KAMBI ya upnzani Bungeni imelitaka Bunge kutumia mamlaka yake kuchukua hatua za kumshitaki Rais Jakaya Kikwete kwa mujibu wa ibara ya 46A ya Katiba kwa kushindwa kuihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Muungano kama kiapo cha kazi yake kinavyomtaka.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Msemaji rasmi wa Kambi ya Upinzani, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Tundu Lissu wakati akichangia hoja ya makadirio ya matumizi na mapato ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Lissu alisisitiza kuwa Rais Kikwete ameshindwa kuihifadhi, kuitetea na kuilinda Katiba ya Muungano kwa kuiacha na kuiruhusu Zanzibar kufanya mabadiliko ya Katiba yaliyovunja kwa kiasi kikubwa makubaliano ya Muungano.
Alisema Kikwete si tu kwamba aliponzwa na hofu ya kuwaudhi Wazanzibari, lakini pia alishiriki katika kufanya mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ambayo inavunja makubaliano ya Katiba ya Muungano.
Kwa mujibu wa Lissu, mabadiliko ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeweka vifungu ambavyo vinakiuka misingi mikuu ya makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano na haviwezi kubadilishwa bila kura ya maoni ya Wazanzibari.
“Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, masuala kama Tanzania ni nchi moja au la, majeshi ya ulinzi, polisi, n.k. ambayo yamekuwa mambo ya Muungano kwa mujibu wa makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano si mambo ya Muungano tena hadi hapo wananchi wa Zanzibar watakapoamua kwa kura ya maoni kuyarudisha kwa mamlaka ya Muungano. Huku, Mheshimiwa Spika, ni kutangaza uhuru wa Zanzibar bila kutaja neno uhuru! Huku ni kuua Muungano bila kukiri hadharani!
“Mheshimiwa Spika, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, hatuna tena nchi moja inayozungumzwa katika Katiba ya Muungano bali tuna nchi mbili. Kwa mtazamo huo huo, masuala ya ulinzi na usalama, polisi, n.k. si tena Mambo ya Muungano kwa sababu sasa kila nchi ina majeshi yake na kila moja ina Amiri Jeshi Mkuu wake,” alisema.
Lissu alisema kwa sasa kuna marais wawili, wakuu wa nchi wawili na viongozi wa serikali wawili, akidai mambo haya yote yanakiuka moja kwa moja makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano.
“Kwa upande mwingine, kwa mtazamo wa Katiba ya sasa ya Zanzibar, Rais wa Muungano hana tena mamlaka ya kugawa mikoa na wilaya kwa upande wa Zanzibar, na wala hawezi kumshauri tena Rais wa Zanzibar anapoteua wakuu wa mikoa wa Tanzania Zanzibar.
“Aidha, Mahakama ya Rufani ya Tanzania licha ya kuwa moja ya mambo ya Muungano kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, haina tena mamlaka ya kusikiliza na kuamua rufaa zinazohusu haki za msingi na uhuru wa mtu binafsi zinazotoka Zanzibar,” alisema.
Lissu alisema wakati Zanzibar ikifanya mabadilko ya Katiba, Rais Kikwete na Chama cha Mapinduzi (CCM), walikuwepo lakini hawakuchukua hatua zozote kuzuia na kuilinda Katiba ya Muungano kama alivyowahi kufanya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
“Kwa wale wanaodai kwamba wana-Uamsho wanataka kuvunja Muungano kwa sababu tu ya kudai kura ya maoni, tunaomba tuwakumbushe yafuatayo: “Kwanza, kwa mujibu wa Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: ‘Huko nyuma baadhi ya viongozi wa Zanzibar wapinzani wa Muungano wamewahi kudai tufanye referendum kwa Zanzibar kuhusu Muungano.
Tukakataa kwa sababu safi kabisa.’ Hapa Mwalimu alikuwa anamzungumzia aliyekuwa Rais wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe, Waziri Kiongozi Ramadhani Haji Faki na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Bashir Ebassuah Kwaw Swanzy waliong’olewa madarakani mwaka 1984 baada ya ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa,’’’ alisema.
Kwa mujibu wa Lissu, kifungu cha 5(1)(a)(iii) na (iv) cha Sheria ya Muungano kinataja ‘ulinzi’ na ‘polisi’ kama sehemu ya mambo kumi na moja ya Muungano. Na hivyo ndivyo inavyosema aya ya (iv)(c) na (d) ya Makubaliano ya Muungano.
“Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, katika kile kinachoonekana kama hojaji kubwa ya msingi huu wa Makubaliano ya Muungano na Sheria ya Muungano, ibara ya 121 ya Katiba ya sasa ya Zanzibar imeunda majeshi ya Zanzibar inayoyaita ‘Idara Maalum.’
“Mheshimiwa Spika, si tu kwamba Katiba mpya ya Zanzibar inaanzisha majeshi bali pia inamfanya Rais wa Zanzibar kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi hayo. Kwa mujibu wa ibara ya 123(1) ya Katiba hiyo, “Rais atakuwa Kamanda Mkuu wa Idara Maalumu na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa (la Zanzibar), kinafaa.” Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 123(2), mamlaka ya Rais wa Zanzibar chini ya ibara ndogo ya (1) yanaingiza “... uwezo wa kutoa amri ya kufanya shughuli yoyote inayohusiana na idara hiyo kwa manufaa ya taifa.
“Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, haya ni mamlaka ya kutangaza au kuendesha vita ambayo, kwa mujibu wa ibara ya 44(1) ya Katiba ya Muungano, ni mamlaka pekee ya Rais wa Jamhuri ya Muungano,” alisema.
Alisema katika mazingira ya sasa ambapo upande mmoja wa Muungano umejitangazia uhuru ni wakati muafaka kuanzishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika.
“Mheshimiwa Spika, katika mazingira ambayo upande mmoja wa Muungano si tu una Serikali kamili, Bunge kamili, Mahakama kamili, wimbo wa taifa, bendera ya taifa, na sasa una nchi kamili yenye mipaka na eneo la bahari linalojulikana, una majeshi yake na Amiri Jeshi Mkuu wake, huu ni muda mzuri kwa Serikali ya Tanganyika kuzaliwa upya,” alisema.
“Katika mazingira kama haya, Mheshimiwa Spika, upande wa pili wa Muungano unatakiwa kuwa na vitu vyote hivyo pia ili uweze kujadiliana na upande wa kwanza katika hali ya usawa.
“Huu ni wakati wa kurudishwa tena kwa Serikali ya Tanganyika kama ilivyopendekezwa na Tume ya Rais ya Chama Kimoja au Vyama vingi mwaka 1991 na Tume ya Kissanga mwaka 1998, na kama ilivyopendekezwa na kundi la wabunge 55 wa Bunge hili tukufu na kuungwa mkono na Serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi kabla ya hoja hiyo kutunguliwa na Baba wa Taifa mwaka 1993!” alisema.
Alisema CHADEMA inaungana na wote wanaoendelea kudai kuitishwa kura ya maoni ya wananchi ili waweze kuamua mustakabali wa taifa kwani kuendelea na kiini macho cha Muungano wakati serikali zote mbili na chama tawala cha CCM wanauvunja kivitendo, kutaliweka taifa kwenye njia panda.
Alisema kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka Watanzania waamue, kwa kura ya maoni, kama bado wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu lao ni ndio, ni muundo gani wa Muungano wanautaka.
“Kama, kwa busara zao, wataamua kwamba nusu karne ya Muungano inatosha basi itakuwa afadhali kwenda njia ya Czechoslovakia ya zamani kuliko kwenda njia ya Yugoslavia ya zamani, au Ethiopia na Eritrea au Sudan na Sudan Kusini,” alisema.
Mwanasheria Mkuu ampinga
Kuhusu madai ya Lissu kutaka Rais Kikwete ashitakiwe kwa kuvunja Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alimjibu akifafanua kuwa si kweli kwani hakuna sheria yoyote iliyovunjwa.
“Nikiri kuwa tamko hilo la kuridhia makubaliano ya Muungano sijaliona lakini Aprili 25 mwaka 1964 Baraza la Mapinduzi la Zanzibar lilipitisha makubaliano hayo na baadaye Bunge liliyaidhinisha,” alisema.
Jaji Werema alifafanua kuwa hata kama hakuona makubaliano hayo hiyo haiwezi ikawa hoja ya kusema Muungano haupo, akibainisha kuwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa kitendo cha nchi kuonesha dalili ni kwamba imekubaliana.
Alisema kuwa wengi wanaohoji kasoro za Muungano katika maeneo mengi nchini si kwamba wanaupinga bali wanataka mkataba wa makubaliano uwekwe wazi, jambo alilokiri kuwa linakosekana.
Kuhusu mabadiliko ya hivi karibuni ya Katiba ya Zanzibar ambayo Lissu alidai yamevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuitamka Zanzibar kuwa ni nchi, Jaji Werema alisema hayajavunja Katiba.
“Mabadiliko yaliyofanywa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar hayajavunja Katiba ya Muungano, Zanzibar kweli ni nchi, si dola wala Zanzibar si Jamhuri lakini ni nchi maana bila hivyo hakuna Muungano,” alisema Jaji Werema.
Chiligati anena
Chiligati ambaye alikwepa kujadili hoja ya kutaka Bunge lichukue nafasi yake kumshitaki Rais Kikwete, alisema hata kama italazimika kuundwa kwa serikali ya Tanganyika, bado itakuwa ni balaa jingine kiuchumi kwani uwezo wa kiuchumi wa kuendesha serikali tatu haupo na itakuwa mzigo mkubwa.
“Kufufua Tanganyika na Utanganyika ni kurudi nyuma na kuvunja Muungano na Watanzania wenye nia njema lazima tuukatae,” alisema.
Chiligati alisema muungano wa nchi mbili ndiyo zimelifikisha taifa hapa ilipo, na akakumbusha namna ambavyo baadhi ya mataifa yaliyoungana yalivyosambaratika kwa kuwa hawakuwa na muungano wa aina ya Tanzania.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment