
aliongeza: “Kufanikisha hilo ni lazima tukubali kubadili mfumo kwa maana
kwamba kuweka sera mpya zitakazowezesha kuokoa kundi linaloathirika
zaidi na ugonjwa huu.”
Dk Katabira alifafanua:
“Kinachohitajika ni kuweka mfumo utakaowashirikisha wafadhili na watunga
sera katika kuweka mpango mzuri wa pamoja tuweza kulimaliza tatizo kwa
silaha hizi za kisayansi.”
Naye Mtaalamu wa
Tiba katika Chuo Kikuu cha California, Profesa Diane Havlir alisema:
“Ujumbe wangu kwenu, hasa kwa watunga sera ni kwamba: endeleeni kuwekeza
katika mipango ya kisayansi.”
Kwenye mkutano
huo walishiriki pia wanasayansi wenye dawa na ushahidi unaoonyesha kuwa
katika miaka ya karibuni zimeonyesha dalili nzuri za kutibu Ukimwi na
kifua kikuu (TB).
Wataalamu wengi wa afya
waliunga mkono kauli hiyo wakisema kwa sasa kuna uelewa mkubwa wa
kitaalamu juu ya muundo na tabia ya VVU hivyo ni rahisi kwao kutengeneza
dawa kwa ajili ya kuzuia, kutibu na chanjo.
Tafiti za awali
Kauli
ya wanasayansi hao imekuja baada ya miaka 30 ya kipindi kigumu cha
kutafiti namna ya kupata chanjo au tiba ya ugonjwa huo ambao umeua
mamilioni ya watu duniani, hususan wataalamu na nguvu kazi inayohitajika
kuimarisha uchumi.
Waligundua VVU mwaka 1981
na ilikuwa vigumu kupata dawa ya kuviua kwa sababu ya tabia zao na uwezo
wa kujigeuza kuwa sehemu ya mwili na kutumia selikinga kuzalisha virusi
wengine.
Wanasayansi hao walitoa kauli hizo za
matumaini kukabili VVU mbele ya viongozi mashuhuri wa kisiasa, akiwemo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton na Rais wa Ufaransa,
François Hollande.
Mtaalamu anayesimamia
mipango ya afya Ikulu ya Marekani, Profesa Antony Fauci, ambaye piya ni
Mkurugezi wa taasisi ya nchi hiyo ya Utafiti wa Magonjwa ya Kuambukiza
na Mzio (NIAID), alikuwa miongoni mwa waliohutubia na kusifu hatua
iliyofikiwa na wanasayansi duniani.
Ofisa Mkuu
na Rais wa Taasisi ya Mapambano ya Ukimwi nchini Marekani, Phill Wilson
aliweka bayana kuwa pamoja na ugonjwa huo kuonekana tishio hasa kwa
nchi zinazoendelea, hakuna nchi, hata zile tajiri, ambazo zinaweza
kutamba haziathiriki na tatizo hilo.
Kwa hivyo
akasema mikakati na sera mpya za kisayansi zinahitajika dunia nzima,
hivyo akawataka wanasayansi hao ‘kuanika hadharani silaha zao’ ili
zianze kutumika ulimwenguni kote.
Mkurugenzi wa
Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mapambano ya Ukimwi (UNAIDS), Sheila
Tlou aliwataka wataalamu hao kuweka mkakati mzuri utakaowezesha silaha
hizo za kisayansi kuelekezwa katika nchi maskini hasa barani Afrika.
Wanasayansi
hao wamekuja na kauli hizo za matumaini wakati ambapo tayari wamefanya
tafiti mbalimbali na kugundua tabia za VVU ikiwa ni pamoja na vitu
ambavyo vinaviwezesha kushambulia seli nyeupe za damu, maarufu kwa jina
la CD4, ambazo ni sehemu ya kinga ya mwili wa binadamu.
Licha
ya tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa kuna kila dalili ya kupatikana kwa
chanjo, miaka michache iliyopita, waligundua moja ya dawa zinazotumika
kupunguza makali ya VVU (ARV) ijulikanayo kama Truvada, yenye uwezo wa
kumkinga mwathirika kumwambukiza mpenzi wanayeshiriki naye tendo la
ndoa.
Wiki chache zilizopita, Mamlaka ya
Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) iliidhinisha Truvada, ambayo ilianza
kutumika sehemu mbalimbali duniani tangu mwaka 2004, kuwa ni tiba ya
kuzuia kuenea kwa Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Kwa
mujibu wa maelezo ya FDA, mwathirika anayetumia dawa hiyo anaweza
kujamiiana na mwenza wake ambaye hana VVU bila kutumia kondomu na
hatomwambukiza.
Matokeo ya utafiti huo wa ARV
yaliwahi kuchapishwa kwenye gazeti hili toleo la Februari 12, mwaka huu.
Kwa mujibu wa FDA, Truvada inatarajia kuanza kutumika na kusambazwa
duniani katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment